Sunday, August 17, 2014

TUFAA LATOA AJIRA KWA VIJANA WA MJINI



              








“Asiyefanya kazi na asile” hii ni kauli ya Athumani Idd mfanya biashara wa matunda na mboga mboga Soweto jijini Mbeya. Alitoa kauli hiyo alipotembelewa na mwandishi dukani kwake jijini Mbeya.

 Athumani ni miongoni mwa wafanyabiashara wa maaatunda ya tufaa, embe, zabibu na machungwa na kwa upande wa mboga mboga huuza Uyoga, spinachi cornflower. Biashara hiyo aliibuni baada ya kutafuta ajira kwa mda mrefu bila mafanikio hivyo alianza kujihusisha na kilimo cha mboga mboga na kisha kuanza biashara hiyo aliyo nayo. Alisema “Vijana wengi wa mjini wamekuwa wakilalamikia ugumu wa maisha kutokana na ukosefu wa ajira ambapo imepelekea wengi wao kujihusisha katika vitendo vya uvunjifu wa sheria za nchi. Nimemaliza chuo cha UDSM (University of Dar es salaam) nimesomea mambo ya biashara, lakini sijabahatika kupata ajira hivyo nimeona nijiajiri mwenyewe kwenye kilimo cha mbogamboga na uuzaji wa matunda kitu ambacho sijutii kukifanya na Napata faida kubwa kuliko hata mshahara ambao ningelipwa. Na kati ya matunda yote niyauzayo tufaa linauzika sana kuliko mengine yote.

Mbali na Athumani Idd pia wapo vijana wengi sana ambao wamekuwa wakijishughulisha na biashara ya matunda hayo katika sehemu mbalimbali za nchi yetu haswa mijini. Hapo awali lilionekana ni tuda linaloliwa na watu wenye kipato kikubwa au watu wa mjini peke yao kitu ambaocho kimekuwa tofauti kwa sasa kutokana na uwingi wa matunda hayo na kuuzwa karibu kila mahalli hata barabarani kitu ambacho hapo awali haikuwa hivyo kwani hapo mwanzo tunda hili liliuzwa katika maduka makubwa pekee.

Mbali na biashara ya matunda ambayo imeenea sana sehemu za mijini, tufaa ni Tunda pekee ambalo limeonekana kutoa ajira kwa vijana wengi wanaojishughilisha na biashara hiyo. Na hiyo  ni kutokana na tunda lenyewe kupendwa na watu wengi pia upatikanaji wake hauna msimu maalum.
 
Kwa kuliongelea tunda hili ni tunda moja maarufu duniani ambalo hupendwa kuliwa na watu wote bila kujali lika la mtumiaji, hii inatokana na utamu, ulaini wake pamoja na faida za kiafya zinazopatikana kwa kula matufaa. Na wakati mwingine limekuwa likitumiwa na wapendanao ili kutoa ishara ya upendo baina yao

 Matunda haya hustawi zaidi kwenye nyanda za juu ambako joto sio kali, sehemu kama lushoto, mkoani Tanga, Arusha, miteremko ya Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe, Songea na sehamu nyingine nyingi zenye hali ya hewa zinazofanana na hizo. Udongo unaofaa kwa kilimo cha tufaa ni wenye rutuba ya kutosha na usiotuamisha maji.

Unaweza kupanda kwa kutumia mbegu au kwa kununua miche bora kutoka kwenye taasisiza kilimo mfano Uyole Mbeya kwa wakulima wa nyanda za juu, Tengeru kwa wakazi wa Arusha na SUA kwa wale wa Morogoro nk. kama utatumia mbegu basi ni bora kununua mbegu bora au ukikosa mbegu basi jaribu kutumia zile utakazopata kutoka kwenye tunda lenyewe kwa kufuata kanuni bora za kilimo

Kutokana na hilo ipo haja ya serikali ya nchi yetu kuona kwamba hiyo ni fursa tosha kwa wakulima kupewa mafunzo na kuwawezesha ili kujizatiti katika kilimo cha matunda pendwa kama tufaa ili kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja kama si kwa taifa zima

Kwa sasa matufaa mengi yaonekanayo barabarani huletwa Tanzania yakitokea Afrika ya kusini ambako ndiko mafanikio makubwa yamepatikana kwa kilimo cha matunda barani Afrika. Na kilimo cha tufaa nchini humo limefanikiwa baada ya utafiti wa mbegu bora (hybrid) kufanyika na tufaa ni miongoni mwa tunda ambalo lilifanyiwa utafiti huo na ndipo mafanikio yalipopatikana.

