“Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.
“Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri.
Mchakato ni mgumu, lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria
kweli kweli tutafika tuendako vizuri,” alisema Rais Kikwete.
Alisema anasikitishwa na tofauti za viongozi wa siasa na kuleta
mfarakano kwa taifa, hali ya kuwa tangu awali aliwaambia kuwa
wakijiruhusu kushindana na kuviziana ni wazi mchakato wa Katiba
utakwama.
“Niliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa siyo Katiba ya CCM, ama ya
Chadema, ama ya NCCR, ama ya CUF. Niliwaambia kuwa hii ni Katiba ya
wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa
tukayaacha kwa sasa na kukubaliana kwa yale ambayo hatuna
tofauti,”alisema.
Awali akisoma risala ya wanafunzi kwa Rais Kikwete, Rais wa Serikali ya
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Boniface Juma, alisema wanaunga
mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuridhishwa na hatua
iliyofikiwa.
“Mheshimiwa Rais, tunaridhishwa sana na hatua iliyofikiwa na Bunge
Maalumu la Katiba, tunaamini kuwa mwafaka unawezekana kwa vipengele
vingine vya Rasimu ya Katiba. Na imani yetu theluthi mbili za kupitisha
Katiba Mpya inawezekana kupatikana,” alisema Juma.
TCD kuteta na JK
Wakati huo huo, taarifa kutoka Dodoma zinaeleza kuwa Ukawa watakutana
wiki hii na Rais Kikwete kuzungumzia suluhu kuhusu mchakato wa Katiba
mpya.
Julai mwaka huu, Ukawa walikacha mazungumzo na Msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba,
Samuel Sitta na hatimaye kugomea mchakato huo kwa kutohudhuria vikao vya
Bunge hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, alisema azimio la kutaka kuonana
na Rais Kikwete ni baada ya mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es
Salaam Agosti 23, mwaka huu na kuhudhuriwa na wenyeviti wa vyama vyote.
Cheyo alikataa kusema ajenda zitakazozungumzwa katika kikao hicho na
Rais, lakini alisema jambo kubwa ni kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Alisema kikao cha maazimio ya kukutana na Rais kiliwakilishwa na
viongozi mbalimbali ambapo CCM, iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake,
Kinana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba na Makamu wake, Magdalena Sakaya na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi,
James Mbatia.
“Viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda TCD waliketi katika mkutano wa
wakuu wa vyama ambapo kwa pamoja walijadili na kutafakari maendeleo ya
mchakato wa Katiba mpya.
“Viongozi hao katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, waliazimia
kutafuta nafasi ya kuonana na Rais kwa lengo la kushauriana naye ambapo
Rais amelipokea ombi hilo na ameahidi kuonana na viongozi hao mwisho wa
wiki hii,” alisema Cheyo.
Hata hivyo, Cheyo, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (UDP),
alipoulizwa ni kitu gani wanakwenda kuzungumza na Rais wakati mchakato
wa Katiba umefika mbali, na nini kimeonekana kimekwenda sivyo hadi
kufikia hatua ya kuomba kukutana naye kwa mashauriano, alikataa
kuzungumzia hilo.
Alisema ajenda za kikao hicho ni siri, na kwamba viongozi wa vyama,
walikubaliana kutosema hadi pale mazungumzo hayo yatakapokwisha.
“Nimesema ni kuhusu mchakato wa Katiba, hayo mambo mengine mtajazia wenyewe, si mnayajua,” alisema Cheyo.
Katibu Ukawa anena
Akizungumzia uamuzi wa kukutana na Rais Kikwete, Katibu wa Ukawa ndani
ya Bunge, Julius Mtatiro, alisema suala la maridhiano kwa nia ya
kupatikana Katiba mpya ni jambo jema ambalo halina matatizo kwao.
“Sisi hatuna matatizo na kukutana na Rais na tunajua kuwa kuna utaratibu
ambao unatakiwa kufuatwa, hivyo endapo utashughulikiwa, tuko tayari
kuonana na Rais ili tunusuru hali ya mvutano inayoendelea,” alisema
Mtatiro.
Alisema kitendo cha Ukawa kususia mchakato huo ni kwa manufaa ya umma,
kwani Katiba itakayoandikwa itakuwa ya Watanzania wote, hivyo ni vyema
kuwa na Katiba ambayo itakubalika na wananchi.