Monday, May 2, 2016

VIJANA WAFUNGUKA MACHO KUHUSU KILIMO CHA MBOGA MBOGA NA MATUNDA





Japokuwa awamu ya tano ya uongozi wa Raisi John Pombe Magufuli umefanya mabadiriko mengi yanayokonga nyoyo za watanzania wengi bado kilimo kimebakia kuwa uti wa mgongo wa uchumiTanzania.
 
Hata hivyo mpaka sasa hajafanikiwa kuufuta usemi huu ambao umekuwa ukibakia kama ulivyo na ndivyo ilivyo kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, kikichangia takribani nusu ya Pato zima la Taifa na robo tatu ya bidhaa zote zinazouzwa nje ya nchi. Pamoja na kuzalisha chakula, kilimo vilevile kinatoa ajira kwa asilimia 80 ya Watanzania. 

Sehemu kubwa ya kilimo Tanzania ni cha wakulima wadogo-wadogo (small-holder farmers) ambao wengi wao hawatumii njia za kisasa na wengine mpaka leo hawajawahi hata kuzijua.
Takwimu za Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, zinaonyesha kuwa Tanzania, wakulima wake hulima hekta milioni 5.1 nchi nzima kila mwaka, na kati ya hizo asimilia 85 ni kwa ajili ya mazao ya chakula ikiwa ni pamoja na mazao ya mbogamboga na matunda, ambayo huzalishwa kwa wingi karibu katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani. 



Kilimo cha mboga na matunda kimekuwa maarufu nchini kwa sasa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji katika soko la ndani na nje, kuongezeka elimu kwa wakulima na watumiaji, upatikanaji kwa urahisi wa pembejeo na uwezeshaji unaofanywa na serikali pamoja na taasisi binafsi.

 Mikoa ya Kanda ya Kaskazini Arusha, Manyara, na Kilimanjaro kilimo hiki kimeanza kuwavuta kwa kasi makundi ya vijana na wanawake ambao sasa ndio wanaonekana kukivalia njuga  kilimo hicho hasa kufuatia uelimishaji na uhamasishaji unaofanywa na Taasisi zinazojishughulisha na utafiti na uuzaji wa pembejeo zinazohusu kilimo hicho.

Rijk zwaani imekuwa mstari mbele katika kuwapatia wakulima mafunzo ya kilimo cha mboga na matunda, pia kuwaaunga mkono wakulima wote wanapata mafunzo kwao kwa kuhakikisha wanapata mazao bora na masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi, pembejeo na madawa muhimu na ushauri wa kitalaamu unaotolewa na maafisa ugani wa shirika hilo. 

Mbali na shirika hilo pia AVRDC pia wamekuwa mstari wambele kuendeleza utafiti wa mbegu mbali mbalii za mbogamboga na kutoa elimu kwa makundi tofauti tofauti ya wakulima kuhusu kilimo bora cha mbogamboga na hata wakati mwingine kutoa mbegu bure kwa makundi hayo ili kuyawezesha makundi hayo.

Licha ya hivyo SEVIA pia ndio limekuwa shilika la kimbilio la wakulima baada ya wao kujidhatiti katika kutoa mafunzo yajinsi ya kulima kwa kutumia kilimo cha kisasa ambacho imeonekana ndio njia pekee ya mkulima kujikwamua kutoka katika kilimo kisicho na tija na kuwa kilimo cha tija.

Ally Materu (30) ambaye ni mkazi wa Moshi Mkoani Kilimanjaro, amekuwa akijishughulisha na kazi ya kupanda mlima na watalii bila kujua kuwa anaweza akafanya shughuli nyingine mpaka alipojiunga na kikundi cha “kijana jikwamue” ambao hivi karibuni walitembelea Rikj zwaani na kupata mafunzo ya kilimo ndipo alipotambua kuwa kuna fursa ambayo anaweza akaifanya na ikampatia kipato kikubwa kuliko hiyo aifanyayo. 

“Leo nimetambua ya kuwa nilikuwa najicheleweshea maendeleo yangu mwenyewe kwa ajiri ya kutegemeo upandaji mlima wakati kumbe kilimo kinaweza kikanitoa kirahisi nikidhamilia” alisema Ally. 

 Nae mwalimu Ole Lengai (29) mkazi wa kijiji cha Olkokola Mkoani Arusha ambaye alibainisha kuwa kilimo hicho kimekuwa “dawa” ya tatizo sugu la ajira nchini ambalo linawakabili vijana wengi. “Nilianza kilimo hiki miaka miwili iliyopita, baada ya kujifunza kwa kutembelea shamba darasa la AVRDC, kwa kweli kiuchumi hali yangu imebadilika sana kutokana na mazao ninayozalisha kama nyanya, na aina nyingine tofauti za mboga kuuzika kwa haraka na kuwepo kwa soko la uhakika hasa baada ya wanunuzi kujua ubora wa mazao yangu alisema Ole. 

