Miss Tanzania 2014 aliyevuliwa taji, Sitti Abbas Mtemvu akipanda jukwaani kupata maombi ya Nabii Yaspi Bendera.
Stori: Chande Abdallah, Deogratius Mongela na Musa Mateja.
TENA! Saa
chache tu baada ya Miss Tanzania 2014 aliyezua tafrani la kuchakachua
umri kwa kujipunguzia miaka 2 ya kuzaliwa, Sitti Abbas Mtemvu
kujisalimisha kwa kujivua taji mwenyewe, mapya yameibuka na Ijumaa
Wikienda lina mzigo mkononi!
Mapya
hayo yameibukia ndani ya Kanisa la Revelation Church lililopo
Buza–Kipera jijini Dar kwa Nabii Yaspi Bendera ambaye amezungumzia ishu
ya Sitti kujivua taji mwenyewe.“Alikuja
kwangu nikamwombea, akapata taji. Hata alipopata alikuja kushukuru,
nilimwambia aendelee kudumu kwangu hadi atakapokwenda kwenye taji la
dunia (Miss World) lakini hakufanya hivyo, akawa haji tena.“Hivi,
nitoe mfano mmoja. Kama mtu akienda kwa mganga kuomba apewe dawa ili
apate ujauzito, akishapata akaenda kwa mganga mwingine kuomba amfanyie
dawa ili ujauzito huo usitoke. Je, siku ukitoka nani analaumiwa, mganga
wa kwanza au wa pili?”
Aliyekuwa Miss Tanzania 2014 akipokea maombi ya nguvu kutoka kwa Nabii Yaspi Bendera
TAFSIRI YAKE HAPA!
Kwa
tafsiri rahisi sana ya mazungumzo ya nabii huyo, Sitti alikwenda
kanisani kwake akaomba baraka ili ashinde taji la Miss Tanzania,
akashinda lakini baadaye alihama kanisa na kwenda kusali kwingine mpaka
alipovua taji.
Nabii
Yaspi aliandelea kudai kwamba, kama Sitti angeendelea kudumu kwenye
kanisa lake na kuombewa maombi ya nguvu, asingevua taji na angefanikiwa
kwenda Miss World 2015 ambako pia angetwaa taji la dunia.
Lakini
baada ya kutwaa taji alienda kanisa jingine akiwa na taji lake, matokeo
yake mambo yakawa magumu mpaka alipolazimika kuvua taji hilo.
Nabii Yaspi Bendera akimkumbatia Sitti Abbas Mtemvu.
KUMBE ALISHAONYWA
Habari
nyingine kutoka kwa mtu asiye msemaji wa kanisa hilo zinasema kuwa,
baada ya kutwaa taji, Sitti alionywa na Nabii Yaspi kwamba kutaibuka
vikwazo katika nafasi yake hiyo lakini alichotakiwa kufanya ni kudumu
katika maombi ya kanisa hilo ili vikwazo hivyo vifutike lakini kwa
sababu hakufanya hivyo matokeo yake ni hayo!
SITTI AMEFIKAJE HAPA?
Siku
chache baada ya Sitti kutwaa Taji la Miss Tanzania 2014 katika shindano
lililochukua nafasi ndani ya Ukumbi wa Mlimani City, Dar, Oktoba 11,
mwaka huu, yaliibuka madai kwamba, mrembo huyo alichakachua umri akidai
ana miaka 23 wakati ana miaka 25.
Mwenyekiti wa kamati ya Miss Tanzania, Hashimu Lundenga akijibu hoja kutoka kwa wanahabari
Sheria za Miss Tanzania, mrembo mwenye miaka 25 haruhusiwi kushiriki mashindano hayo.
Katika
madai hayo, ilisemekana kwamba, mrembo huyo alizaliwa Mei 31, 1989
kwenye Hospitali ya Aga Khan jijini Dar. Lakini yeye cheti
alichokipeleka kwenye Kamati ya Miss Tanzania akidai alikipata kwa
Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kilionesha mlimbwende huyo
alizaliwa Mei 31, 1991 hivyo ana miaka 23.
PASPOTI NDIYO CHANZO
Mazito
yote yaliyompata Sitti, chanzo ni hati yake ya kusafiria (paspoti)
ambayo ilibandikwa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha mrembo huyo
ambaye ni binti wa Mbunge wa Jimbo la Temeke kwa tiketi ya CCM, Abbas
Mtemvu, alizaliwa Mei 31, 1989.
Mrithi wa Miss Tanzania 2014, Lillian Kamazima akiwa ni mwenye furaha.
KESI BADO MBICHI!
Katika
barua yake kwa Kamati ya Miss Tanzania aliyoiandika Novemba 5, mwaka
huu na kufika ofisi za kamati hiyo, Novemba 6, mwaka huu, saa 9:25
mchana, Sitti alisema ameamua kwa hiyari yake kuvua taji hilo baada ya
kusakamwa na vyombo vya habari kwamba alichakachua umri.
“Leo
nalivua taji rasmi nililopewa na binadamu lakini alilonipa mwenyezi
Mungu bado ninalo. Mwisho naomba radhi Watanzania wote kwa uamuzi huo
niliochukua,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo ya Sitti.
Nafasi ya Sitti imetwaliwa na mshindi wa pili, Lilian Kamazima aliyetokea Arusha.
Hata
hivyo, kuna ushahidi wa kutosha kutoka Rita na Idara ya Uhamiaji kwamba,
umri wa miaka 25 uliopo kwenye paspoti ya kusafiria ya Sitti ambayo
imesambaa kwenye mitandao ya kijamii ndiyo sahihi!
Kwa maana hiyo,
Sitti kujivua taji anakuwa amemalizana na kesi ya wananchi waliokuwa
wakimkomalia, lakini kesi ya kughushi cheti cha kuzaliwa bado inamhusu
kwa sababu kwa sheria za Tanzania, mtu akithibitika kudanganya umri
kifungo chake ni miaka 3 jela na jamhuri inaweza kumshtaki kwa kusimamia
kesi yenyewe.
Miss Lillian Kamazima akipozi.
NI HISTORIA KWA MISS TANZANIA
Hii
ni mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya Miss Tanzania
yaliyoanza nchini mwaka 1994 baada ya kufutwa awali ambapo mshindi wa
kwanza anajivua taji ingawa pia haikuwahi kutokea mshiriki kuvuliwa taji
kwa kosa lolote lile.
ILIWAHI KUTOKEA MISS KUDANGAYA SHULE
Mwaka
1995, Miss Tanzania alikuwa ni Emily Adolf, mwanafunzi wa kidato cha
pili Shule ya Sekondari ya Central, Dodoma. Ushindi wake ulileta
malumbano baada ya kubainika alishiriki akiwa mwanafunzi huku akidai
alimaliza. Alifukuzwa shule lakini hakuvuliwa taji.
WEMA ALINUSURIKA NA UMRI
Mwaka
2006, Miss Tanzania, Wema Isaac Sepetu naye alinusurika kuvuliwa taji
kwa madai kwamba alidanganya umri wake. Wema alidaiwa kushiriki
mashindano hayo akiwa na miaka 17, yeye akadai ana 18 lakini vuguvugu la
wananchi kumkomalia miaka hiyo haikuwa kama sasa.