Ghati
Bunyige akiwa amekaa kwenye benchi akisubiri huduma ya matibabu katika
kituo cha afya cha Sirari wilayani Tarime mkoani Mara.
UKISTAAJABU ya Musa utayaona ya Firauni! Mwanamke mmoja, mkazi wa
Kitongoji cha Buriba, Kijiji cha Sirari wilayani Tarime, Mara aitwaye
Bunyige Chacha (25) amepigwa mshale kwenye makalio na mumewe, Ghati
Nyamarandi kisa kikidaiwa kuanzia kwenye pesa ya mahari na
watoto. Akisimulia mkasa wake mzito uliompata Oktoba 5, mwaka huu majira
ya jioni, mwanamke huyo alisema siku hiyo, mumewe alirudi na kumuuliza
walipo watoto wao wawili (hakuwataja majina) ambao aliwaondoa nyumbani
siku kadhaa nyuma bila kumwambia.
Akasema, alipomuuliza hivyo tu, ndipo mumewe akamjia juu na
kumshambulia kwa matusi huku akisema watoto aliwapeleka kuuzwa eneo
linaloitwa Nyumba Ntobu. “Mume wangu alifika nyumbani, nilipomuuliza
watoto wako wapi ndipo akanifungia ndani ya chumba na kunishambulia kwa
matusi.
“Kwa bahati nzuri nilibahatika kutoroka na kukimbilia kwa majirani
lakini wakati nikivuka uzio wa mlango nilianguka, akapata nafasi,
akanirushia mshale ulionichoma sehemu ya makalio, chini ya mguu wa
kulia,”alisema mwanamke huyo.
Ghati Bunyige akiongea na mwandishi wa habari kuhusiana na mkasa aliokumbana nao.
Mama huyo aliongeza kuwa, watoto wake wawili waliuzwa Nyumba Ntobu na
baba huyo kuchukua mahari bila kumshirikisha mke suala ambalo lilizua
mtafaruku ndani ya nyumba mwanamke akidai watoto wake kila siku.
“Kwanza mume wangu alimwachisha masomo binti yetu wa kwanza ambaye
alikuwa akisoma darasa la tatu katika Shule ya Msingi Sirari, akamuoza
Nyumba Ntobu na kupokea mahari yeye.
“Baadaye akamwachisha masomo binti yetu wa pili aliyekuwa akisoma
darasa la pili katika Shule ya Msingi Nyamaraga, nchi jirani ya Kenya,
akamwozesha hukohuko Nyumba Ntobu na akapokea mahari peke yake.“Baadaye
nilikuja kugundua kuwa, alikuwa akipokea mahari kwa siri kwa sababu
alitaka kulipia mahari ili na yeye aoe mke wa pili ambaye anaishi naye
tayari, lakini ni mke wa mtu,” alisema mwanamke huyo.
Picha ya mama huyo akiwa katika usafiri akipelekwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Hivi karibuni, Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (Tamwa) kupitia
kwa mkurugenzi wake mtendaji, Valarie Msoka alifika kumwona mwanamke
huyo na kumpa pole kwa tukio lililompata. Alimtaka mama huyo kumshitaki
mumewe ili akamatwe na sheria ichukue mkondo wake.
Msoka amekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki ya mama na mtoto
na kulaani vitendo vinavyofanywa na jamii vya ukatili wa kijinsia kwa
madai kuwa nimila au desturi za makabila husika.
Kwa upande wake, mwanasheria msaidizi wa Kata ya Sirari, Zablani
Zablani aliliambia gazeti hili kuwa, mwanamke huyo alifika ofisini kwake
kuomba msaada wa kisheria baada ya kujeruhiwa kwa mshale na mumewe
ambapo yeye alimpeleka Kituo cha Polisi cha Sirari ili kupata PF3 na
kwenda kupata matibabu katika Zahanati ya Alpha iliyopo mji mdogo wa
Sirari.
No comments:
Post a Comment