Thursday, August 7, 2014
KWA MTINDO HUU UJUE WATU WAMECHOSHWA
Gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T.589 AZS likiwa limebeba magunia ya madawa ya kulevya aina ya bhangi mara baada ya kukamatwa eneo la Sanawari jijini Arusha na askari wa kitengo cha kuzuia Madawa ya Kulevya mkoani hapa.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha.
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha limewakamata watu watano wakiwa na magunia saba ya madawa ya kulevya aina ya bhangi wakiwemo mke na mume.
Awali askari wa Kitengo cha Kuzuia Madawa ya Kulevya Mkoani hapa wakiwa doria walipata taarifa toka kwa raia wema iliyoeleza kuwepo kwa watu wanaosafirisha madawa hayo.
Mara baada ya kupata taarifa hiyo askari hao waliweka mtego maeneo ya Sanawari ambapo muda wa saa 3:30 usiku walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Hussein Rashid (35) mkazi wa Sakina, dereva pamoja na mwenzake Sebastian Wilbert (37) Fundi magari, mkazi wa Ilboru wakiwa wanasafirisha magunia matano ya madawa ya kulevya aina ya bhangi yenye uzito wa kilogramu 171 kuelekea nchi jirani ya Kenya kwa kutumia gari aina ya Toyota Corolla lenye namba za usajili T. 589 AZS.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas alisema kwamba, mara baada ya watuhumiwa hao kuhojiwa walikiri kosa hilo na kumtaja mwanamke aitwaye Flora John (38) Mkazi wa Ekenywa- Ngaramtoni kuwa ndio aliyewauzia.
Kamanda Sabas aliendelea kwa kusema kwamba, askari hao walianza kumfutilia mwanamke huyo ambapo jana Jumanne tarehe 05.08.2014 walikwenda nyumbani kwake na kumkuta mtuhumiwa ambaye ni muuzaji akiwa na mume wake aitwaye John Meleji (45) Mkazi wa Ekenywa na mara baada ya kufanya upekuzi walikuta gunia moja la madawa ya kulevya aina bhangi ndani ya nyumba hiyo.
Mbali na kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni mke na mume pia askari hao walimkamata jirani yao aitwaye Loseriani Metelami (21) Mkulima mkazi wa Ekenywa baada ya yeye pia kukutwa na gunia moja la madawa ya kulevya aina ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia yaliyokamatwa kuwa saba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment