Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya
siku ya kimataifa ya Amani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh.
Seif Rashid akiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuhudhuria
maadhimisho hayo na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Albino
Tanzania (TAS), Joseph Masasi (wa pili kulia), Kamishna wa Ustawi wa
Jamii, Bw. Dunford Makala (katikati) na Kamishna wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora Tanzania , Bw. Ali Rajab (kulia) pamoja na
viongozi wengine taasisi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinizim)
WAKATI Katibu Mkuu wa umoja wa
mataifa Ban Ki-moon anahimiza serikali duniani kutafuta chanzo cha
kukosekana kwa amani na kuongezeka kwa watu wenye misimamo mikali,
wasemaji katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa amani Duniani wameitaka
serikali ya Tanzania kutupia macho makali mauaji ya albino nchini.
Akimwakilisha Katibu mkuu wa Umoja
wa Mataifa katika adhimisho lililofanyika viwanja vya Mnazi mmoja leo
Mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi mkazi wa UNDP nchini
Alvaro Rodriguez, alisema ili kudumisha amani kuna mambo mengi
yanatakiwa kufanyiwa kazi hasa kutambua chanzo cha migogoro
inayosababisha msuguano mkubwa katika jamii na kukosekana kwa amani.
Alisema amani ina maana kubwa kwa
jamii na ndio maana Umoja wa mataifa miaka 13 iliyopita iliamua
kuadhimisha siku hiyo kwa lengo la kushawsihi makundi yanayosigana
kupata nafasi ya kuzungumzia na kuona maana ya amani.
Alisema pamoja na kuwepo kwa hatua
kubwa tangu kupitishwa kwa azimio la Umoja wa Mataifa la kuadhimisha
amani, safari ya kufikia amani ni ndefu na ili kufanikiwa pande zote ni
lazima kwenda hatua kwa hatua kwa kushirikiana.
Alisema mafanikio ambayo
yamepatikana ni pamoja na UN kufanikiwa kufundisha kada ya habari juu ya
uandishi katika mazingira tete na kusaidia majadiliano ya kitamaduni
yanagusa masuala ya amani.
Mtaalam wa Mahusiano na
Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce Temu (katikati)
akimtambulisha Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na
mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini,
Alvaro Rodriguez (wa pili kushoto) mara baada ya kuwasili kwa Katibu
Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania
(THBUB), Bi. Mary Massay.
Aidha alisema kwamba wanafanyakazi
na Wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha kwamba wanastawisha mipango yote
inayolenga kuzuia ghasia na kuboresha mipango inayoimarisha amani.
Akihutubia bada ya mashuhuda
kuzungumzia hali ya tishio la amani nchini Tanzania hasa la kukosekana
kwa amani miongoni mwa watu wenye ulemavu wa ngozi albino, Mwakilishi
huyo wa Umoja wa Mataifa aliipongeza serikali ya Tanzania kw ajuhudi
zake za kuimarisha amani katika kanda ya maziwa makuu na kushiriki
katika operesheni mbalimbali za Umoja wa Mataifa ziliziolenga kuleta
hali bora zaidi ya maisha kwa watu wanaoishi katika hekaheka za kivita.
Akiwa na mwezi mmoja tangu awalisili
nchini mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini amesema kwamba
anatarajia kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na wananchi wa
Tanzania kuhakikisha taifa la Tanzania linaendelea kuwa na amanai
Wakati Mwakilishi huyo amesema
kwamba watu wengi duniani wanawaonea gere wananchi wa Tanzania kwa amani
wlaiyonayo, mwakilishi wa Under the Same Sun, Vicky Ntetema ametaka
kupitiwa upya kwa sheria ya uchawi ya mwaka 1928 iliyofanyiwa mabadiliko
mwaka 2002 ili kukabiliana na mauaji ya albino nchini ambayo kwa kiasi
kikubwa yanachochewa na waganga wa kienyeji.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya
Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akisalimiana na Mgeni rasmi
kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Mh. Seif Rashid meza kuu.
Alisema sheria hiyo ina mwanya
mkubwa wa wauaji kucheza nayo na kusababisha sehemu kubwa ya kesi
zilizopo kushindwa kuwatia hatiani wahusika.
Alisema wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu mauaji ya albino na ukataji wa viungo umeongezeka.
Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi
25 za afrika zinazofanya ukatili dhidi ya walemavu wa ngozi, toka mwaka
2006 watu 74 wameuawa, 56 wamenusurika na 11 wameongezewa ulemavu huku
makaburi 18 ya albino yakinajisiwa kwa kufukuliwa.
Watu wa kituo cha haki za binadamu
wamesema pamoja na kuwepo na matukio 120 ya ukatili dhidi ya albino kesi
11 tu ndio zilizofikishwa mahakamani huku tano zikiwa zimekatiwa hukumu
ambazo hazijaridhisha.
Vicky alisema katika matukio yote
hayo chanzo ni ushirikina lakini kutokana na kukosekana zimeshindikana
kuzimaliza zinavyotakiwa.
Brass band ya jeshi la Magereza
ikiongoza maandamano ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya amani
wakiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam wakati wa
maadhimisho hayo jana.
Vicky aliitaka jamii kuwalinda
albino kwani serikali pekee haiwezi kufanya kitu chochote huku akisema
kwamba hesabu ya albino mmoja katika kila wananchi 1,400 haiwezi
kulindwa kwa dhati na serikali kutokana na idadi ya polisi kutokua sawa
na wananchi.
Aidha alishauri serikali kutoa
msaada wa kisheria kwa waathirika kabla ya kuingia mahakamani ili waweze
kusimulia vyema kadhia zao na pia wasiangushwe na wanasheria ambao
wanatumia udhaifu wa kisheria kuwatoa watuhumiwa hatiani.
Pamoja na Vicky Ntetema kushawishi
wananchi kulinda albino na kuwafichua wauaji Kaimu Mufti Sheikh Ismail
Habibu Makusanya ameitaka serikali kuhakikisha kwamba kila mwananchi
anapata utulivu wa kutosha kuendelea na shughuli zaka na kuhimiza
mahakama kutenda haki.
Aliwakumbusha wananchi kama
alivyosema Sydina Omar kwamba kila mmoja ataulizwa amefanya nini
kukomesha madhila katika jamii wakati wa kiama na kusema serikali
isipowajibika itasema nini na wananchi nao pia watajibu nini.
Pichani ni baadhi wadau kutoka
taasisi mbalimbali pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism)
wakiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja huku wakiwa wamebeba mabango
yenye jumbe mbalimbali za kuhamasisha amani nchini na kupinga mauji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism) nchini wakati wa maadhimisho ya
siku ya kimataifa ya amani iliyofanyika jana jijini Dar.
Alisema amani hailetwi kama mvua ,
inatafutwa na kusema watu wasipotafuta amani na kuhakikisha amani
inakuwapo itakuwa shida kubwa kwa taifa hili ambalo miaka yote
limeogelea katika bahari ya amani.
Aliwasihi waumini wa Kiislamu na wananchi wengine kuhakukisha kwamba amani inakuwa ajenda ya kudumu kila wanapokutana pamoja.
Katika maadhimisha hayo ambapo
wananchi walianza maandamano shule ya Uhuru Mchanganyiko hadi viwanja
vya Mnazi mmoja, mgeni rasmi Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii Dk Seif
Rashid alisema serikali imejipanga kuhakikisha inakomesha mauaji ya
albino na kuwataka wananchi kuisaidia kwa kutokuwa waoga kutoa ushahidi
na pia kuwaripoti watuhumiwa.
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya
haki ya amani kwa watu wote, komesha mauaji ya albino inahamasiaha umma
wa Tanzania kulaani,kukemea na kukomesha mauaji kwani yanakwenda
kinyume na katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 14 ambayo inaeleza
kwamba kila mtu ana haki ya kupata hifadhi katika jamii.
Aidha waziri alitaka kutekelezwa kwa
agizo lake kuhusu tiba mbadala na za asili na kusema serikali
itaendelea kulinda amani na kutoa ulinzi kwa wathirika.
Meza kuu ikipoeka maandamano ya siku ya kimataifa ya amani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Albino Tanzania (TAS), Joseph Masasi akitoa neno la ukaribisho kwa mgeni
rasmi Mh. Seif Rashid (wa pili kulia). Kutoka kushoto ni Mratibu Mkazi
wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, Kamishna wa Ustawi
wa Jamii, Bw. Dunford Makala, Balozi wa Uturuki nchini, Mh. Ali
Davutoglu.
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya
siku ya kimataifa ya Amani, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh.
Seif Rashid, akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya
amani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya
Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, akisoma ujumbe wa Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon kwenye maadhimisho ya siku ya
kimataifa ya amani duniani.
Mratibu Mkazi wa mashirika ya
Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akipongezwa na Balozi wa Uturuki
nchini Tanzania, Mh. Ali Davutoglu baada ya kusoma ujumbe wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la
UNDER THE SAME SUN, Vicky Ntetema akisoma risala yake kwa mgeni rasmi
wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani iliyofanyika jana
jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mufti Sheikh Ismail Habibu
Makusanya, akizungumza kwenye maadhimisho hayo ambapo alilaani vikali
mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinizim) na kusema kuwa watu
wote wanaoshiriki katika mauaji hayo kamwe hawatoiona Pepo ya Mwenyezi
Mungu.
Balozi wa Uturuki nchini
Tanzania, Mh. Ali Davutoglu akisoma ujumbe kwa niaba wa umoja wa
mabalozi kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani duniani.
Baadhi ya wadau kutoka taasisi na asasi mbalimbali nchini walioshiriki kwenye maadhimisho hayo.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki
za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania (THBUB), Bi. Mary Massay
akitoa nasaha kutoka kwa Tume hiyo, ambapo alitoa rai kwa mtu yeyote
yule ambaye ana malalamiko au matatizo katika Haki za Binadamu
anakaribishwa kwenye tume hiyo kwa ajili kupata msaada wa kisheria.
Shuhuda aliyenusurika kwenye
mauaji ya Albino ambaye amekatwa mikono yote miwili, Mariam Stanford
akitoa ushuhuda wake na killio chake mbele ya meza na wageni waalikwa
waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani
iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Mnazi mmoja.
Mke wa Balozi wa Uturuki nchini
Yesim Davutoglu, akilia kwa uchungu baada ya kusikia shuhuda kutoka kwa
mhanga wa mauaji ya Albino aliyekatwa mikono yote miwili, Mariam
Stanford (hayupo pichani) ambaye hadi sasa anapewa matunzo na Shirika la
Under The Same Sun.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la
UNDER THE SAME SUN, Vicky Ntetema akimfariji mke wa Balozi wa Uturuki
nchini Yesim Davutoglu, wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya
amani duniani iliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar.