
· Ni kweli ngazi ya vyama tawala na mikutano ya upatanishi
kufanyika Arusha.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ametangaza kuwa Tanzania imekubali kuwa msuluhishi wa mgogoro wa kisiasa
ndani ya chama tawala cha Sudan Kusini cha Sudanese People’s
Liberation Movement (SPLM), mgogoro ambao umesababisha kuzuka kwa vita
ya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Hata
hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa usuluhishi huo utakuwa wa kichama na
Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho kitaongoza usuluhishi huo katika
mazungumzo yatakayofanyika Arusha na kuwa jitihada hizo za Tanzania
hazitaingilia mazungumzo ya kujaribu kusimamisha mapigano nchini humo
yanayoendelea huko Addis Ababa, Ethiopia.
Rais
Kikwete amesema kuwa ulikuwa uongozi wa SPLM na hasa Mwenyekiti wa Chama
hicho, Rais Salva Kiir ambao wameiomba Tanzania kusaidia jitihada za
kisiasa za kupatanisha pande ambazo zinavutana na kutofautiana ndani ya
SPLM wakiamini kuwa mapatano ndani ya chama yatafanikisha kumaliza
mgogoro wa kisiasa katika Serikali ya nchi hiyo ambayo imegawanyika na
kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Rais
Kikwete ametangaza jitihada hizo za upatanishi za Tanzania wakati
alipohutubia maelfu kwa maelfu ya wananchi na kupitia kwao Taifa kwenye
Sherehe ya Kuzima Mwenge wa Uhuru, Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na
Kilele cha Wiki ya Vijana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini
Tabora.
Rais
Kikwete amewaambia wananchi kuwa Tanzania imekubali kuwasaidia ndugu zao
wa Sudan Kusini kwa nia ya kutimiza wajibu wake wa kimataifa na kwa
kuongozwa na kaulimbiu ya Oktoba Mwaka 1959 ambayo Baba wa Taifa,
Mwalimu Nyerere, aliitoa wakati nchi ya Tanganyika bado ikidai uhuru
wake kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza.
Rais
Kikwete ameikariri kaulimbiu hiyo maarufu: “Sisi Watu wa Tanganyika
tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike hata
nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambako hakuna matumaini, upendo
mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau.”
Rais
Kikwete amesema kuwa Mwenge wa Uhuru unabeba falsafa kubwa ndani yake
kuhusu “nchi yetu na uhusiano wake na watu wengine duniani hasa
wanyonge, wenye dhiki na wasiokuwa na amani. Dhamira hii ya Mwalimu na
nchi yetu ilitimizwa Desemba 9, 1961, siku Tanganyika ilipopata Uhuru
ambako Bendera ya Taifa huru la Tanganyika na Mwenge wa Uhuru
vilipandishwa juu ya kilele cha Mlima Kilimanjaro na Mwenge kuwashwa.”
“Toka
wakati huo mpaka sasa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kumulika nchi nzima
ukipita katika mitaa, vijiji, shehia na majimbo, wilaya na mikoa
ukieneza ujumbe wa udugu, umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni
mwa Watanzania.
Kwa
kuzingatia ujumbe uliobebwa na Mwenge wa Uhuru, nchi yetu na sisi
Watanzania tumejitolea kwa hali na mali kusaidia ndugu zetu Barani
Afrika waliokuwa wanatawaliwa kujikomboa kutoka kwenye makucha ya
wakoloni na wabaguzi wa rangi,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni
fahari kwetu kwamba wananchi wa Msumbiji, Zimbabwe, Angola, Namibia na
Afrika Kusini nao wako huru na tumetoa mchango wetu. Ni jambo la faraja
kubwa kwamba nchi yetu imeweza kupatia hifadhi ndugu zetu wa nchi
jirani na hata mbali wakati maisha yao yalipokuwa hatarini kwa sababu ya
kukosekana kwa amani ama kukimbia mateso ya uongozi wa kidikteta. Ndugu
zetu wa Kongo, Burundi, Rwanda, Kenya na Comoro wanaujua ukweli huo.
Na, kwa Uganda tuliwasaidia kuling’oa Dikteta Idd Amin na Comoro
tulisaidia kuunganisha nchi yao tena.”
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment