
viongozi
wa vyama na Serikali nchini Tanzania ambao majina yao yanatajwa na
wananchi kuwa wanaweza kuwania nafasi ya urais kwenye uchaguzi mkuu
mwakani.
Dar es Salaam. Kumekucha. Pengine hilo ndilo
neno linalofaa kutumika kuelezea matokeo ya utafiti kuhusu
kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 ambayo yanaonyesha
kuwa iwapo ungefanyika leo, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
angeibuka mshindi.
Wakati
Lowassa angeibuka na ushindi kwa asilimia 13 na Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda angefuatia kwa karibu akiwa na asilimia 12 huku Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa akiwa wa tatu kwa asilimia kumi na moja.
Hata hivyo, asilimia 33 ya wananchi waliohojiwa walisema bado hawajaamua wampigie kura mgombea gani.
Utafiti
huo wa Taasisi ya Twaweza unayoonyesha wagombea hao kukabana kwa
tofauti ya asilimia mojamoja na ambao ulitangazwa Dar es Salaam jana,
ulifanywa Septemba 2014 kwa kuwahoji wananchi 1,445 kutoka Tanzania
Bara.
Akitangaza matokeo hayo, mtafiti wa Twaweza, Elvis
Mushi alisema utafiti huo ni wa tatu kufanyika nchini na kwamba awamu ya
kwanza ilifanyika mwaka 2012 na Lowassa alipata asilimia sita kabla ya
mwaka jana na mwaka huu kuibuka na asilimia 13.
Akimzungumzia
Pinda, mtafiti huyo alisema mwaka 2012 alipata 16, lakini zilishuka
mwaka 2013 hadi kufikia asilimia kumi na moja na kupanda tena mwaka huu
hadi 12.
“Kwa upande wa Dk Slaa, mwaka 2012 na 2013 alipata asilimia 19 lakini sasa ameshuka hadi asilimia kumi na moja,” alisema Mushi.
Wagombea
wengine waliotajwa na asilimia zao kwenye mabano ni Profesa Ibrahim
Lipumba (6%), Dk John Magufuli (3%), Freeman Mbowe (3%), Samuel Sitta
(4%), Bernard Membe (5%) na Zitto Kabwe (1%).
“Hata hivyo,
kitu muhimu cha kuangalia katika ripoti hii siyo tu majina ya mgombea,
bali ni idadi ya wananchi asilimia 33 ambao wamesema hawajui watamchagua
nani,” aliongeza Mushi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa iwapo
vyama vyote vya upinzani vitaungana na kumchagua mgombea urais mmoja,
asilimia 41 ya wananchi waliohojiwa walisema wangemchagua Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willibrod Slaa, akifuatiwa na Profesa Lipumba (14%), Mbowe
(11%) na Zitto Kabwe (6%).
Wanasiasa wengine waliotajwa ni
Tundu Lissu, Maalim Seif Sharif Hamad, James Mbatia na Augustino Mrema
ambao kila mmoja aliambulia asilimia moja.
Wengi kuchagua CCM
Pia
utafiti unaeleza kuwa iwapo Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
utasimamisha mgombea mmoja wa urais dhidi ya CCM, asilimia 47 ya
wananchi walisema wangeichagua CCM huku asilimia 28 wangempigia kura
mgombea wa muungano wa upinzani. Asilimia 19 ya wananchi walisema
watampigia kura mgombea bila kujali chama chake.
“Kura za
kundi hili zitategemea ubora wa wagombea. Kama kura hizo zitagawanywa
kwa CCM na upinzani, CCM itashinda urais kwa kuzidi upinzani kwa kura
nyingi kiasi. Kutakuwa na kitisho kwa ushindi wa CCM endapo wapigakura
wote watamchagua mtu badala ya chama watampigia mgombea wa upinzani,
kitu ambacho kina uwezekano mdogo kutokea,” inasema ripoti hiyo.
Wananchi walia uchumi, afya na elimu
Wananchi
walipoulizwa ni matatizo gani matatu makubwa yanayoikabili Tanzania
walitaja ukosefu wa elimu bora, afya na hali mbaya ya kiuchumi na kwamba
matatizo hayo yameshika nafasi ya juu kwa miaka mitatu mfululizo.
“Umaskini
umeongezeka kutoka asilimia 49 mwaka 2012 hadi 63 mwaka 2014, huku
matatizo ya afya yakiongezeka kutoka asilimia 40 hadi 47 na elimu
imeshuka kutoka asilimia 46 mwaka jana hadi 38 mwaka huu,” alisema
Mushi.
Wabunge na ahadi zao
Katika utafiti huo,
imeelezwa kuwa ahadi nyingi zilizotolewa na wabunge kwenye mikutano ya
kampeni wakati wa uchaguzi hazijatekelezwa na kwamba asilimia 78 ya
wananchi bado wanazikumbuka.
Ahadi nyingi zilizotolewa na
wagombea zilihusu miradi ya ujenzi barabara, maji, ujenzi wa hospitali,
kuboresha elimu, umeme, mikopo kwa vikundi, kuongeza ajira, kujenga
madaraja na kuboresha kilimo.
Pia ripoti imeweka wazi kuwa
karibu nusu ya wabunge wote huenda wasirudi tena katika nyadhifa zao.
Asilimia 47 ya wananchi walioulizwa iwapo watampigia tena kura mbunge
wao walisema hapana huku asilimia kama hiyo wakisema ndiyo.
Akizungumzia
utafiti huo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu
alihoji namna majina ya wagombea yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo
yalivyopatikana huku akipendekeza namna sahihi ya kuwalinganisha
wagombea hao.
“Walitakiwa kulinganishwa kwa mfano kwenye
kilimo, watuambe Mizengo Pinda anaweza kufanya nini akilinganishwa na
mgombea mwingine. Vinginevyo inakuwa ni mashindano ya urembo. Tunatumia
muda mrefu kumchagua mbuzi Vingunguti kumbe atachinjwa kesho,” alisema
Ulimwengu.
Kwa upande wake, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, alisema hatashangaa kusikia kuna watu wengine wametoa
ripoti nyingine kupinga utafiti huo kwa kuwa kumekuwapo na utamaduni wa
kutokukubaliana na matokeo ya namna hiyo.
“Tafiti hupingwa na
tafiti, kwa hiyo mtu asianze kupinga tu, fanya kama wao (Twaweza)
jifunze kutumia takwimu,” alisema huku akionyesha kukasirishwa na watu
waliokuwa wakitoa maoni ya kupinga ripoti hiyo.
Kauli ya Nape
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema anakubaliana na
matokeo hayo kwa kuwa yamepatikana na njia ya simu katika nchi ambayo
ina watumiaji wengi wa aina hiyo ya mawasiliano.
Hata hivyo,
alisema: “Tatizo ahadi nyingi zinazotolewa na viongozi kwa wananchi
hazitekelezwi. Tunasema asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima lakini
asilimia mbili ya viongozi ndiyo walioahidi kuhusu kilimo.”
Mjumbe
wa lililokuwa Bunge la Katiba, Maria Sarungi alisema ripoti hiyo haina
habari njema kwa vyama vya siasa kwa sababu inaonyesha kuwa wananchi
wamekosa imani ya kupata msaada, badala yake wameanza kumtafuta
‘mkombozi’ atakayewasaidia.
“Inapotokea asimilia 41 wanasema
hawajui watamchagua nani huku asilimia 10 wakisema inategemea na mtu
atakayejitokeza inaonyesha wananchi wanamtafuta mtu atakayewasaidia na
siyo chama.
“Mambo ya wananchi yanatatuliwa na Katiba,
tatizo la utawala bora na umaskini haliletwi na vyama vya siasa
linaletwa na Katiba.”MWANANCHI