IMEELEZWA kuwa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imeshindwa kupaa
kiuchumi kutokana na kushindwa kutumia fursa ya kuvitangaza vivutio vilivyopo
ambavyo havipatikani duniani kote vitakavyopelekea wilaya hiyo ipae kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na katibu mkuu wa Christian and
Gospel Ministry (CGM)wilayani humo Watson Pamesa wakati wa makabidhiano ya jengo
la kufungia mitambo kwa ajili ya matumizi ya Redio Rungwe inayotarajiwa
kufunguliwa siku za hivi karibuni.
Makabidhiano hayo ya jengo la ngazi moja yalifanyika jana
baada ya uongozi wa Christian kuketi na wakuu wa idara kwenye ofisi ya
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Veronika Kessy ambapo mapendekezo na
muhtasari wa kikao hicho yatapelekwa kwenye kikao cha baraza la madiwani Agosti
26 mwaka huu kujadiliwa.
Pamesa alisema waliiandikia halmashauri hiyo barua ya kutaka
kukodi jengo kwa matumizi hayo yenye kumb,RDC/E.1/117/97 ya tare,07/8/2013
ambapo ilijibiwa na kusainiwa na kaim mkurugenzi wa halmashauri hiyo Elias
Sangi kwa barua yenye kumb,TKY/7.6/VOL.010/2014 ya Tar,30/05/2014 kuwa ombi lao
limekubaliwa.
Alisema baada ya makubariano hayo siku ya alhamisi ya
tare,11/9/2014 walienda kuoneshwa jengo pamoja na mapendekezo ya ulipaji na
kuwa kinachosubiriwa ni maamuzi ya madiwani ambapo wataketi siku hiyo na kutoa
maamuzi.
Alivitaja vivutio hivyo ambavyo havipatikani Duniani kote
kuwa ni Vinyonga na Nyani wekundu
waliopo mlima Rungwe,daraja la mungu,ziwa ngozi na kisiba wenye ambayo maji yake
hayajai wala hayakauki,mti Rungwe ambao jina la wilaya limetokana na mti huo na
unatibu magonjwa zaidi ya 45.
Alisema ujio wa redio hiyo utavitangaza vivutio hivyo na
kupelekea watalii kuzuru wilaya hiyo na kujionea maajabu ambayo hayapatikani
Duniani kote na kuwa wilaya hiyo itakuwa haishikiki kiuchumi kuliko ilivyo sasa
ambapo ni ya pili kutoka mwisho kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Christian and Gospel Ministry
wilayani humo Amoni Mwakilomo mbali na kuipongeza halmashauri ya wilaya hiyo
kwa kuwaunga mkono pia amesema mchakato wa redio umefikia ukingoni na sasa
wanajipanga kuanzisha gazeti kwa lengo la kutoa huduma ya kihabari kwa
wanarungwe.
Chrispin Meela mkuu wa wilaya hiyo alisema watakuwa bega kwa bega
na mtandao huo ili kuhakikisha wilaya hiyo inatumia Digital na kuondokana na
analojia kwa kuuhabarisha umma kwa matukio mbalimbali na kukuza pato la ndani nje
wilayani humo.