Mkandarasi
mkuu wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka (BRT), Strabag
International ametangaza mabadiliko ya matumizi katika makutano ya
barabara za Morogoro na Kawawa.
Mabadiliko
hayo yanaanza Jumatatu tarehe 17 hadi tarehe 30 mwezi huu. Akitangaza
mabadiliko hayo leo jijini Dar es Salaam, Afisa uhusiano wa kampuni
hiyo, Bw. Yahya Mkumba alisema mabadiliko hayo yanatokana na matengenezo
yatakayokuwa yanafanyika eneo hilo.
Akielezea
zaidi, alisema magari yatakayokuwa yanaelekea Ubungo kutokea Jangwani
yatalazimika kutumia mchepuko uliopo kabla ya kituo cha Magomeni Mapipa
kwa kuingia barabara ya mabasi yaendayo haraka.
Pia
magari yatakayokuwa yanatokea Ilala Boma kuelekea Morocco, Ubungo na
Jangwani yatalazimika kutumia barabara moja ya upande wa
kushoto. “Wananchi watuvumilie katika kipindi hiki na tunaomba radhi kwa
usumbufu wowote utakaotokea,” alisema.
Mradi
wa BRT unalenga kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es
Salaam.bKilomita 20.9 za mradi huo awamu ya kwanza zipo mbioni
kukamilika na kwa mujibu wa ratiba, zabuni za kupata watoa huduma
zinatarajia kutangazwa mapema mwakani. Mradi huu ni moja ya miradi mikubwa duniani katika mfumo huo ambao unatarajiwa kuwa mfano katika eneo hili la Afrika ya Mashariki na kati.
Katika
siku za hivi karibuni, viongozi na makundi ya watu mbalimbali yameeleza
kuridhishwa kwao na maendeleo ya mradi huo na kutoa mapendekezo ya
kuuboresha zaidi.
No comments:
Post a Comment