''Watu wote duniani huwa tuna ndoto za kufanya kitu fulani lakini tumejikuta ndoto hizo
hazijitokezi bayana kwa sababu ya kukosa UTHUBUTU''.
Migogoro ni ukinzani unaotokana na utofauti wa kiitikadi juu ya watu waaminio juu ya jambo fulani.
Mahusiano ni ukaribu wa watu ambao wana ushabihiano wa dhamira moja aidha dhamira ya kazi, au mapenzi mpaka ndoa.
Migogoro haiepukiki. Katika maisha lazima migogoro itokee kwa
sababu ya mambo mbalimbali kama vile kitabia. Lakini wakati huo huo
migogoro kwa wakati fulani ni mizuri kwani hutusaidia katika:
* Kujitambua
* Kujichuja kujua tabia ya mtu alivyo
* Husaidia kujua msimamo wa mtu mwingine
* Husaidia kuchomoza kwa mtu mwingine
Migogoro ya kimahusiano mahali pa kazi, familia na mapenzi
hujitokeza na lazima itokee kila tunapokutana katika mzunguko wa maisha
ya kila siku.
SABABU ZA MSINGI ZA MIGOGORO KATIKA MAPENZI NA KAZI:
1> Maeneo tutokayo na tuzaliwayo.
Utofauti wa maeneo ni chanzo cha migogoro kwa sababu kila jamii au familia huzaliwa katika mitazamo
fulani, au uthamani fulani. Hivyo utofauti huo huleta migogoro.
Mfano: Mtu kutoka mikoa ya kusini mwa Tanzania hutofautiana kimtazamo,
thamani na muonekano wake na aliyetoka mikoa ya kaskazini (Kilimanjaro),
hivyo tukutanapo katika maeneo ya kazi na mapenzi huleta migongano
awali kisha baadae hupoa.
Hivyo uzoefu unaonyesha kuwa kama umetoka katika familia inayoongozwa na upendo basi hata wafuasi
wa familia hiyo kwa kiasi kikubwa wataongozwa na upendo, lakini mambo yakiwa kinyume na hapo
basi kazini na hata katika mapenzi itakuwa Pakistani.
2> Muonekano (personality)
Binadamu hutofautiana. Tumetofautiana katika maeneo makuu manne (katika mawasiliano).
# Namna tunavyotenda mambo yetu, katika kundi hili wapo wanaotenda mambo yao haraka wengine
kwa wastani na wengine taratibu, hivyo hata katika mapenzi tofauti hizi hujitokeza.
# Tofauti katika mapenzi: Katika uga huu hutofautiana kwa kiasi kikubwa kwani wapo wanaopenda
kubembelezwa na wale wasiopenda kubembelezwa, wengine wapo kimvuto zaidi na wengine hapana.
# Masuala ya uchumi na fedha. Watu hutofautiana katika kupata fedha. Katika suala zima la kutunza
utumizi wa pesa, migogoro mingi katika familia nyingi Tanzania na duniani husababishwa na fedha kwani
watu hutofautiana. Wapo wanaojua kutafuta na kuzitumia fedha, wapo wanaozitafuta na wanakuwa
wabahili wengine wanaweza kuzitafuta na watafunaji wazuri, Hivyo mtazame vyema mwenza wako na
umjue ili muweze kusuluhisha tatizo.
3> Matarajio (expectations)
Jambo jingine linalosababisha migogoro katika maisha ya kimahusiano ya kikazi na katika kimapenzi ni
matarajio. Watu wengi huwa na matarajio fulani lakini wengi wao wanapoingia na kukuta ndivyo sivyo
na matarajio, huibuka migogoro.
Mfano kama unaomba kazi unategemea mshahara mzuri na kukuta sivyo, basi hapo ndipo mgogoro huibuka.
4> Kukosa Imani (lack of trust).
Kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watu katika maeneo ya kazi na mahusiano huzua migongano.
Katika maeneo ya kazi uaminifu unapotoweka ndipo makundi na unafiki huibuka, pia katika mapenzi
msipoaminiana lazima kutakuwa na migogoro. Kama miongoni mwenu kuna hisia kuwa unachezea timu
mbili basi utaibua mgogoro. Tambua kuwa katika maisha hakuna jambo zuri kama THAMANI;
Usimchukulie poa mpenzi wako. Daima elewa kuwa kupenda na kupendana ni kuonesha udhaifu ulio
nao kwa umpendaye. Katika mapenzi hakuna kuchukuliana poa.
Tambua kuwa duniani kuna watu ambao huamini kuwa dunia inaweza kusimama kwa kupiga mluzi, yaani
kila wanachokisema wao wako sawa na wana haki, watu wa aina hii wanapoingia katika mahusiano basi
huwa ni hatari. Tabia hii ni heri akawa nayo mwanamme kuliko mwanamke.
5> Ubinafsi (selfishness)
Watu wengi wana tabia ya ubinafsi hivyo wanasababisha migogoro katika mahusiano ya kimapenzi.
Hivyo unapokutana na mtu wa aina hii basi umeumia. Unaweza kuona umekosea na huwezi kuonekana
kuwa hujui lolote. Watu wa aina hii hata ukimwambia... I MISS YOU...!
Utasikia: kheeee! Leo umejifunza wapi?... Hivyo unaweza kuwa mtumwa, mwisho huchoka. Ipo athari
kama moyo uliopenda ukichoka hasa wa mwanamke kama vile:
@ Moyo wa mwanamke uchokapo ni kama bomu, kwa sababu huingiza maumivu na kutengeneza uvungu
ambao hutengeneza bomu linalosubiriwa kulipuka.
@ Wanaume wao hubeba mambo, wanapotaka kulipuka hujulikana mapema.
@ Elewa uwekezaji mkubwa katika mapenzi kwa mwanamke ni hisia hivyo mwanamke anapoikosa basi
hufanya chochote ili aipate. Hivyo wanaume wanatakiwa kuwatunza, kuwathamini na kuwajali vyema
wake zao. Na uwekezaji mkubwa wa wanaume katika mapenzi ni hisia na fedha, daima moyo uwapo
katika vuguvugu za kukosa amani basi utafanya ufujaji katika pesa kwa kununua vitu vya thamani ili
kuitafuta amani iliyopotea, Je? Wanawake wangapi ambao wana magauni mapya ya thamani ambayo
hayajavaliwa bado na wanaendelea kununua?
Tambua kuwa moyo uchokapo lazima utaingia katika DUARA la
umasikini pia elewa kuwa vurugu vurugu za maisha zipo kila iitwapo leo,
hivyo ukizikubali vurugu hizo zivunje miguu ya moyo wako utakuwa hoi
kutumika.
VITU VYA KUFANYA ILI KUONDOKEWA NA MIGOGORO KATIKA MAPENZI NA KAZI:
Vipo vichocheo viwili ambavyo huweza kuondoa migogoro katika mapenzi na kazi, ambavyo ni:
a) Vitu tunavyoweza kufanya katika hatua yeyote ile (mahali popote)
b) Jinsi ya kutengeneza mahusiano (mapenzi) yenye afya.
Jambo muhimu daima ni kuwa tuingiapo katika mahusiano na kazi, kumpenda
mtu hatutarajii kuumia na kuteseka. Yatafakari haya kwako na mengine
hapo baadae.
Kisaikolojia hunenwa kuwa lazima uanze na wewe mwenyewe ndipo uende kwa
mwingine. Watu wengi maishani hutumia muda mwingi kuwabadilisha wengine
badala ya kuanza na wao wenyewe.
Hivyo uonapo hapo ulipo hapakufai anza kuleta mabadiliko wewe.
Vitu vya kufanya katika hatua yeyote ile:
* Kuwa mtu mzima (grow up)
Hapa haina maana kuwa mtu mzima ni kuwa na ndevu (mabadiliko ya
kibaiolojia), bali ni uwezo wa kusimamia mambo yako. Mtu mzima hahukumu
watu wengine anapopatwa na migogoro. Mtu mzima hukubali makosa na
kufikiria nafasi nyingine yenye usalama zaidi juu ya mahusiano yake.
* Muombe Mungu akukuze, akupe busara na upeo.
Daima muombe Mungu akupe upeo na busara chanya ili uwe na uwezo wa
kuchuja na kuacha mawazo mabaya. Elewa kuwa duniani watu waliofanikiwa
ni wenye busara na upeo katika maamuzi yao.
* Jikubali namna ulivyo.
Kwa bahati mbaya katika maisha wengi wetu hudanganya, na mpaka
hujidanganya wao wenyewe. Katika kufanikiwa usijidanganye. Angalia
mapungufu ulio nayo na uyafanyie kazi, kubali vitu usivyoviweza kisha
fanyia kazi ili uweze.
*Uwe tayari kujishusha.
Kuwa na tabia ya kuangalia na kusikiliza lakini si kwa kila kitu. Tambua siku zote kuwa ''kusikia si kuona na kuona si kweli''. Daima hakikisha kuwa unajua nini kinaendelea. Pia kuwa mnyenyekevu ingawa kitu kigumu duniani ni kuwa mnyenyekevu.
Watu wengi huona kuwa mtu mnyenyekevu ni mtu aliyeshindwa au ni muoga. Tambua kuwa kukubali ndio ushindi. Kwa nini ubishane?
Unyenyekevu katika mahusiano hususan katika mapenzi ni moja ya silaha kuu ambayo itaufanya uhusiano wenu kuwa wa mfano. Daima
unyenyekevu utawavusha katika mpando na mshuko wenu katika mahusiano.
Mungu akiwapa neema hii (unyenyekevu) basi mtakuwa imara na wa mfano
katika ndoa yenu.
b) Kichocheo cha pili.
Ni namna ya kujenga mahusiano yenye afya njema. Kila binadamu hupenda
thamani yake ipande kila iitwapo leo lakini watu hushushana kila siku.
Kila binadamu hupenda, hupendwa na kuthaminiwa.
MISINGI YA KUTENGENEZA MAHUSIANO YENYE AFYA.
a] Mkubali mpenzi wako.
Kama unahitaji kupendwa lazima umkubali mpenzi wako. Mtu anayemkubali
mpenzi wake huyo hujiheshimu. Mtu anayejiheshimu hawezi kumdhalilisha
mwingine kwani unapomdhalilisha hujidhalilisha mwenyewe.
b] Mheshimu na jiheshimu mwenyewe.
Mtu anayejiheshimu hatumii lugha chafu, huonesha heshima yake kuwa mwanzo wake. Hateremshi chupi ovyo ovyo.
c] Onesha mapenzi kwa kila hali.
Tambua kuwa unapompenda mtu hii humaanisha kuwa umemkubali na umekubali
vitendo vyake, namna anavyosema n.k. Wasilisha upendo wako kwa namna
zote iwe katika kuongea ama kushirikiana, kuweni marafiki. Neno
samahani, ashakum si matusi.
Ngoja niulize kidogo.
'Ni nani yupo tayari kujamba mbele ya mpenzi wake?' (wote kimya)
Mkifikia hapa mjue mpo huru na mnapendana; ukiwa na hofu tambua kuwa
hakuna upendo. Daima upendo huanzia machoni, kwenda kinywani, kisha
huishia moyoni ambako hutulia tuliiii!!!!!. Bahati mbaya siku hizi
mapenzi huanzia katika zipu au mfukoni.
d] Pokea na utoe mapenzi.
Ukiona kuwa wewe ni wa kutoa au kupokea mapenzi siku zote za mahusiano yenu basi unatakiwa uondoke mapema. Au anza upya.
e] Jipende mwenyewe.
Kumbuka kuwa huwezi kufanya mambo yote haya kama hujipendi wewe
mwenyewe. Kama utajipenda wewe mwenyewe basi utajua namna ya kupenda.
Ukimuona au ukisikia mtu anasema kuwa yuko tayari kufa kwa ajili yako
huyu achana naye maana huweza kukuacha pia hata wewe ukitokwa na uhai.
Pia kama mpenzi wako amekugeuza baba au mama basi achana naye. Omba
Mungu akupe uwezo wa kumpenda na uwezo wa kuwa mkamilifu siku zote.
Nyakati zote muombe Mungu, ukiwa katika unyenyekevu.
f] Daima muombe Mungu.
Daima omba Mungu kwani yeye hutuwazia mambo mema siku zote na majibu yake huwa ni ndiyo, si sasa na nina mawazo au mpango mzuri.
DONDOO MUHIMU:
// Uvumilivu katika mapenzi ni muhimu. Elewa kwa moyo uliopenda hauchoki wala kuhukumu, uko hai siku
zote.
// Unapoamua kumsamehe mtu samehe na kusahau. Na kama hujamsamehe kwa wakati huo mwambie ili
ajue na atafute mbinu m'badala ya kukuomba radhi.
// Zipo tabia ambazo hutokana na mazingira, kaeni chini muelimishane.
// Usione aibu katika mapenzi, elezaneni ukweli.
// Jifunzeni kutafuta chanzo na kiini cha tatizo.
// Ni vyema kuwa na mahusiano yenu binafsi. Pia kuelewa ndio jambo muhimu katika maisha.
// Usiingie katika mapenzi (mahusiano) kiupofu.
// Msome mwenzi wako.
// Mapenzi ni namna unavyomuonesha, unavyosema, matendo na ukifanyacho juu ya umpendaye. Fanyia kazi
mahusiano yako.
// Pesa ni upendo siku zote. Usikubali kuingia katika mahusiano kwa sababu ya pesa.
// Mawasiliano ni muhimu. Muulize mpenzi wako namna anavyotaka apendwe na wewe .
// Nyumba ndogo ni hatari.
// Mtu anayependa kweli hachoki. Mtu hupenda mara moja.
// Usiingie ukurasa mpya wa mapenzi mapya kabla ya kuufunga wa awali.
// Elewa kusamehe na kusahau ndiyo nguzo ya mahusiano.
// Utandawazi usitufanye tuache mila na desturi za upendo wa kifamilia au kuwapeleka kwa bibi na babu.
// Mpenzi wako akifunga virago pengine anahitaji SAIKOLOJIA PUMZISHI (rest psychology) akizidi
mueleze kuwa siku nyingine ukienda nitakuacha uende jumla.
// Msaidie kujaza imani iliyotoka juu ya mapenzi.
// Elewa kuwa watoto wana haki ya kuona baba na mama hata kama mkiachana.