Friday, August 1, 2014

TGT NA MBINU YA MKULIMA MWEZESHAJI KUKOMBOA KILIMO CHA PAMBA NCHINI


 Lydia Mapunda
Katika maisha ya sasa mkulima ni mtu pekee anayetakiwa kuheshimiwa kutokana na kutokuwa na historia ya kugoma na kuendelea kufanya kazi hata katika mazingira magumu yasiyostahili. Japokuwa serikali imekuja na misemo mingi ihusuyo kilimo ambayo kwa wakati mwingine imekuwa ikimtia moyo mkulima katika kazi yake lakini amebakia kuwa mtu mwenye kipato cha chini kisichoendana na msemo wa ‘kilimo ndio uti wa mgongo Tanzania’.
Katika kipindi cha miaka ya 70 hadi 80 mwishoni mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Singida, Mara, Kagera na Tabora ilikuwa maarufu sana kwa kilimo cha pamba ambapo ilikuwa ikizalisha asilimia 95 ya zao hilo.

Lakini kwa upande wa mikoa ya ukanda wa mashariki ya Morogoro, Manyara, Tanga na Kilimanjaro uzalishaji wake ulikuwa ni asilimia tano. Kitu ambacho ni tofauti na hali ya sasa ambapo imefikia wakati wakulima kukata tama ya ulimaji wa zao hili katika mikoa hiyo.
Hata hivyo pamba ilitoa ajira nyingi kwa wantanzania wakiwemo wa vijijini na mijini, na pia ilikuwa chanzo kizuri cha mapoato ya nchi ya fedha za kigeni kutokana na kiasi kikubwa cha pamba kuuzwa nje ya nchi. Pamba iliyokuwa inapatikana kwa miaka ya nyuma ilifanyika matokeo ya kuwepo kwa viwanda kama vile Urafiki, Mwatex, Mbeyatex, Kilitex, Mutex na vingine vingi nchini ambavyo kwa sasa baadhi ya viwanda hivyo vimebakia kuwa historia kutokana na kubadirika na kuwa magofu kwa kutokufanya kazi kutokana na uhaba wa pamba nchini. 

Matumaini ya wakulima wengi waliokuwa wamekata tamaa ya kulima pamba yamerudi tena ambao kwa hivi karibuni wameonyesha matumaini ya kuanza kuweka jitihada  katika kilimo cha zao la Pamba baada ya TGT (Tanzania Gatsby Trust) likishirikiana na TCB kutoa elimu kwa wakulima hao njia na kanuni bora za kilimo nchini.
Tanzania Gatsby Trust (TGT) ni shirika lililo anzishwa na Lord David Sainsbury wa Turville, ambaye ni mwanzilishi wa Gatsby Charitable Foundation. Shirika hili ambalo makao makuu yake kwa hapa Tanzania yapo jijini Mwanza lina nia ya kukiinua kilimo cha pamba katika mikoa inayojishughulisha na kilimo hicho. Hata hivyo shughuli ambazo zinafanywa na TGT ni kuwaelimisha wakulima kutumia mfumo wa kilimo cha kisasa ili kumkomboa mkulima katika hali ya umaskini

Bwana Ruyemerya ambaye ni mshauri wa TGT amesema kuwa Mbinu kubwa wanayoitumia TGT ni kuanzisha kilimo hifadhi (conservation agriculture), ambapo wao kama TGT walitafuta wakulima wachache kutoka sehemu mbali mbali za ukanda wa ziwa na kuwapa mafunzo ya kilimo hifadhi na kuwapa uhalali ya kwenda kuwafundisha wakulima wenzao kitu ambacho kinafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kurudisha matumaini kwa wakulima wa    pamba kwamba wanaweza wakarudi katika hali ya zamani ya kuliingiza zao la pamba kwa mara nyingine tena katika ramani ya dunia kwa kutumia kilimo hifadhi.

 Kwa kupitia elimu ya mkulima mwezeshaji Finias Rafael wa kibondo mkoani kigoma ambaye ni mkulima mwezeshaji wa kilimo cha mahindi pamoja na pamba alisema kuwa tangu ameanza kazi hiyo aliyopewa na TGT  ana uzoefu wa miaka miwili sasa na ameshuhudia kuwa kilimo cha pamba changamoto zake kubwa ilikuwa ni bei ya kuuzia pamba ambapo amedai kuwa kwa sasa bei si hoja kutokana na uzalishaji anaoupata kutokana na kanuni za kilimo bora ambapo alidai kuwa wakulilma wengine walimfuata ili awape mafunzo naye bila hiyana anafanya hivyo kwasababu hiyo ndio kazi kubwa ya mkulima mwezeshajia aliyopewa na TGT.
Nae Enock nyambui mkulima mwezeshaji kutoka Musoma alisema kuwa kutoka kilo 300 au 250 kwa hekta alizokuwa akipata hapo awali lakini kwa sasa huvuna kilo 1000 mpaka 1200 kwa hekta na pia amewasihi wakulima wengina kuachana na kilimo tulicho achiwa na mababu zetu na tubadirike kutokana na sayansi na teknologia ili kuachana na malalamiko ya kila siku kwa serikali.

Wote kwa ujumla wameipongeza TGT kwa Elimu yao kwani hata wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa katika kilimo hifadhi baada ya kuona mafanikio kutoka kwa wakulima wawezeshaji. 

Bwana Enock aliwakosoa wakulima wanaokataa kutumia dawa ya kupuliza shambani kwa madai ya kuwa yanaharibu afya, na kusema kuwa ni upotofu na ni ufinyu wa mawazo na elimu. “me nashangaa sana wanatumia vipodozi vya kubadiri ngozi na nywele bila woga lakini wanaogopa kutumia dawa ya kuuwa wadudu shambani eti inaharibu  afya, na wanaovuta sigara pia nao wanalalamika wanasahau wanatumia kitu ambacho paketi yake too ina onyo juu basi tuache vitu vyote vya viwandani.”
Kwa upande wake mkulima mwezeshaji kutoka mkoa wa Simiu Bwana Lupande Nila amesifia sana matumizi ya jembe la liper ambayo amepata kutoka TGT. Jembe hilo limefanyika mkombozi mkubwa kwa mkulima kwakuwa hutumia mda mfupi kufanya kazi kubwa sana na matumizi wa jembe hili huruuhusu maandalizi ya shamba mapema sana na huepusha usumbufu kwa udongo na huuwezesha udongo kuhifadhi unyevu shambani tafauti na kilimo cha jembe la mkono au plau.  

 
Waandishi wa habari wakiwahoji wakulima  wawezeshaji 


Hata hivyo Bi Everina Lukonge ambaye ni mtafiti wa zao la pamba kutoka UARI (Ukiriguru Agricultural Research Institute) amesema kuwa, Wanatoa mbegu nzuri zinazostahimili hali ya hewa ya ukanda wao ili kuwapa wakulima mbegu ambazo zitawafanya kupata pamba bora na ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa pamba mbegu kwa kumrahisishia mkulima ghalama ya mbegu kwa msimu unaofuata. Pia amewaomba wakulima kutoa ushirikiano kwao kama watafiti ili kuweza kupata mrejesho bora kutoka kwao ili kuweza kurahisisha kazi ya utaafiti kuwa bora zaidi.

Pia Bi Everina amewatoa wasiwasi wakulima kwa kusema kuwa ukiriguru ina kitengo cha Agronomia ambacho kinasimamia utafiti wa mbegu bora, aina bora ya kilimo, utafiti wa udhibiti wa magonjwa ya pamba pamoja na kutoa elimu kwa wakulima ili kufikia malengo ya kilimo bora Tazania hivyo kuwataka wakulima kutokusita kuwafuata pale wanapohitaji msaada kutoka kwao kama wataalamu.

Pembejeo za kilimo muhimu yaani mbolea, madawa na mbegu bora ni changamoto inayowakabilil wakulima wengi nchini iwapo  zinaendelea kupatikana kwa mawakala binafsi ambao huleta kufuatana na mahitaji na ununuzi kutoka kwa wakulima. Hata hivyo pembejeo nyingi zinapatikana makao makuu ya mikoa na wilaya, na chache katika maeneo ya vijijini.  Japo ipo sababu ya kuendelea kuhamasisha wakulima kutumia pembejeo ili kuongeza tija katika kilimo. Vilevile kuhamasisha wafanya biashara wenye uwezo kifedha maeneo ya vijijini na vyama vya kuweka na kukopa kuwa mawakala wa pembejeo kwakuwa asilimia kubwa ya wakulima wapo vijijini na si mjini. Serikali pia itoe kipau mbele kwa mawakala waishio vijijini kupata pembejeo kwa wingi na kwa haraka ili kwenda sambamba na msimu wa kilimo.
Hata hivyo, mabadiliko ya sayansi na teknolojia pamoja na sera ya uchumi wa huria duniani ambayo Tanzania haikuwa imejiandaa kikamilifu ilifanya viwanda vyake vishindwe kuhimili kishindo. Kitu ambacho kimewaacha watu wengi kupoteza ajira zao hata kwa upande wa kilimo ambacho mapaka sasa bado ndio mkombozi kwa watanzania. Hivyo serikali inatakiwa kujipanga na kujidhatiti katika kilimo ambacho ndio tegemeo la wengi.