Monday, August 18, 2014
UKAWA WAMTESA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, AWABEMBELEZA KURUDI BUNGENI DODOMA.
Mwanasheria Mkuu akizungumza wakati wa mkutano na waandishi jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao.
Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema amesema mchakato wa Katiba Mpya ukikwama kufika mwisho kutokana na mvutano unaoendelea wa makundi mawili kushikilia misimamo yao, kutafanyika marekebisho ya 15 katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 ili kuruhusu kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Pia, ameipongeza iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuandaa Rasimu bora na kuwaomba wajumbe wake kuwa na ngozi ngumu ya uvumilivu katika kipindi hiki na waepuke kurushiana maneno na watu wanaowakejeli.
Jaji Werema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuelezea mchakato huo ulipotoka, ulipofika na unakokwenda huku akitumia Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Rasimu ya Katiba kufafanua baadhi ya mambo.
Mwanasheria huyo, akijibu swali aliloulizwa kuwa Bunge Maalumu la Katiba linaendelea wakati wajumbe kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiwa hawashiriki, Je, ikishindikana kupatikana kwa theluthi mbili itakuaje? Alisema: “Katika kamati theluthi mbili inatosha, lakini kule mwisho (katika kura ya maoni ya kuipitisha Katiba itakayopendekezwa) kama tutafika darajani, hilo ni suala la siku za usoni.
“Kama tutafika huko na kukuta hakuna pa kutokea, tutarudi bungeni (Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na kufanya marekebisho ya 15 katika Katiba ya sasa ya mwaka 1977 kama uwepo wa Tume huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi na kupunguzwa kwa mamlaka ya Rais, vitu ambavyo vimekuwa vikizungumzwa sana na wananchi,” alisema Jaji Werema.
Kuhusu madaraka ya Rais kulivunja au kulisitisha Bunge hilo, Jaji Werema alisema “Sheria haimruhusu Rais kulivunja au kulisitisha na katika maongezi yangu na yeye (Rais Kikwete) nilimweleza kwamba hana madaraka hayo.”
Aliongeza: “Nimemwambia hana mamlaka ya kusimamisha, hana mamlaka ya kulivunja na wala asifikirie kwani Sheria haikumpa mamlaka na akifanya hivyo atakuwa anavunja Katiba.”
Jaji Werema alisema mamlaka ya Bunge hilo inatokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inayolitaka kujadili na kupitisha Rasimu iliyopendekezwa na Tume kisha kuandaa Katiba na kuipeleka kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.
“Kisheria maana ya kujadili ni kuboresha, kubadilisha na kuweka jambo vizuri na hii siyo mimi bali tulikubaliana wote na kanuni zikaandaliwa,” alisema Jaji Werema.
Kuhusu mabadiliko ya kanuni ilizozifanya Bunge hilo wakati Ukawa wakiwa hawapo alisema: “Tulifanya hivyo kwani Rais (Kikwete) amesema siku 60 alizoongeza zikiisha hawezi kuongeza tena, hivyo tumefanya hivyo ili kuwezesha siku hizo zitoshe.”
Aprili 16 mwaka huu, wajumbe wa Ukawa kutoka vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201 walisusia kushiriki shughuli zote za Bunge hilo hadi pale Rasimu iliyowasilishwa na Jaji Warioba iheshimiwe kutokana na kubeba maoni na mapendekezo ya wananchi.
Hata hivyo, Bunge hilo liliendelea na vikao vyake hadi lilipoahirishwa Aprili mwaka huu kupisha Bunge la Bajeti na Agosti 5 mwaka huu. Lilirejea tena na kuanza vikao vyake huku wajumbe wa Ukawa wakiwa wameendelea kushikilia msimamo wao.
Mvutano mkubwa wa Ukawa na Tanzania kwanza (wajumbe kutoka CCM) ulianza wakati Kamati 12 za Bunge hilo zilipokuwa zikiwasilisha maoni ya Sura ya Kwanza na ya Sita inayohusu muundo wa muungano kuwa wa Serikali tatu kama ulivyo katika Rasimu hiyo, huku CCM wakitaka Serikali mbili.
Jitihada zimefanyika za kutafuta maridhiano baina ya makundi hayo, Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samwel Sitta aliteua kamati ya mashauriano, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi aliwakutanisha Ukawa na Tanzania Kwanza na wanaharakati kadhaa kuandaa meza ya mashauriano kwa kumwita Mkurugenzi wa Shule ya Sheria Kenya, Profesa Patrick Lumumba lakini jitihada hizo zimegonga mwamba.
Jaji Werema akizungumzia maridhiano alisema: “Huwezi kupata maridhiano wakati kila upande unashikilia msimamo wake hivyo kinachotakiwa tuijadili Rasimu hii na wananchi ndiyo wataamua ni serikali mbili au tatu na tusiwabeze kwani wao ndiyo wenye uamuzi wa mwisho.
Akiizungumzia iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema, “Hawa wazee walifanya kazi nzuri sana jambo hili linachukua hisia sana, hivi sasa wanajibishana. Mimi nawaomba wawe wasuluhishi kwani baadhi walikataa na mimi niliwashauri wakakubali na leo yanayowatokea ndiyo hayo waliyoyakataa.”
Aliongeza: “Wavumilie, haya mambo ya umma ni lazima uwe na ngozi ngumu na kama unajibu jibu kidogo tu.”
Mwanasheria huyo aliyebobea katika masuala ya usuluhishi wa migogoro aliwaomba wajumbe wa Ukawa kurejea bungeni kujadili sura zilizosalia ambazo zinagusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment