TAARIFA YA WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA TOKA WAJUMBE 201 KUHUSU MWENENDO WA SHUGHULI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Sisi
Wawakilishi wa Jumuiya na Taasisi za Dini, tuliopendekezwa na Taasisi
zetu na baadaye kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
baada ya kushauriana na Rais wa Zanzibar kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la
Katiba, na kula kiapo cha utekelezaji wa jukumu hili kubwa.
Tukiamini
kuandaa Katiba Mpya kwa maridhiano ya Kitaifa kwa wananchi wote,
tulipokea jukumu hili kama wajibu wetu Kitaifa. Aidha tunaamini kwamba
katika kupata maridhiano ya Kitaifa ni muhimu kuheshimu kila wazo na
fikra inayotolewa na kuunganisha fikra hizo kwa usahihi, kwa njia ya
kidemokrasia kwa kupiga kura na kukubaliana na matokeo ya wengi.
Kama
ilivyoelezwa hapo awali, kabla ya kuanza shughuli za Bunge Maalum, kila
mjumbe alikula kiapo cha kuwa mwaminifu na mtiifu kwa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kwa kadiri ya uwezo wake na ufahamu wake,
kufanya kazi zinazomhusu, bila upendeleo na kumuomba Mwenyezi Mungu
amsaidie.
Tumeshangazwa
na kusikitishwa sana kuona kwamba mchakato wa kutayarisha Katiba
itakayopendekezwa na Bunge hili kwa wananchi, unachafuliwa taswira
yake. Bunge Maalum la Katiba linachafuliwa na, shughuli zake kuingiliwa
na kupotoshwa na wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge, Makundi, Taasisi
na Vyombo mbali mbali vya habari, uhalali na ukweli wa shughuli za
BungeMaalum la Katiba unapotoshwa. Wananchi wanaaminishwa yasiyo na
ukweli.
Upotoshwaji huu umezua mijadala mbali mbali katika jamii ya Watanzania na bado linaendelezwa kama ifuatavyo:
1. Kwamba
Bunge Maalum la Katiba halina uhalali kwa kuwa hao wajumbe wenzetu
walioondoka wameliondolea uhalali wake kwa vile hwapo, wakiwepo Bungeni
basi uhalalai wake utakuwepo - utapatikana;
2. Inadaiwa kwamba Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zinavunjwa ovyo ovyo;
3. Inadaiwa
pia, kwamba kinachojadiliwa sasa katika Bunge hili ni Waraka mwingine
na si Rasimu iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
iliyowasilishwa rasmi Bungeni na kuanza kujadiliwa na wajumbe;
4. Inadaiwa
na watu na Taasisi mbali mbali, kwamba viongozi wa dini, wajumbe wa
Bunge Maalum la Katiba, na wajumbe wa Kundi la 201, wanapewa rushwa.
Isitoshe Vyombo vya habari vimeandika tuhuma kama hizi.
5. Inadaiwa pia kwamba wajumbe waliomo katika Bunge hili ni wachache, ukilinganisha na hao walioko nje ya Bunge hilo;
6. Bunge hili, kwa tuhuma hizo, lazima lisitishwe au livunjwe na Mhe. Rais.
Kabla
ya kuanza kuusahihisha upotoshwaji huo, sisi Wawakilishi wa Taasisi za
Dini mbali mbali na Wajumbe wa Kundi la 201 katika Bunge Maalum la
Katiba, tunapenda kufahamisha umma wa Tanzania mchakato wa kutayarisha
Katiba Mpya ulivyo kisheria.
Tunapenda
kuwafahamisha Watanzania wenzetu kwamba mchakato huu una hatua tatu kwa
mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mpaka hivi sasa ni hatua
moja imekamilika. Hatua ya pili ndiyo inayoendelea, na hatua ya tatu
bado haijaanza.
Hatua
ya kwanza ni ile ya uandaaji wa Rasimu. Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Sura ya 83 iliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya kifungu cha
tano cha sheria hiyo. Tume hii ilipewa jukumu la kuratibu na kukusanya
maoni ya wananchi juu ya Katiba, kuanisha na kuchambua maoni ya wananchi
na kisha kuandaa rasimu ya Katiba. Kazi hiyo ilifanyika kwa kipindi
cha takriban miaka miwili na hatimaye Rasimu ya Katiba ilikamilika.
Hatua
ya pili ilikuwa ni kuipeleka Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalum la
Katiba, ambalo liliundwa kwa shughuli maalum ya kuandika Katiba
inayopendekezwa, ili ifikishwe kwa wananchi ambao wataamua waikubali au
waikatae kwa kuwa wao ndio wenye maamuzi ya mwisho. Hawa ni Watanzania
wote wenye uwezo wa kupiga kura kwa kutoa maoni yao. Hoja ya Mamlaka ya
Bunge hili hatujazungumzia kwa vile imefikishwa Mahakama Kuu ya
Tanzania ili kupata tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge hili.
Tunachoweza kusema ni kwamba jukumu kuu la Bunge hili ni kutengeneza
Katiba inayopendekezwa na Bunge ili ifikishwe kwa wananchi waipigie
kura ya maoni. Hatua hii ya pili bado inaendelea.
Hatua
ya tatu ni pale Bunge Maalum la Katiba tutamkabidhi Mhe. Rais Katiba
inayopendekezwa ambayo itafikishwa kwa wananchi ili waikubali kama
wataridhika nayo au kuikataa kama haikidhi matarajio yao.
Hatua hii ni ya mwisho wananchi wakiikubali tunapata Katiba Mpya wakiikataa, tunaendelea na Katiba tuliyonayo.
Kilichotokea
ni kwamba, wajumbe wenzetu walio nje ya Bunge hili wameamua kuukiuka
utaratibu uliowekwa kisheria. Badala yake wamepeleka Rasimu ya Katiba
kwa wananchi wakati mchakato wa kutayarisha Katiba inayopendekezwa bado
haujakamilika.
Sisi
Wawakilishi wa Taasisi za Dini, ambao kuuhubiri, kuutangaza na
kuusimamia ukweli ni moja ya majukumu yetu katika jamii, tumesikitishwa
sana na taarifa potofu zinazosambazwa kwa makusudi na makundi, taasisi
na vyombo vya habari mbali mbali na tukiwa wajumbe wa Bunge hili ambao
tunafahamu kwa kina na tunaridhika na kila hatua ya mchakato huu. Tuna
wajibu wa kusahihisha upotofu huu, unaoendeshwa kwa makusudi na hivi
kuwaeleza Watanzania ukweli na hali halisi inayojiri hapa Bungeni.
Watanzania msifadhaishwe na wala msibabaishwe. Hali ni shwari.
Mchakato unaendelea kwa amani na utulivu.
Katika
kusahihisha upotofu unaozungumzwa kupitia mijadala na midahalo mbali
mbali katika jamii, tunaomba kufafanua hali ilivyo kama ifuatavyo:-
TUHUMA KWAMBA BUNGE MAALUM LA KATIBA KUKOSA UHALALI
Jambo
hili si kweli hata kidogo kwani kuna wajumbe wa aina tatu Bungeni ambao
wamewekwa na kutambuliwa kisheria. Hawa ni kama wafuatao:
1. Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
3. Wajumbe 201 walioteuliwa na Mhe. Rais, baada ya kupendekezwa na Taasisi, Mashirika na makundi mbali mbali nchini,
Uhalali
wa Bunge unakuwapo wakati wajumbe kutoka makundi hayo matatu wapo
Bungeni, na si Vyama vya Siasa pekee. Iwapo kwa mfano wajumbe wa 201
wakiamua kutoshiriki katika shughuli za Bunge, basi sehemu moja muhimu
ya Bunge haitakuwapo na uhalali wa Bunge hautakuwepo.
Hata
hivyo, Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zimeweka idadi ya akidi ambayo
ni nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum. Akidi hii ikifikiwa Bunge
huendelea na shughuli zake. Akidi hii hufikiwa kila wakati BungeMaalum
linapokutana. Hii inamaanisha kwamba Bunge Maalum la Katiba linaendesha
shughuli zake kwa misingi ya sheria na taratibu zilizojiwekea. Bunge
lina uhalali wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
TUHUMA KWAMBA KANUNI ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA ZINAVUNJWA
Suala
hilo halijawahi kutokea. Kanuni za Bunge Maalum la Katiba zilipitishwa
na wajumbe wote kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sheria
Namba 83. Vile vile uendeshaji wote wa shughuli za Bunge zinafanywa kwa
mujibu wa Kanuni za Bunge Maalum. Kanuni hizo zinatoa fursa ya Bunge
Maalum kuzirekebisha pindi inapobainika ipo haja ya kufanya hivyo kwa
mujibu wa kanuni Namba 87.
WARAKA MWINGINE UNAJADILIWA NA SI RASIMU YA TUME
Hili
nalo si kweli. Tunawahakikishia Watanzania wote kwamba sisi kama
Wawakilishi wa Taasisi za Dini miongoni mwa wajumbe wa Kundi la 201, kwa
ujumla tunasema hii si kweli. Ni upotoshaji wa makusudi. Tunaijadili
Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ibara kwa ibara. Ibara nyingi
zimeachwa kama zilivyo. Kuna ibara ambazo zimeboreshwa au kurekebishwa,
kuna ambazo zimeondolewa na kuna nyingine mpya ambazo zimewekwa ili
kuweka mambo ya msingi ambayo Rasimu haikuyazingatia au haikuyaona.
WAWAKILISHI WA TAASISI ZA DINI, WAJUMBE WA KUNDI LA 201 WA BUNGE LA KATIBA KUPEWA AU KUPOKEA RUSHWA
Sisi
Wawakilishi wa Taasisi za Dini na Wajumbe wa Kundi la 201 wa Bunge hili
tumesikitishwa sana na taarifa hii iliyosambazwa na baadhi ya watu, na
kukaririwa na baadhi ya vyombo vya habari aidha kupitia kwenye mijadala,
midahalo na makongamano mbali mbali. Baadhi yetu sisi Viongozi wa
Kiroho tumeapishwa viapo vya uadilifu katika uongozi wetu wa kiroho na
tuko mstari wa mbele kuongoza waumini wetu kuepuka dhambi ya tamaa ya
fedha, na kusema uongo. Taarifa kama hizo hazionyeshi heshima kwa dini
au nafasi zetu za kipekee katika uongozi wa kiroho. Taarifa hizi
zinatangazwa kwa makusudi na watu mbali mbali kupita vyombo vya habari
kwa malengo ya kisiasa na kutudhalilisha sisi Viongozi wa kiroho mbele
ya umma. Tunaomba tabia hii ikomeshwe.
TUHUMA KWAMBA BUNGE KUWA NA WAJUMBE WACHACHE
Hili nalo si kweli. Wajumbe wanaohudhuria Bunge wanakidhi akidi inayohitajika kwa mujibu wa kanuni.
HOJA YA KUSITISHWA AU KUVUNJWA KWA BUNGE MAALUM
Hii
ni hoja inayozungumzwa katika mijadala mbali mbali katika jamii.
Msingi wa hoja hiyo ni kutokuueleza umma ukweli ulioko Bungeni kwa
kupeleka taarifa potofu kwa wananchi kwamba Bunge Maalum limekosa
mwelekeo. Hatuoni sababu za hoja hii kutiliwa maanani kwa kuwa hakuna
sababu za msingi na za kisheria za kufanya hivyo.
HITIMISHO
Kumekuwa
na taarifa mbali mbali zenye malengo ya ama kuingilia shughuli za Bunge
hili au kutudhalilisha sisi wajumbe ambao si Wabunge au Wawakilishi.
Wajumbe 201, ambao mchango wao katika mijadala ya Kamati mbali mbali
umekuwa na uzito wa pekee, hautambuliki katika taarifa hizo ambazo
zimejaa malengo ya kisiasa zaidi kuliko ukamilishaji wa shughuli za
Bunge Maalum.
Kuna
taarifa nyingine zimesambazwa zikiwa na upotoshaji mkubwa, licha ya
kwamba Taasisi zinazosambaza taarifa hizo zina wajumbe wake katika Bunge
Maalum. Wajumbe hao wangeweza kuzielimisha Taasisi zao ukweli ulipo
hapa Bungeni, na hivyo kuwafikishia wasomaji wao taarifa zilizo za kweli
na ili kulijengea Bunge hili heshima machoni pa umma wa Tanzania na
Kimataifa. Udhalilishaji kama huu unatuumiza hata sisi wajumbe ambao
kwa hiari yetu tuliamua kubaki Bungeni na kuyatimiza hayo ambayo
tulitumwa tuje tuyakamilishe.
Kama
tulivyosema hapo awali ni wajibu wetu kama Viongozi wa Dini na Wajumbe
wa Bunge hili kuutaarifu umma hali halisi katika shughuli za Bunge
Maalum na kuwasihi wapotoshaji kwamba wauheshimu ukweli na wawaheshimu
watanzania kwa kuwaeleza ukweli.
Ahsanteni sana.
……………………. …………………………
SHEIKH HAMID MASOUD JONGO ASKOFU AMOS JOSEPH MUHAGACHI
BAKWATA KIKRISTO
No comments:
Post a Comment