Monday, September 1, 2014

MFANYABIASHARA AMCHARANGA MAPANGA ALBINO MOROGORO!


Mlemavu wa ngozi Damas Valeniani aliyecharangwa mapanga na mfanyabiashara maarufu mkoani Morogoro anayefahamika kwa jina moja la Lyimo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro likimshikilia mkazi wa wilayani Mvomero, Johnson Damian Mkude kwa msala wa kumchinja mdogo wake na kupeleka kichwa kwa mganga wa kienyeji ili awe bilionea, jeshi hilo linamshikilia mfanyabiashara mwingine maarufu mkoani hapa aitwaye Lyimo kwa tuhuma za kumcharanga mapanga Damas Valeniani (36) ambaye ni  mlemavu wa ngozi (albino). Jamaa huyo maarufu kwa jina la Mangi, anadaiwa kutenda unyama huo wiki iliyopita usiku wa manane kwenye Msitu wa Milima ya Uluguru, Mtaa wa Bingwa Kiwasi Juu, Kilakala, wakati mlemavu huyo, akiwa amelala. 
“Nilikuwa nimelala, ghafla nikasikia mtu akiingia akiwa ameshika panga na kuanza kunikatakata huku akitaka kuninyofoa masikio yangu. Nilimtambua kuwa ni Lyimo ambaye ni jirani yetu.”

Eneo la tukio ambalo Bw. Damas Valeniani alishambuliwa kwa mapanga.

 Alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo, alijitetea vya kutosha na kufanikiwa kuchomoka, kwa bahati nzuri mpwa wake, Mathias John alitokea na kumsaidiahuku wakipiga kelele za kuomba msaada lakini tayari alikuwa amshamcharanga panga kichwani na kusababisha atokwe na damu nyingi.

Alisema kuwa kutokana na woga alioupata, aliogopa kulala hivyo alikimbilia kwa mjumbe wa mtaa wao, Filemon Gyuna ambako alipatiwa huduma ya kwanza.

Dada wa Damas Valeniani.


 “Kulipokucha ndipo tukaenda kuripoti polisi na kupewa jalada la kesi namba MOR/RB/5122/2014-SHAMBULIZI.
“Polisi walifika nyumbani na kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha kwenye mkono wa sheria na mimi nikapewa PF-3 kwa ajili ya matibabu kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro,” alisema Damas kwa maumivu makali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, SAC Leonard Paul akifafanua jambo.

 Akihojiwa na mwandishi wetu juu ya tukio hilo, mwenyekiti wa mtaa huo, Ally Malekela alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba Lyimo alipewa saa 24 za kuhama kwenye mtaa huo.
 Wananchi mbalimbali waliozungumza na Ijumaa Wikienda, walisema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, SAC Leonard Paul, anatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kukabiliana na matukio kama hayo.Kwa upande wake, mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Mkoa wa Morogoro, David Mganga alisema: “Natoa wito kwa jamii ielewe kuwa kiungo cha albino hakiwezi kumpa mtu utajiri au mafanikio, waache kututesa sisi maalbino.”

No comments:

Post a Comment