Japokuwa
kumekuwa na dhana ya kwamba mkulima ni mtu maskini na asiyeweza kufanya
shughuli nyingine ya maendeleo, lakini kwao UFUMAKIFU wanajiuliza walikuwa wapi
kufanya kilimo hiki tangu siku nyingi.
Akiongea
na mwandishi wa habari Bi Farida Mrisho Pyara, mwenyekiti wa kikundi cha
UFUMAKIFU (Umoja wa wanawake Kiwangwa na Fukayosi) alisema kuwa kilimo cha
mananasi kimekuwa mkombozi kwao kwani tangu walipoanza kujishughulisha na
kilimo hicho kama kikudi maisha ya wanakikundi wengi yamebadirika kutoka katika
hali duni na kuwa bora zaidi.
Kikundi
hicho kilianzishwa mwaka 2012 na shirika la DotAfrika kwa madhumuni ya
kuwakwamua wanawake kimaendeleo katika kazi zao, kina wanawake zaidi ya 50 wa
umri tofauti tofauti. Walianza kwa kuwa na shamba la pamoja ambalo walilima
wanachama wote kwa kupanda mbegu mpya kutoka chuo cha SUA ambazo walipewa na
shirika hilo kama msaada.
Hata hivyo
mwenyekiti huyo alidai kuwa baada ya kulima kama kikundi lakini lilikuwa ni
darasa tosha kwao kwani walijifunza mambo mengi mapya ya jinsi ya kulima kilimo
bora na kutumia mbegu bora za mananasi
kwa kupata mavuno bora kwa manufaa zaidi.
Bi farida
alisema shamba hilo ambalo lilikuwa kama ni shamba darasa kwao liliwapa mafunzo
ambayo kwa sasa kila mwanakikundi ana shamba lake na analima kwa kutumia ujuzi
uleule walioupata hapo awali na kila mmoja amefunguka na kutambua kuwa walikuwa
wanadharau kilimo kwa kuwa walikosa elimu ya kutosha, ni jinsi gani wanaweza
kufanya kilimo chenye manufaa kwao.
“Wanawake
wengi tulikuwa tunafanya biashara ndogo ndogo huku tukiwaachia wanaume kwenda
mashambani peke yao, matokeo yake wengi wetu tulibaki kuwa tegemezi na inakuwa
hali mbaya zaidi ikitokea mwanaume kafariki. Lakini tangu tumeanza kikundi hiki
wengi wetu tuna mashamba yetu binafsi ambayo hutupatia kipato cha kutosha”
alisema Bi Farida.
Hata hivyo
alisema mpaka sasa kila mwanachama anashamba lake ambalo analilima mwenyewe
kama shamba darasa, na iwapo wanapata
tatizo linalohitaji ufumbuzi wanae Afisa kilimo Bwana Amir Abdul ambaye
amekuwa msaada mkubwa sana kwao kwani ndiye anayewapa elimu ya kilimo kila
wanapohitaji elimu hiyo.
Nae Bi
Halima Muhamed Athumani (58) mjumbe wa UFUMAKIFU alisema elimu waliyopewa ni
bora na isiyo ya gharama katika kufanikisha kilimo hicho.
“Tumeletewa
mbegu za mananasi isiyokuwa na magonjwa yaliyokuwa yanatusumbua kipindi cha
nyumaa, na tumejifunza njia ya kulima bila kulichosha shamba wakati huo huo
tunazuia matunda yasiharibiwe na jua kwa kupanda mazao mawili shambani yaani
mananasi na migomba pamoja, wakati huo huo tunarutubisha shamba kwa kuchoma
masalia ya nanasi shambani baada ya kuvuna kitu ambacho tulikuwa hatukijui hapo awali”. Alisema Bi
Halima
“Siku hizi
huwa tunaweka mbolea ya DAP na UREA kwa ajili ya kukuzia na hatutumii dawa ya
aina yoyote kuzuia magonjwa kwani mbegu hii haina usumbufu huo. Na pia mbegu
hii inawahi kukomaa.”
Aliendelea
kwa kusema mbegu hii ni nzuri kwa kuwa hainyauki tunda wala kuozea shambani na
inatoa mazalia bora pia ambayo huwa yanakuwa ni mbeyu kwa ajili ya kupatwa
msimu mwingine nah ii ni tofauti na mbegu tulizokuwa nazo siku za nyuma
Kikundi hicho
ambacho kwa sasa kimeamua kulima kilimo cha kisasa kwa ajili ya kuondoa
umaskini majumbani mwao, wameamua kwenda mbali zaidi kwa kufanya biashara ya
mananasi nje ya nchi na mikoa ya mbali kwa kuyasindika mananasi na
kuyasafirisha.
“Hivi
saasa tumejenga makaushio (dryer) kwa ajili ya kukausha mananasi na kuyahifadhi
vizuri kwenye mifuko tayari kwa kuyapeleka sokoni ili kuwa na tija zaidi.
alisema Mwenyekiti huyo
Bi Farida
akiwa ndani ya makaushio (dryer) akitoa maelezo jinsi kipima joto kinavyofanya
kazi
Kilimo cha nanasi kinastawi zaidi
katika ukanda wa nchi za joto na kwenye udongo usituamisha maji. Hapa Tanzania
zao hili linastawi sehemu nyingi lakini kwa wingi linastawi mikoa ya Pwani,
Morogoro, Shinyanga Tanga Mtwara Lindi na Bukoba. Katika mkoa wa pwani, zao
hili linalimwa katika wilaya ya Bagamoyo, Mkuranga Kibaha na Kisarawe. Kwa
Bagamoyo linalimwa zaidi katika kata ya Kiwangwa na maeneo ya Gongo.
Zao hili lina kiasi kikubwa cha
vitamini A na B na kiasi kidogo cha vitamini C, pia kuna
madini kama potasiam, kalsiam, chuma na magnesiam
Nanasi
huliwa baada ya kumenywa ganda la nje na pia hukamuliwa maji yake
na kunywa kama juisi.Nanasi pia linaweza kuanikwa na kukaushwa ambapo huliwa kwa
kutafunwa. Nanasi pia baada ya kukauka husagwa na unga wake hutumika
kutengeneza juisi au kuchanganywa katika vilaji vingine kama vile Pizza nk