“Vijana wengi wanalalamika kuwa hawana mitaji ya kuanzisha shughuli za kilimo, malalamiko yao hayana mantiki sana kwasababu vijana wengi wanamiliki vitu vya bei ya juu kama simu, laptop, nguo za thamani na wakati mwingine wanapatikana sehemu za starehe wakitumia pesa za kutosha kuanzisha mradi wa kilimo”Alisema Ally. 

Kwa mujibu wa Ole, kilimo cha mboga ni rahisi sana kwa sababu hakihitaji eneo kubwa la ardhi, na pia mazao ya aina hiyo hukomaa ndani ya mda mfupi na mkulima anakuwa ameshapata fedha za mauzo na kurudisha gharama zake. 

Akijitolea mfano yeye mwenyewe alisema alihamasika sana baada ya kutembelea shamba darasa na kuona vijana wanaolima pembezoni mwa shirika la AVDRC na kupata shuhuda kutoka kwao akaamua kukata shauri ya kuondokana na maisha ya kupoteza mda kwa kukaa vijiweni.
“Nilianza kwa kulima matuta mawili ya mnafu na baada ya kuuza na kupata faida ndipo nilipoamua kujidhatiti katika kilimo, hivi sasa nina shamba la hekari moja ambalo nililinunua mwenyewe baada ya kupata faida ya mboga mboga na sasa nalima nyanya, mnavu pamoja na kabichi ambapo kilimo hiki kimenifanya mda mwingi kuwa shambani mpaka naambiwa naringa baada ya kuacha kuhudhuria vijiweni nilikokuwa nikienda kupoteza mda wa mafanikio haya niliyonayo sasa” aliongeza Ole

Hata hivyo wakulima wote wanalalamikia sana changamoto ya mbegu feki madukani pamoja na miundo mbinu ya barabara zisizopitika kabisa kwa gari hivyo wengi kushindwa kufikisha mazao yao katika masoko kwa muda na hata wakati mwingine imekuwa kikwazo cha kuwafanya wateja wao kushindwa kuwafikia kiurahisi pale wanapohitaji bidhaa kutoka kwao, hivyo wanalazimika kila wakati kuwapelekea sokoni 

 “Kama unavyoona hali ya barabara ni mbaya sana, hasa wakati wa masika barabara hazipitiki kabisa na hii ni changamoto kubwa sana kwa sisi wakulima, gharama zinaongezeka na matokeo yake faida pia inapungua”alisema mmoja wakulima wa nyanya.
”Serikali imesahau maeneo ya wakulima ambayo yanazalisha mazao ya biashara na chakula, tumelalamikia hali hii kwa muda mrefu na hata viongozi wetu yaani madiiwani na wabunge wanajua ila hakuna hatua zilizochukuliwa”. Aliongeza mkulima huyo

 Nae Abel kuley wa Rijk zwaan anabainisha kuwa mipango ya taasisi hiyo ni kuwafikia wakulima wengi zaidi katika maeneo yote ambayo kilimo cha mboga na matunda kinaweza kufanyika.
 “Sasa tunaelekeza nguvu zetu katika maeneo yote ambayo kilimo kinaweza kufanyika, malengo yetu ni kuwahusisha zaidi vijana na wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa tatizo la ajira nchini na tunadhani kwamba sekta hii inaweza kuwa mkombozi wa tatizo la ajira na kupunguza umaskini,”alisema. 

Nae Fekadu Fufa Dinssa kutoka, mzalishaji wa mbegu (vegetable breeder) AVRDC alisema kwa kushirikiana na serikali wanaweza kupunguza kabisa tatizo la ajira kama si kulimaliza kabisa ikiwa bei za pembejeo zitapunguzwa ili kuwapa fursa wakulima wengi kupata nafasi ya kujihusisha na kilimo bora

 Kwa mujibu wa taarifa ya Gavana wa Benki ya Tanzania, ya mwaka 2014 sekta ya kilimo imeonekana kupigwa kikumbo na sekta za utalii, dhahabu, viwanda na usafirishaji wa mizigo nje ya nchi. Kwa mujibu wa takwimu hizo sekta ya utalii iliingizia Taifa dola za Marekani bilioni mbili, dhahabu dola bilioni 1.7, viwanda dola bilioni 1.3  na kilimo kinachoingiza dola milioni 830 kwa mwaka. Hata hivyo bado kilimo kimebakia kuwa uti wa mgongo wa uchumi Tanzania.