Mkazi wa Mbagala Zakhiem, Mwanaharusi
Hamis amepoteza kiganja chake cha mkono wa kulia baada ya kulipuliwa na
kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu lililorushwa na polisi wakati wakitawanya
wananchi. Mwanaharusi alilipuliwa na bomu hilo Agosti Mosi 2014,
saa 3:00 usiku alipokuwa anatoka ndani kwenda msalani.Akizungumza na
mwandishi jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wodi ya Mwaisela
namba mbili alikolazwa, alisema tukio hilo limebadilisha kabisa
mustakabali wa maisha yake.Mwanaharusi, ambaye ni mama wa watoto wawili
alisema alikumbwa na madhila hayo wakati polisi walipokwenda mtaani kwao
kumkamata mtuhumiwa wa wizi wa pikipiki.
Alisema walipofika, vijana waliokuwa maeneo hayo waliwarushia polisi
mawe, ndipo polisi walipofyatua mabomu ya machozi na risasi kuwatanya
wananchi hao.
“Ilikuwa saa 3:00 hivi mimi na watoto wangu tukiwa ndani hatujui nini
kinachoendelea nje, ghafla tulianza kusikia milio ya risasi na mvumo wa
kitu kuelekea upande wa ilipo nyumba yetu. Wakati huo nilikuwa natoka
ndani kwenda msalani, nikaona kitu kimenipiga na kunichana sehemu za
mkono na miguuni, baadaye nikagundua kilichonipiga kilikuwa bomu,”alisimulia Mwanaharusi.
Alisema baada ya tukio hilo polisi walimpelekea kituoni kwa ajili ya
kupata fomu namba ya tatu ya matibabu (PF3) na baadaye Hospitali ya
Temeke, alikopewa rufaa ya kwenda Muhimbili kwa kuwa alikuwa akitoka
damu nyingi.
“Nimechanganyikiwa. Mimi ndio mtafutaji wa familia, mwanangu wa kwanza amemaliza kidato cha nne na wa pili ana miaka tisa,” alisema.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Temeke, Kienya Kienya alikiri kutokea kwa
tukio hilo na kusema ufafanuzi utatolewa leo na kamanda wa Kanda ya Dar
es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.
No comments:
Post a Comment