Wakazi
wa Manispaa ya Shinyanga, kwa siku mbili mfululizo walikumbwa na
kiwewe, baada ya kuenea uvumi kwamba kuna mgonjwa wa mwenye homa hatari
ya ebola, aliyefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Taarifa
za kuwepo kwa mgonjwa huyo, zilidai kuwa mgonjwa huyo alitoka katika
moja ya mitaa ya Manispaa ya Shinyanga na alikuwa akitokwa damu puani
na mdomoni kabla ya kuzimia.
Akizungumzia hali hiyo jana, Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Shinyanga, Dk Ntuli Kapologwe alisema mgonjwa huyo ambaye
alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani, alifika hospitalini hapo juzi na
baada ya kufika wauguzi na madaktari walitaharuki.
Kwa mujibu wa Dk Kapologwe, mgonjwa huyo
alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), huku baadhi ya wauguzi na
madaktari wakimkimbia hali iliyotia hofu kwa baadhi ya wahudumu na hata
wagonjwa hospitalini hapo.
Hata hivyo, Dk Kapologwe alisema baada ya uchunguzi wa awali, ilibainika kuwa mgonjwa huyo ana matatizo ya kutokwa damu mara kwa mara na hajaambukizwa virusi hao wa ebola.
Akielezea namna mkoa ulivyojiandaa
kukabiliana na ugonjwa huo uliokwishaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi
za Afrika Magharibi, Dk Kapologwe alisema waganga wakuu katika
halmashauri zote sita za wilaya mkoani Shinyanga, wameshajiandaa.
Alisema wamekubaliana atakapogundulika mtu
mwenye dalili za ugonjwa huo, taarifa itolewe mara moja katika ngazi ya
mkoa, ambako kuna timu maalumu ya wataalamu iliyoandaliwa kushughulika
na ugonjwa huo hatari.
Baada ya taarifa kutolewa kwa mujibu wa Dk
Kapologwe, timu hiyo itathibitisha kama mgojwa ana dalili zote za ebola
na taarifa kutolewa kwa umma.
Wakati ugonjwa huo ukisababisha kiwewe
mkoani Shinyanga, mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe
ameshauri wakazi wa mkoa huo kuwa macho na tayari kutoa taarifa kwenye
vituo vya afya vilivyo jirani waonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa
huo.
Alitoa mwito huo kupitia kwa waandishi wa
habari aliozungumza nao jana ofisini kwake mjini hapa, baada ya kuibuka
taarifa kuwa Rwanda kulikuwa na mtu anayehisiwa kuwa na ebola.
Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes
Binagwaho alisema juzi kuwa mwanafunzi mmoja wa Ujerumani aliyefika
nchini humo akitokea Liberia, alihisiwa kuwa na ugonjwa huo lakini
baada ya sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za kimataifa,
hakukutwa na ugonjwa huo.
Massawe alisema Mkoa wa Kagera unapakana na
nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na pia upo mwingiliano wa watu na
shughuli mbalimbali za kijamii.
Alisema nchi jirani zikipata mlipuko wa
ugonjwa huo, upo uwezekano wa kuvuka mipaka na kuingia mkoani Kagera,
hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutoa taarifa akiona mtu anayedhaniwa
kuwa na ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo unaoenezwa na virusi
vya ebola ni pamoja na kutokwa na damu sehemu mbali mbali za mwili,
kuumwa na kichwa, mwili kuishiwa nguvu, maumivu ya misuli na hatimaye
kifo.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa damu na majimaji ya mgonjwa pamoja na kugusa vifaa au nguo za mgonjwa.
Massawe alisema Kagera wamechukua hatua kwa kuweka mikakati kuhakikisha mlipuko wa ugonjwa hauingii nchini kupitia mipakani.
Miongoni mwa halmashauri ambazo
zimeelekezwa kuchukua hadhari kutokana na kuwa mpakani mwa nchi, ni
wilaya ya Bukoba, Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara.