Sunday, August 24, 2014

WATUHUMIWA 7 WA MAUAJI YA ALBINO WATIWA MBARONI

JESHI la polisi mkoani Simiyu limefanikiwa kuwakamata watu saba wanaodhaniwa  kuwa wauwaji wa aliyekuwa mlemavu  wa ngozi (albino) Munghu Mugata (40) aliyeuwawa kwa kukatwa mapanga  mnamo mwezi mei  katika  kijiji cha Gasuma kata mwaubingi wilayani  bariadi.

Akiongea na waandishi wa habari ofisi kwake, mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa ambaye pia ni mkuu wa mkoa Paschal Mabiti, alisema kuwa kati ya watuhumiwa hao mmoja ni mganga wa jadi.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Kudawa Yelema (52) ambaye ni mganga wa jadi, Sitta Maduhu (39), Jasamila Sungwa (42), Mpamba Saguda (18), Dede Madono (54), Majeshi Sunja (38), pamoja na Mabula Bindondo (52) wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Gasuma

Alisema kuwa jeshi la polisi kwa kushirikiana na wasamaria wema, liliendesha msako mkubwa wa kuwasaka wahusika wa tukio hilo, ambapo lilifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa hao saba.

Alibainisha kuwa Dede Madono (54) mmoja kati ya watuhumiwa hao, aliugua ugonjwa wa malaria wakati akiwa maabusu na kupelekwa katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi, ambapo alifariki dunia akiwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu.

Mabiti alieleza  jeshi la polisi bado linaendelea kumsaka mdhamini wa mauaji hayo, pamoja na kutafuta sehemu viungo vya mlemavu huyo wapi vilipelekwa ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani na kujibu tuhuma zinazowakabili.

Aidha mkuu huyo wa mkoa alieleza kuwa marehemu Lughata alimwacha mtoto wake Tiri Kulwa (8) darasa la kwanza, ambaye alieleza kuwa kwa sasa mtoto huyo anahudumiwa na halmashauri ya Wilaya ikiwemo kumsomesha.

Hata hivyo mkuu huyo alizitaka  wilaya zote kuhakikisha wanakusanya takwimu sahihi za watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwa pamoja na kutambua mahali wanapoishi.

Alisema mbali na kuagiza kukusanywa kwa takwimu hizo viongozi ngazi ya vijiji na kata wameagizwa kuhakiksha albino wote wanawekewa ulinzi wa kutosha kwa kushirikina na wanachi katika maeneo wanakoishi.

Sambamba na hilo mabiti alitoa onyo kali kwa watu wanatenda matukio hayo na kuwataka kuacha mara moja, huku akieleza kwa atakayebainika kutenda unyama huo utakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Tukio hilo lililotokea mei 12 mwaka huu katika kijiji ca Gasuma kata ya mwaubingi Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, baada ya mlemavu  wa ngozi Mugata kuvamiwa na watu wasiojulikana majira ya saa 8 usiku  akiwa amelala nyumbani kwake.

No comments:

Post a Comment