JESHI la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia askari wake WP Fatuma wa
Kituo cha Polisi Igogo wilayani Nyamagana kwa kosa la kumjeruhi mtumishi
wake wa ndani kwa mkumkata vidole vyake vinne vya mkono wa kulia kwa
panga, akimtuhumu kumwibia Deki ya Video nyumbani kwake.
Tukio hilo la kujeruhiwa kijana Steven Magessa (18), lilitokea Oktoba 20
mwaka huu katika kijiji cha Magange Mugumu wilayani Serengeti mkoani
Mara nyumbani kwao kijana huyo aliyekuwa amekimbilia huko baada ya
kudaiwa kumwibia mwajili wake nyumbani eneo la Igogo.
AKIONYESHA NAMNA ALIVYOJERUHIWA NA MAMA HUYO
Akizungumza na waandishi wa habari kijana huyo alieleza kuwa kufanya
kazi kwa askari huyo kulikuja mara baada ya askari huyo kumfuata
kijijini na kumuomba ridhaa ya wazazi wa kijana huyo kuambatana naye
jijini Mwanza ili kumsaidia kazi za nyumbani ambapo walikubaliana malipo
ya kiasi cha Sh 50,000/= kila mwezi jambo ambalo askari huyo alilikiuka
na kushindwa kulitekeleza kwa muda wa miezi sita bila kumlipa mshahara.
“Nilipoona hajanilipa mshahara wangu kwa muda wa miezi sita huku kila ni
kimwambia ananijia juu na kunitukana matusi basi nilimuomba ruhusa ya
kwenda kijijini Oktoba 15 mwaka huu kumuona mama yangu mzazi aliyekuwa
anaumwa ili kupata nafasi ya kurudi nyumbani” alisema.
Steven alieleza kuwa wakati akiwa kijijini askari huyo (Mwajili wake)
alikuwa akimpigia simu kumtaka arudi Mwanza kuendelea na kazi na kudai
kuwa atamlipa malimbikizo ya mshahara wake kiasi cha Sh 300,000/=
zilizokuwa kama deni, Steven alikubali ombi hilo kwa kuomba atumiwe
nauli na pesa kidogo ya kumwachia mama yake, jambo ambalo askari huyo
alikaa kimya bila majibu.
“Siku ya Oktoba 20 mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi alifika kijijini
akiwa na askari watatu kwenye gari la Polisi (Difenda) wa Kituo cha
Mugumu na kudai kuwa nipo chini ya ulinzi kisha kunifunga pingu, akidai
kuwa nilimwibia Deki ya Video na kutoroka nyumbani kwake, walinipandisha
kwenye Difenda kunipeleka kituoni “ alisema.
Kijana huyo alieleza kuwa baada ya kufikishwa kituoni Mugumu askari huyo
na wenzake walianza kumuhoji huku wakimpa maneno ya vitisho, kijana
huyo alipokataa kuwa hakuiba wala kutoroka, Sajenti Fatuma aliamuru
kijana huyo kuvulishwa shati alilovaa na kisha akafungwa usoni na
kuombwa anyooshe mkono mezani ili apewe 'Sapraizi'.
"Sekunde chache nilihisi kitu kikali kimenipitia kwenye vidole vyangu
vinne vya mkono wa kulia na kufuatiwa na maumivu makali, niliusogeza
mkono wangu mdomoni kuupoza kwa kuupuliza ndipo nilipo gundua kuwa
nimekatwa kabisa vidole vyangu vinne vya mkono wangu wa kulia ikibakia
dole gumba tu" kijana Steven alisimulia kwa uchungu.
“Niliangua kilio kutokana na maumizu na sijui vidole vyangu hadi sasa
sijui vikowapi, askari wenzake baada ya kuona nimetokwa na damu nyingi
walimshauri anipeleke hospitali ya Wilaya ya Mugumu ili nipatiwe
matibabu kabla ya kuondoka kuja Mwanza,”alisisitiza.
Steven alisema baada ya kupatiwa matibabu, tulienda kupanda basi ili
kuja Mwanza kwa madai kuwa amenifungulia kesi ya wizi wa Deki ya Video
na tuliopfika alinipeleka kituo cha Polisi Kati Nyamagana na kuniweka
Mahabusu akinituhumu wizi, lakini nilipochukuliwa maelezo nilikana
tuhuma za wizi na kueleza ukweli wangu ili kupata msaada.
Huku taarifa zingine kutoka ndani ya jeshi zilizopatikana zilidai kuwa
askari huyo alikusudia kufanya ukatili huo kutokana na udanganyifu ambao
alifanya kwa uongozi wake akiomba kupatiwa silaha (SMG) kwa ajili ya
kuitumia kwenye kazi za nje lakini lengo ikiwa ni kwenda na silaha hiyo
kwa ajili ya kumkamata na kumtishia kijana huyo, jambo ambalo uongozi
ulimgomea.
JESHI LA POLISI LINASEMAJE
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Valentino Mlowola, jana
ofisini kwake amethibitisha kuwepo kwa taarifa za tukio hilo na kueleza
kuwa tayari Jeshi hilo limechukuwa hatua madhubuti hatua ya awali ikiwa
ni kumshikilia askari huyo kwa kufanya ukatili huo kwa kuvunja sheria
na kujichukulia sheria mkononi kumjeruhi kijana huyo.
Mlowola alisema pamoja na kijana huyo awali kufunguliwa jarada la
kutuhumiwa kufanya kosa la wizi (Jinai) na kudaiwa kutorokea kijijini
kwao, bado askari huyo alitakiwa kufuata mfumo wa kiutawala na kisheria
uliopo kushughulikia suala hilo badala ya kuamua kujichukulia maamuzi ya
kumwadhibu mtuhumiwa kabla ya uthibitisho wa mashitaka yaliyokuwa
yamefungulia.
“Nilipopokea taarifa hizi kwa mashangao na masikitiko makubwa na
zimenisitua sana, si kitendo cha kiungwana hata kidogo kwa mtu ambaye
anatakiwa kufuata taratibu za mfumo wa utawala na sheria katika
utekelezaji wa kushughulikia kero na matatizo ya jamii, alitakiwa
kutumia busara kwani tayari aliishamfungulia jarada la kumtuhumu
kumwibia ikizingatiwa naye ni mzazi wa watoto watano ni lazima anaujua
uchungu,”alisema.
Kamanda Mlowola alieleza kufatia ukatili huo kufanywa na askari wake
ameunda timu ya kikosi cha askari kwenda hadi kijijini Magange wilayani
Serengeti mkoani Mara ili kufanya uchunguzi wa tukio hili ikiwa ni
pamoja na kufanya mahojiano na familia, wananchi wa kijiji hicho kisha
Hospitali ya Wilaya ya Serengeti alipopatiwa matibabu ya awali.
HIVI NDIVYO VIDOLE VILIVYOKATWA NA MAMA HUYO.
“Ili tupate ukweli wa jambo hili tumeunda timu hiyo, kwani kijana Steven
tumemhoji ametueleza jinsi askari Fatuma alichomfanyia na kudai
hakumwibia, lakini askri wetu pia amehojiwa awali amedai hakufanya
kitendo hicho bali wananchi ndo walimfanyia ukatili huo hivyo ni
mkanganyiko lakini ukweli utapatikana tu japo kuwa tukio hili
halikufanyika Mwanza”alisisitiza.
Mlowola alisema kwamba tayari tunamshikiria askari huyu na kumfungulia
jarada la uchunguzi kwa taratibu za kijeshi na ikibainika kutenda kosa
hilo tutumfukuza kazi na kumfikisha katika vyombo vya sheria ili
kuchukuliwa hatua zaidi kulingana na kosa alilofanya, lakini pia kijana
Steven naye anashikiriwa kwa tuhuma alizonazo za wizi kufatia jarada
lililopo.
“Hatuwezi kuendelea kucheka na kufumbia macho kitendo hiki ni jambo
ambalo linamgusa kila mtu hata mimi ni mzazi ukiachana na utumishi wangu
wa umma, ntahakikisha jambo hili nalishughulikia kwa umakini na kutoa
taarifa kwa umma ili pia kueleza wananchi kuwa tukio hili limefanywa na
mtumishi kama mtu si Taasisi ya Jeshi la Polisi na ahidi kutenda haki
kwenye hili,”alisisitiza.
Wito wangu kwa wananchi ni kuacha kujichukulia sheria mkononi na
kuwaadhibu watuhumiwa mbalimbali kabla ya kuthibitika kwa makosa na
tuhuma hizo, lakini wazingatie kufuata taratibu za kuwafikisha kwenye
vyombo vya sheria ili kushughulikia matatizo yao nawaomba waendelee
kutoa ushirikiana na kufuata mfumo uliopo badala ya kujichukulia sheria
mkononi.