Ndugu wanahabari
Sote tunaelewa kuwa kwa matakwa ya CCM, Bunge Maalum la Katiba (BMK)
limeendelea kufanya vikao vyake mjini Dodoma kuanzia Agosti 5 mwaka huu,
kinyume kabisa na matarajio ya Watanzania, ambao kupitia fursa
mbalimbali wamepaza sauti zao wakisisitiza maridhiano na mwafaka wa
kitaifa kutangulizwa mbele badala ya maslahi ya watawala.
Tukiwa viongozi wa kisiasa ambao ni sehemu ya uongozi ndani ya jamii,
wenye wajibu wa kuwa na maono chanya na muhimu kwa taifa letu,
tumeendelea kufuatilia kwa karibu namna mchakato wa Katiba Mpya
unavyoendelea kunajisiwa kupitia vikao hivyo vya BMK linaloendelea mjini
Dodoma, likitumia rasilimali za taifa, zikiwemo kodi za Watanzania
wanyonge, kujadili vitu visivyotokana na wananchi.
Mtu
yeyote makini ataweza kubaini kuwa kwa namna mchakato wa Katiba Mpya
unavyopelekwa au unavyokwenda kwa sasa ni matokeo ya kukosekana kwa
uongozi wa kisiasa kwa Chama kinachoongoza Serikali, CCM.
Kuna
ombwe kubwa la uongozi wa kisiasa katika jambo hili. Ni kama vile
mchakato unajiendea tu wenyewe bila mwongozo wowote kutoka kwa watu
walioko madarakani ambao wananchi walitarajia wangetumia mamlaka yao ya
dhamana ya uongozi ili taifa lipite salama katika wakati huu mgumu na
tupate Katiba Mpya na bora.
Vipo viashiria vingi tu vinavyoweka wazi hali hiyo ya ombwe la uongozi
wa kisiasa katika mchakato huu wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na kauli
kinzani za viongozi wa Serikali na CCM yenyewe.
Wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza kama vile kunahitajika
mazungumzo zaidi na kwamba suala la muundo wa serikali lilipaswa
kupigiwa kura kabla, Mwenyekiti wa BMK anaendelea kuongoza bunge kama
vile mchakato ni mali binafsi ya CCM na walioko madarakani.
Wakati
baadhi ya viongozi wa Serikali ya CCM wakitoa kauli za kuhitaji kuwa
makini na taratibu za kuendesha mchakato huu chama chao kinatoa kauli za
kuzidi kuharamisha na kutia najisi mchakato mzima. Mchakato unakwama,
nchi inayumba, Watanzania wako katika sintofahamu kwa sababu tu tumekosa
uongozi wa kisiasa katika jambo hili.
Kiashiria
kingine cha pengo hilo la uongozi wa kisiasa ambacho kwa kweli kwetu
sisi kimetusikitisha zaidi kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kuendelea na
‘hamsini zake’ kama vile nchi haina tatizo lolote.
Yaani
wakati nchi na wananchi wako katika sintofahamu ya hatma ya Katiba Mpya
itakayoweka misingi ya wao kujitawala na kuongozwa watakavyo, makundi
mbalimbali yakipaza sauti zao, mataifa mengine yakituangalia kwa makini
na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wakifuatilia mchakato, Rais
Kikwete anapata muda wa kutembelea ranch ya Rais Mstaafu wa Marekani
George Bush!
Wakati
Rais Kikwete akiendelea kutalii dunia, wenzake wako mjini Dodoma
wakichukua posho kwa kazi ambayo wananchi hawajui wanaifanya kwa maslahi
ya nani!
Kwa ujumla mambo yote yanayoendelea sasa katika mchakato huu ni matokeo ya ombwe hilo kama tulivyosema.
Inaonesha kuwa CCM wamelewa madaraka na viongozi wanaona dhamana ya
uongozi iko juu ya wananchi hivyo hawajali umuhimu na nafasi ya mamlaka
ya wananchi katika kuamua mstakabali wa taifa lao kwa ajili ya kizazi
cha sasa na kuweka msingi wa vizazi vingi vijavyo.
Hivyo leo tungependa kuzungumza tena kuhusu Rasimu ya Katiba na mchakato wenyewe hapa ulipokwama;
Tunapenda
kusema wazi kuwa tumeshangazwa sana na kitendo cha CCM na Serikali yake
kulazimisha kuendelea kwa Bunge Maalum la Katiba Mpya, tena kwa mtindo
ule ule wa kunajisi na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu
ya Pili ya Katiba Mpya kama yalivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
Wamefanya
hivyo pasi na kujali kilio cha wananchi kinachopazwa kutoka kila kona
ya nchi, ambapo Watanzania mmoja mmoja na katika makundi mbalimbali
wametaka maoni yao yazingatiwe kwa kujadiliwa, kuboreshwa na kisha
kupitishwa na Bunge Maalum la Katiba kabla wao hawajayapigia kura ya
maoni kwa ajili ya kuipitisha au kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya.
Wajumbe
wanaotokana na CCM pamoja na makada wengine wapatao 166 wa chama hicho
ambao waliteuliwa kuingia kwenye bunge hilo kusimamia maslahi ya CCM
kupitia kundi la wajumbe 201, wameamua bila haya mbele ya umma si tu
kupuuza rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi bali sasa wameamua
kuingiza mambo yao waliyodhamiria tangu mwanzo kwa kadri ya maamuzi na
maelekezo ya vikao vya chama hicho vikiongozwa na Mwenyekiti wao Jakaya
Kikwete.
Bila
kujali wala kuguswa na miito ya Watanzania mbalimbali wanaotaka jambo
hili liongozwe na maridhiano kwa ajili ya mwafaka wa kitaifa badala ya
kuweka matamanio ya watawala mbele, CCM na mawakala wao katika mchakato
huu wameendelea pia kufuja na kutumia vibaya fedha za wananchi kupitia
Bunge Maalum la Katiba kwa kujadili na kuingiza vitu visivyokuwemo au
visiyotakiwa kuwa sehemu ya rasimu hii iliyopo sasa.
Hali hiyo
imefanyika kwa namna kadhaa ikiwa ni pamoja na kutofuata sheria
inayosimamia mchakato mzima, kubadili kanuni za uendeshaji wa BMK hasa
katika taratibu za kujadili na kupitisha ibara na kubwa zaidi kuingiza
masuala ya Tanganyika kwenye Rasimu ya Katiba ya Muungano.
Kimsingi
masuala wanayoyajadili na kuyachomeka kinyemela kwenye Rasimu ya Pili ya
Warioba, mathalan masuala ya Ardhi, Elimu, Maji, Kilimo, Uvuvi, Mifugo,
Serikali za Mitaa nk ni masuala yanayopaswa kuandikwa kwa kina ndani ya
Katiba ya Tanganyika na siyo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni vyema
kukumbuka kuwa Zanzibar walijadili wenyewe mambo Yao ya Ndani na
kutengeneza Katiba yao na hatuoni mantiki ya kuruhusu Wajumbe toka
Zanzibar kujadili na kuamua mambo ya Tanganyika. BMK haina Sifa ya
kujadili yasiyo ya Muungano.
Hivyo
tofauti na wanavyotaka kujionesha katika jamii, CCM kupitia BMK wameamua
kupindua kabisa rasimu nzima na kuweka maazimio ya vikao vyao kuwa
ndiyo Katiba ya Tanzania. Jambo hili haliwezi kukubalika.
Kutokana na uchakachuaji huo wa Katiba Mpya unaoendelea kufanywa na CCM kupitia BMK, UKAWA tumefikia maamuzi yafuatayo;
· Tunamtaka Rais Jakaya Kikwete asitishe shughuli za BMK mara moja lisiendelee kuvuruga
na kuharibu mchakato wa Katiba Mpya na kuiweka nchi katika sintofahamu juu ya jambo hili
nyeti;
· Tunamtaka Rais Kikwete asitishe BMK ili lisiendelee kufuja fedha za Watanzania maskini
wanaopigania Katiba Mpya iwapatie matumaini ya kuongozwa na kujitawala wanavyotaka.
· Tunamtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum
kwenye matumizi ya fedha za BMK ambayo kuanzia Bunge la Bajeti lililopita tumebainisha
wazi kuwa yana uvundo mkubwa wa ufisadi na hayana maelezo sahihi.
· Iwapo Rais Kikwete atashindwa kutumia mamlaka yake kusitisha BMK na hivyo likaendelea
kinyume cha matakwa na maslahi ya wananchi kama lilivyofanya awali na linavyofanya sasa,
UKAWA tutawaongoza Watanzania kupaza sauti zaidi kupinga najisi inayotiwa kwenye maoni
yao, kupitia maandamano na mikutano ya hadhara nchi nzima.
Asanteni kwa kutusikiliza.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti CUF
Freeman Aikaeli Mbowe
Mwenyekiti CHADEMA
James Francis Mbatia
Mwenyekiti NCCR Mageuzi
Wilbrod Peter Slaa
Kny Makatibu Wakuu, UKAWA.