Nashambuliwa, tunashambuliwa! PAC tunasema “Hatutetereki”
Zikiwa
zimebaki siku chache kabla ya Kamati ninayoongoza ya PAC kuwasilisha
Bungeni Taarifa Maalumu kuhusu ukaguzi maalumu wa akaunti ya Tegeta
Escrow, kumekuwa na kampeni za chini chini zinazoendeshwa kwenye korido
za Bunge na kwenye mitandao dhidi yangu binafsi na baadhi ya wabunge
waliosimama kidete dhidi ya wizi wa fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania
akaunti ya Escrow.
Baadhi ya tuhuma nimezipeleka kwenye vyombo
vya dola ili zichunguzwe kwani zina vielelezo vya mahala pa kuanzia
(kama leseni ya udereva ya mwanamke anajulikana kama Vivian Emmanuel
Sirikwa na muhuri wa kampuni ya uwakili inayomilikiwa na Bwana Joseph
Mkandege).
Baadhi ya Tuhuma
Baadhi ya tuhuma nitazijibu moja baada ya moja.
Waziri
mmoja ambaye ni mtuhumiwa wa wizi wa fedha za Tegeta Escrow anazunguka
kwa wabunge akisema tuhuma hizi kupikwa kama njia yake ya kuhamisha
mjadala kutoka uporaji wa Tshs 200 bilioni kwenda kwenye masuala
binafsi.
Tuhuma hizi zenye kichwa cha habari “Zitto na
Filikunjombe wanatumiwa na Kenya na Uingereza kuvuruga na kudhoofisha
Uwekezaji nchini mwetu” zinajibiwa hapa chini. Utaona ndugu Filikunjombe
ametajwa kwa kichwa cha habari ili kumtaja tu bila sababu yeyote ile.
Tuhuma #1:
Zitto
anaye rafiki yake Mkenya aitwae Rapahel Ongangi ambao kwa pamoja
wameanzisha Gombe Advisors Co. Ltd (registered on 24 November 2011,
Certificate No 87387) kwa ajili ya kufanya biashara na Makampuni ya Gesi
na Mafuta yanayofanya kazi nchini hapa.
Majibu:
Gombe
Advisors ni kampuni binafsi isiyofanya faida yaani ‘Company Limited by
Guarantee’. Haina kazi na kampuni yoyote ya Gesi na Mafuta na wala
yenyewe haijuhusishi na biashara hiyo. Gombe advisors haijafanya kazi
yoyote ile na kampuni nyingine zaidi ya kusaidia wasanii wa kundi la
Kigoma All stars. Upotoshaji hapa unalenga kupindisha mjadala.
Tuhuma #2:
Zitto
amemsaidia Ongangi kupata uraia wa Tanzania na kwa sasa ni raia wa
pasipoti. Zitto na Ongangi walimtafutia CEO wa Shell aitwae Axel Knospe
nyumba na gari ya kukodi.
Majibu:
Raphael ni mtu binafsi
ambaye anafanya shughuli zake hapa nchini, amesoma hapa nchini na ameoa
na ana mtoto. Tuhuma hizi hazina msingi wowote ule maana ni uwongo.
Wanaotoa tuhuma hizi waonyeshe hiyo pasipoti ya Bwana Ongangi
kuthibitisha madai yao.
Tuhuma #3:
Mikataba ya STATOIL
iliyokuwa inarushwa kwenye mitandao ya jamii na kuchapishwa kwenye
magazeti ya Kenya ya hapa nchini (The Citizen na Mwananchi) mwandishi
mkuu alikuwa huyo CEO wa Shell.
Majibu:
Mkataba
uliovujishwa wa StatOil ulivujishwa na waandishi wa habari wa Norway.
Uchambuzi wa mkataba huo nimeufanya mwenyewe kwa kutumia utaalamu wangu
niliosomea wa kuchambua mifumo ya kodi kwenye sekta ya mafuta na gesi.
Kwa namna yoyote ile, huyo anayetajwa kuwa CEO wa kampuni ya Shell
hahusiki. Tuhuma hii wanaoitoa watoe ushahidi usio na chembe ya mashaka.
Ikumbukwe
kuwa mkataba wa StatOil utaipotezea Tanzania mapato ya dola za Marekani
bilioni 12 (takribani Tshs 20,400,000,000,000/=) katika kipindi cha
miaka 15 baada ya gesi kuanza kuchimbwa.
Uamuzi wa Kamati ya PAC
kutaka mikataba yote ya Gesi kuwa wazi una lengo la kuchambua kuona kama
mikataba yote nchini haipotezi mapato kwa nchi. Uamuzi huo
umewakasirisha sana baadhi ya waliohusika kuingia mikataba Serikalini
maana wanajua kuna madudu kwenye mikataba na wanataka umma wa watanzania
usijue!
Tuhuma #4:
Kampuni ya SHELL imechukizwa sana
kucheleweshwa kwa kupata kibali cha kutafuta gesi na mafuta kule Pemba.
Vilevile SHELL haina uwekezaji mkubwa Tanzania Bara kwani ilishindwa
kwenye tenda zenye vitalu vyenye gesi nyingi upande wa Bara.
Majibu:
Ukweli
ni kuwa Kampuni ya Shell ina vitalu 4 huko Zanzibar na tayari ina
makubaliano na Serikali ya Zanzibar kuhusu utafutaji mafuta huko katika
vitalu namba 9,10,11 na 12. Shell inafanya kazi na kampuni ya Petrobras
ya Brazil kwenye kitalu namba 6 na namba 8. Taarifa hizi zipo wazi
kwenye tovuti ya TPDC. Tuhuma nyepesi namna hii dhidi ya kampuni kubwa
kama Shell zinaonyesha dharau na kiburi kinachotokana na uelewa mdogo wa
mambo wa watu wanaotuhumu.
Tuhuma 5:
Ongangi anapokea maelekezo kutoka Serikali ya Kenya kuhujumu uwekezaji nchini mwetu.
Majibu:
Nazifahamu
mbinu nyingi zinazotumika kufanya propaganda, lakini mbinu hii
imeshindwa ikiwa mapema sana. Ni vema wanaotoa tuhuma hizi
wazithibitishe vinginevyo ni mwendelezo wa propaganda zisozingatia
diplomasia ndani yake dhidi ya jirani zetu wa Kenya. Hizi ni propaganda
hatari ambazo hata hao wanaotuhumiwa wakisikia watatudharau sana.
Tuhuma #6 (juu ya Uingereza):
Uingereza
imekuwa inamfadhili Zitto kwa miaka mingi kwa mambo yake ya kisiasa kwa
hiyo sasa hivi Ubalozi wa Uingereza unamlipa Zitto na Kafulila
kuhakikisha kwamba Standard Chartered ya Uingereza inalipwa deni lake
lisilotambulika kisheria nchini mwetu.
Majibu:
Nimetangulia
kusema hapo awali kuwa kuna propaganda ambazo haziangalii hata
diplomasia; nyingine ni hii. Pamoja na kukanusha uzushi huu, ni vizuri
wanaotoa tuhuma za namna hii kuthibitisha. Mimi binafsi sijawahi
kufadhiliwa kisiasa na Taifa lolote lile. Inaelekea kuna wanasiasa
wanaofadhiliwa na mataifa mengine ambao kwakuwa kwao ndiyo maisha
wanaamini na wengine tupo kama walivyo.
Kwangu itikadi yangu ni
‘Uzalendo kwa nchi yangu’, ni jambo ambalo halina mbadala wake. Siku
zote nasema “Right or wrong, my country first”.
Kurudia kurusha
tuhuma kwa Ubalozi wa Uingereza nchini ni kudhihirisha kwa mara nyingine
kiburi cha kuwa na mamlaka (arrogance of power) walicho nacho wanaotuma
tuhuma hizi.
Aidha, wanatuhumu kuwa “Kafulila na Zitto wamehaidiwa 15% ya USD 150 million kama deni likilipwa”
Mtanzania
anayeweza propaganda dhaifu kama hizi basi anatakiwa ajitafakari. Hata
hivyo ni vema wanaotoa tuhuma hizi wathibitishe bila chembe ya mashaka.
Tuhuma #7:
Mbunge
Mkono nae ameshikwa hasira kupoteza kazi ya uwakili pale TANESCO.
Kafulila na Zitto wanalipwa na Mkono kuvuruga Serikali kwa hasira za
kukosa fedha za kitapeli za TANESCO.
Majibu:
Hizi ni
tuhuma ambazo sasa tumezizoea kutolewa. Mambo mepesi hayawezi kujibu
mambo ya msingi kama tuhuma za wizi wa fedha zaidi ya Tshs bilioni 200
kutoka Benki kuu ya Tanzania. Kukusanya kila propaganda ili kuuhamisha
umma ni kupungukiwa hekima na busara.
Aidha, wanaotuhumu
wanadokeza kuwa “Naomba tuwe macho na Wabunge wetu achananeni na madai
ya Zitto ya wizi. Huyu mtu anafanya biashara na Kampuni ya SHELL na
inasemekana analipwa na Ubalozi wa Uingereza. Serikali ya Kenya na
tapeli mkubwa Mbunge Mkono nae anawalipa Zitto na Kafulila”.
Watanzania,
haya ni maneno ya hasira ya watu wanaokaribia kukamatwa kwa kushiriki
wizi wa fedha katika Benki kuu ya Tanzania. Kamwe tuhuma kama hizi
haziwezi kutukatisha tamaa katika kupambana ili ukweli ujulikane. Sisi
tutapigana kwa ajili ya Taifa, kwa ajili ya mtanzania na tunachotaka ni
umma uujue ukweli wa mambo.
Hasira hizi zinatokana na mambo mawili:
Moja
ni uamuzi wa kamati ya PAC kuwasweka ndani baadhi ya watendaji wa TPDC
kwa kushindwa kutekeleza maamuzi ya Kamati yanayohusu uwazi wa mikataba
ya Gesi na Mafuta.
Pili, ni uamuzi wa PAC kuagiza ukaguzi maalumu
wa mchakato mzima wa kuanzishwa na kufungwa kwa akaunti ya Tegeta
Escrow ambapo zaidi ya shilingi bilioni 200 ziliporwa na zaidi ya
shilingi bilioni 12 zinalipwa na TANESCO kila mwezi kwenda kampuni ya
PAP inayomilikiwa na Harbinder Singh Seth (50%) na watu wasiojulikana
kupitia kampuni ya Simba Trust iliyosajiliwa na kufichwa nchini
Australia (50%).
Ieleweke kuwa PAP inalipwa shilingi milioni 400
kila siku kutoka TANESCO izalishe au isizalishe Umeme! Watanzania, PAP
itaendelea kulipwa namna hiyo kwa miaka 20 ijayo. Kwa namna ambayo Seth
analindwa na baadhi ya watendaji Serikalini na hasa ndani ya Wizara ya
Nishati na Madini. Aidha, kuna fununu kuwa kuna maofisa serikalini
wanaomiliki hizo 50% za kampuni ya PAP. Seth pia anamiliki kitalu cha
gesi Mnazi bay Kaskazini kupitia kampuni ya HydroTanz.
Hasira
hizi walizo nazo wanaonituhumu na Kamati yangu zimewapelekea kugushi
nyaraka mbalimbali zinazonituhumu mimi na wenzangu ili kutuogopesha na
kutukatisha tamaa katika kutafuta ukweli juu ya suala la uporaji wa
fedha kutoka Benki kuu. Lengo lao ni kututoa kwenye mstari. Mimi na
wenzangu hatutatoka kwenye mstari, tutashirikiana na wabunge wenzetu
kuhakikisha ukweli unajulikana na wezi kuchukuliwa hatua kali.
Harbinder
Singh Seth aliiangusha Serikali ya KANU nchini Kenya, sasa anachotaka
kukifanya kinaweza kuiangusha Serikali ya CCM wakiendelea kumkumbatia.
Watanzania sio mabwege!
Zitto Kabwe
Mwenyekiti PAC
Dodoma, 9 Novemba 2014