Na Saleh Ally
WAKATI
mwingine nimekuwa najiuliza mambo maswali mengi sana kuhusiana na suala
la ubaguzi wa rangi ambalo linaonekana wakati mwingine kulielemea
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Nianze
na mkasa wa juzi ambao umemtokea kiungo nyota wa Brazil, Ronaldinho
Gaucho ambaye hivi karibuni amejiunga na klabu ya Querétaro ya nchini
Mexico ambako anaamini ndiyo atamalizia mpira wake.
Ronaldinho amebaguliwa, amedharauliwa na kuitwa sokwe, licha ya kwamba hakuwa na kosa hata punde.
Aliyembagua
ni mwanasiasa maarufu wa chama kinachojulikana kama National Action
Party (Pan) ambaye pia amewahi kuwa waziri wa serikari ya Mexico.
Jamaa anaitwa Carlos Manuel Treviño ambaye ameingia kwenye kundi la wapuuzi na wajinga wanaoamini ubaguzi wa rangi ni nyenzo.
Kisa
cha kumbagua Ronaldinho ni kwa kuwa mwanasiasa huyo alikuwa akitokea
katika mihangaiko yake anarejea nyumbani, kukawa na foleni kubwa sana
njiani na mwisho aligundua inatokana na mashabiki wa klabu ya Queretaro
waliokuwa wakitokea kwenye Uwanja wa Corregidora kumpokea kiungo huyo
alipokuwa anatambulishwa.
Akaamua
kuweka maneno ya kashfa kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook akimuita
sokwe ambaye amesababisha yeye kuchelewa kufika nyumbani.
Mpira
ni burudani kubwa lakini ni chombo bora kabisa cha kuwaunganisha watu
mbalimbali wakiwemo wale waliogombana, wasiopendana au kutoelewana.
Nchi
nyingi zilizoingia kwenye vita hasa vile vya wenyewe kwa wenyewe,
mwisho zimetumia nguvu zaidi kwenye mchezo wa soka ili kurejesha hali ya
utulivu.
Mfano
mzuri ni Wanyarwanda ambao baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994, soka
ndiyo chombo kilichosaidia kwa asilimia kubwa kuwaunganisha, pia
kujitahidi kusahau mabaya na makali yaliyopita.
Sasa
jiulize, wakati wengine wanatumia soka kama chombo unganishi, vipi hao
wanatumia mchezo huo kama chombo tenganishi kwa lengo la kudharau,
kuonea au kubeza bila hata sababu yoyote ya msingi.
Ninazungumzia
Wazungu, ninazungumzia watu weupe wanaoamini ni bora kuliko Weusi hata
kama heshima yao haiko juu kama wanavyofikiri.
Wakati
mwingine unaweza kufikiri hata wao Fifa ni wababaishaji kwenye hili kwa
kuwa hakuna adhabu kali zaidi kwa wanaofanya hivyo viwanjani.
Kuna
kila sababu ya kuliangalia zaidi kwa kuwa wale wanaowabagua weusi,
wanakuwa hawana heshima ya kimatendo au hata fedha dhidi yao.
Angalia
waliombagua Samuel Eto’o au Yaya Toure kule Urusi. Mfano mwingine wale
mashabiki ambao huwabagua wachezaji Waingereza au kule Hispania.
Ajabu hili linafanywa hata na wachezaji kwa wachezaji, nafikiri ndiyo ungekuwa mfano mzuri zaidi kuwaonya wabaguzi wengine.
Ikitokea mchezaji kambagua mwenzake, halafu ushahidi ukawa umepatikana kwa uhakika, basi afungiwe msimu mzima.
Wale
mashabiki wanaweza kujifunza kupitia adhabu kali ambazo watapata
wachezaji, makocha, viongozi na hata waamuzi ambao wataonyesha ubaguzi.
Nani kasema ngozi nyeupe au ngozi ya mzungu ndiyo akili? Upuuzi mtupu!
Tunajua
Fifa ina Wazungu wengi kuliko Weusi, huenda linaonekana si suala kubwa
sana na mapambano yake yako kwenye mapango tu bila ya vitendo.
Huenda
adhabu ingekuwa kali sana kama Waafrika wangekuwa na nafasi ya
kuwabagua Wazungu pia. Fifa bado inahusika na inapaswa kujua upole wake
katika hilo, unazidi kufanya liendelee.
Wazungu
wanaobagua Weusi ni wapuuzi, Fifa haipaswi kuacha upuuzi huo uendelee
kwa kuwa si Weupe tu ndiyo wanaoujua kuucheza mpira na mfano mzuri wa
kuwa Weusi wanaujua mpira, jikumbushe kwa Pele.
Wajinga
kama mwanasiasa yule wa Mexico aliyembagua Ronaldinho ambaye sasa
tayari yuko katika hali mbaya kisiasa kutokana na kusakamwa sana na
mashabiki wa soka, wanapaswa wapate joto ya jiwe kama anayokutana nayo,
la sivyo hawataacha.
Lakini
kwa Fifa na mashirikisho ya soka Ulaya, nayo yapambane kuzuia hilo kwa
kuwa inakuwa ajabu, hata Wazungu wenye njaa, nao wanawadharau Waafrika
wenye mafanikio zaidi eti kisa ni Weupe. Huu ni upuuzi mkubwa.
No comments:
Post a Comment