Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/Zanzibar. Katiba
inayopendekezwa itakutana na kihunzi kingine katika utekelezwaji wake
kutokana na Zanzibar kutakiwa kubadili Katiba yake, zikiwamo ibara
zilizobeba msingi wa mabadiliko ya 10 katika Katiba ya Zanzibar.
Mabadiliko
hayo ya mwaka 2010, kwa kiasi kikubwa yanakinzana na Katiba ya sasa ya
Muungano pamoja na Katiba inayopendekezwa ambayo inakabidhiwa leo kwa
Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini
Dodoma.
Ili
Katiba inayopendekezwa iweze kutekelezeka ni lazima Zanzibar ifanyie
mabadiliko Katiba yake kwa kuwa Katiba ya Muungano ndiyo Sheria Kuu.
Hata
hivyo, wachambuzi wanahoji iwapo mabadiliko hayo yatawezekana kirahisi
kwa kuwa yanatakiwa kuidhinishwa kwa kura ya maoni ya wananchi wa
Zanzibar, baada ya kupita kwenye chungu cha Baraza la Wawakilishi na
kuamuliwa kwa theluthi mbili za kura.
Tofauti zilizopo
Mosi,
Katiba ya Zanzibar inatamka kwamba Zanzibar ni nchi ambayo eneo la
mipaka yake ni lote la visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa
vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Ibara ya pili inaitambua Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Masharti
hayo ni kinyume na Katiba inayopendekezwa ambayo katika ibara yake ya
kwanza inatamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi yenye
mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya
Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo kabla ya Hati ya
Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili, 1964 zilikuwa nchi huru.
Pili,
Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 26 inatamka kwamba Rais wa Zanzibar
ni Mkuu wa nchi ya Zanzibar, jambo ambalo ni kinyume na Katiba
inayopendekezwa katika Ibara ya 80 (2) ikisema; Rais wa Jamhuri ya
Muungano atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Amiri Jeshi Mkuu.
Tatu,
Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya pili A inatamka kwamba kwa ajili ya
utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais anaweza kuigawa Zanzibar
katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa
na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.
Masharti
hayo ni kinyume cha Katiba inayopendekezwa Ibara ya 2(2) ambayo
inatamka: “Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa
Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengine, isipokuwa
kwa upande wa Tanzania Zanzibar, Rais atashauriana na Rais wa Zanzibar
kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo
mengine.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment