Wednesday, October 8, 2014

KIHUNZI KINGINE CHA KATIBA INAYOPENDEKEZWA

Wakazi wa mjini Dodoma wakiwa kwenye ibada maalumu ya kushukuru kumalizika salama na amani kwa mchakato wa kupatikana kwa Katiba inayopendekezwa, ibada iliyofanyika kwenye Viwanja vya Nyerere Square,jana.  Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/Zanzibar. Katiba inayopendekezwa itakutana na kihunzi kingine katika utekelezwaji wake kutokana na Zanzibar kutakiwa kubadili Katiba yake, zikiwamo ibara zilizobeba msingi wa mabadiliko ya 10 katika Katiba ya Zanzibar.
Mabadiliko hayo ya mwaka 2010, kwa kiasi kikubwa yanakinzana na Katiba ya sasa ya Muungano pamoja na Katiba inayopendekezwa ambayo inakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini Dodoma.
Ili Katiba inayopendekezwa iweze kutekelezeka ni lazima Zanzibar ifanyie mabadiliko Katiba yake kwa kuwa Katiba ya Muungano ndiyo Sheria Kuu.
Hata hivyo, wachambuzi wanahoji iwapo mabadiliko hayo yatawezekana kirahisi kwa kuwa yanatakiwa kuidhinishwa kwa kura ya maoni ya wananchi wa Zanzibar, baada ya kupita kwenye chungu cha Baraza la Wawakilishi na kuamuliwa kwa theluthi mbili za kura.
 Tofauti zilizopo
Mosi, Katiba ya Zanzibar inatamka kwamba Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Ibara ya pili inaitambua Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Masharti hayo ni kinyume na Katiba inayopendekezwa ambayo katika ibara yake ya kwanza inatamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili, 1964 zilikuwa nchi huru.
Pili, Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 26 inatamka kwamba Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa nchi ya Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume na Katiba inayopendekezwa katika Ibara ya 80 (2) ikisema; Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu.
Tatu, Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya pili A inatamka kwamba kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Masharti hayo ni kinyume cha Katiba inayopendekezwa Ibara ya 2(2) ambayo inatamka: “Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine, isipokuwa kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Rais atashauriana na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengine.CHANZO MWANANCHI