Akiongea kuhusu kuruhusu kuingia kwa matunda hayo meneja wa TFDA mkoani Mbeya Bwana Rodney Alananga, amesema kuwa wao kama TFDA wamechunguza kwa umakini na wamehakikisha kuwa matunda haya yanayotoka Afrika ya kusini hayana madhara kama ambavyo watu wengine wamekuwa wakidhani na kuogopa kula matunda hayo kwa dhana ambayo wengi wao wamekuwa wakisema yanamdhara kwa afya ya binadamu. “sisi kama TFDA huwa tunaruhusu chakula kuingia nchini kama hakina madhara hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kufuata sheria za kibiashara mpakani kama vile kulipia ushuru  na vinginevyo watu wayatumie tuu kwani tunawahakikishia kuwa matufaa hayo hayana madhara ya aina yoyote” alisema meneja Rodney


Kwa upande wa wakulima wao wameiomba serikali kuchukua baadhi ya wakulima wanaotoka katika maeneo yanayolima matufaa na kuwapeleka Afika ya kusini ili kujifunza kwa vitendo jinsi ya ukulima bora wa matunda hayo ili wao pia waje kuwa mfano kwa wakulima wengine ili kuinua kilimo cha matunda hayo Tanzania. “sisi mpaka leo tunalima matufaa yaleyale ya zamani ambayo ukiyapeleka sokoni watu huyaita ya kienyeji  na wengi hawayapendi kwakuwa yana radha ya uchachu tofauti na yale ya kizungu” akimaanisha yale yatokayo Afrika kusini. alisema Yuda Nyamirandu mkulima wa njombe

“Mkulima hashawishiki mpaka ameona kwa macho ama sivyo utatumia nguvu kubwa sana kumshawishi mkulima kuwa mbegu Fulani inafaida na ndio maana wakulima wa mahindi wanawekewa shamba darasa ili waone na hii isiishie kwenye mahindi tuu” alisema Emmanuel Sanga

Akiongea kwa uchungu sana, Bwana Emmanuel alisema anasikitishwa sana na serikali ya Tanzania ambavyo haijaweka kipaumbele kujali kilimo kimatendo huku akitolea mfano jinsi wakulima ambavyo wanapata shida katika miundo mbinu, pamoja na teknolojia duni katika kilimo. “ Ndio maana vijana wanaona hakuna haja ya kujitesa kuingia katika sekta ya kilimo maana ni kazi ya mateso na ndio maana wanakimbilia mijini, lakini serikali ingejali sekta hii hakuna kijana ambaye angekwenda mjini wote tungebakia kwenye kilimo, lakini sasa matokeo yake hiyo kazi wanafanya wazee wasiokuwa na nguvu matokeo yake njaa inaikumba nchi”

Ikiwa kama kuna uwezekano wa vijana kupata elimu katika kilimo na kuwezeshwa kifedha ni hakika ya kwamba kilimo kwanza ikatimia kuliko kuiacha kauli hii ikaendelea kubebwa na wazee peke yao kama ilivyo sasa kwa vijana wengi kukimbilia mijini na kuwaacha wazee wakashughulika na kilimo. Na malengo haya yanaweza timia ikiwa kila mtanzania atasumama katika nafasi yake na kutimiza majukumu yake impasavyo.

Hata hivyo Tanzania bado hatujachelewa kwani taasisi za utafiti zipo na hivyo utafiti ukifanyika Tanzania yaweza kujikuta juu katika ramani ya wakulima bora duniani na kupata faida kubwa kama wazipatazo wenzetu. Kwani mbegu bora ni chanzo cha tija na mapato kwa wakulima na taifa kwa ujumla.

VIAZI LISHE MKOMBOZI WA UMASKINI JIJINI MWANZA


 
Kama ilivyo kawaida ya misemo ya watafiti wengi wasemao mbegu bora ndio tija kwa kilimo bora.  Msemo huu umekuwa ukitimia katika vituo mbalimbali vya utafiti katika kilimo kwa kujizatiti katika tafiti za mbegu bora zenye  manufaa kwa wakulima nchini.
Mkoani Mwanza kituo cha Ukiriguru Agricultural Research Institute kimefanya utafiti na kuja na mbegu mpya ya viazi vitamu vilivyopewa jina la viazi lishe. Mbegu hizi za viazi lishe vililetwa mwaka 2002 kutoka nchini Uganda na shirika la International Potato Centre  na kufanyiwa utafiti na hatimaye sasa kanda ya ziwa wameanza kufaidi matunda yake.
Viazi vitamu ni kati ya mazao makuu ya mizizi yanayozalishwa kwa wingi  na kutumiwa kama  chakula.

Mara zote zao hilo linapewa nafasi kubwa kuzalishwa na wakulima kwa sababu linavumilia ukame na linahesabiwa kuwa ni moja kati ya mazao ya kinga ya njaa kama ilivyo kilimo cha mihogo.
 


Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa viazi vitamu ni Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma japo kuwa viazi vitamu hivi hilimwa karibu katika kila mkoa hapa Tanzania
Katika Mkoa wa Mwanza viazi lishe vimeonekana kuwa mkombozi baada ya TAHEA (Tanzania Home Economics Association) kuingilia kati na kuwasaidia wakulima kutambua umuhimu wa viazi hivyo. Kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti ya Ukiriguru UARI (Ukiriguru Agricultural Research Institute), TAHEA waliamua kutoa mafunzo kwa wakulima ili waweze kujikwamua kimaendeleo na kiuchumi kupitia mbegu mpya za viazi lishe ambazo ni matokeo ya utafiti wa mbegu bora za viazi hivyo uliofanywa na UARI.
Wanawake ndio waliokuwa wakwanza kupata mafunzo hayo baada ya kuonekana wao ndio wakulima wa zao hilo kutokana na zana ya kwamba halina faida kibiashara hivyo kulimwa kwa matumizi ya chakula pekee.
Baada ya utafiti kufanyika na kupatikana aina tano ikiwa ni Ejumla, Karoti Dar, karoti C, Kabode na Jewel za mbegu mpya ambazo zimetofutiana matumizi na ustahimilivu wake, ndipo TAHEA ikawafundisha wanawakea hao kilimo bora, uvunaji bora pamoja na usindikaji ili kupata manufaa zaidi ambayo hapo awali hayakuwepo.
 
Pichani, Unga viazi lishe baada ya kuwekwa kwenye paketi tayari kwa kwenda sokoni 

Ramadhani Bundala ambaye ni afisa kilimo wa TAHEA akifafanua kazi kubwa ambayo wameifanya katika mradi huu wa kuwafundisha wakulima wa viazi kujikwamua kimaisha alisema kuwa“ wanawake wamekuwa wakielemewa sana na kazi za kulea familia huku wakijibakiza nyuma kuwa wao huwa wanalima mazao kwa ajili ya chakula hivyo tukaona ni bora tuwaelekeza wanawake hawa kuwa wanaweza wakalima viazi kama zao la biashara. Tukawaweka katika vikundi na kuwapa mbegu mpya kisha kuwafundisha kuanzia kuandaa shamba mpaka usindikaji. Huwezi amini kwa sasa kilimo hiki cha viazi kimevamiwa na wanaume baada ya kuona mafanikio walioyapata kwenye vikundi hivi.”
Bundala alisema kuwa mbali na kuwa chanzo cha mapato viazi lishe pia vina faida kubwa ikiwamo kuboresha afya hasa za watoto chini ya miaka mitano. Pia viazi lishe vyenye vitamin za aina nyingi ikiwamo vitamin A, vinasaidia watu wenye matatizo ya macho, kuboresha afya za akina mama wajawazito na wanaonyonyesha na kuongeza kinga ya mwili hasa kwa watu wanaoishi na maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa upande wao wakulima, wanakikundi cha Imala buhabi cha jijini mwanza wametoa shukrani zao kwa TAHEA pamoja na Ukiriguru kwa kuwafikisha walipo kwani wanamabadiriko makubwa kimaisha tofauti na hapo awali.

Naye Bi Mwanaidi  mjumbe wa kikundi hicho alisema kuwa japo kuwa yeye ni mjane anayelea familia anauwezo wa kuwapeleka watoto wake shule na kujenga nyumba nzuri ya familia kutokana na viazi lishe anavyolima.
Wakieleza kwa upande wa changamoto wakulima hao walisema kuwa pamoja na mafanikio hayo pia wakulima wa zao hilo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na ukosefu wa soko la uhakika na  ukosefu wa usafiri kutoka shambani kwenda sokoni.

Wameiomba serikali kushirikiana mashirika na kampuni binafsi kuwahamasisha wakulima  kuongeza jitihada katika kilimo hicho na kuongeza idadi ya maofisa ugani ili wawaongezee uwezo wa kuzalisha na kutafuta masoko zaidi. Na ikiwezekana serikali iwasaidie wakulima hawa kuwatangazia kazi zao katika soko la nje ili kuwaendeleza wakulima.

kwa mantiki hiyo basi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA),  pia wanapaswa kuwafikia wakulima ili waweze kukagua kazi za wakulima, kuwaelimishe kwa lengo la kuwawezesha kuzalisha kwa ubora zaidi ili kuwapa uelewa wakulima ni jinsi gani wanaweza kuandaa bidhaa zao ili waweze kufika mbali zaidi na kujikwamua kutoka katika wimbi la kilimo duni na kufika mbali zaidi kama ilivyo katika kilimo cha mazao mengine kama vile kahawa, korosho na mazao mengine ambayo yapo kwenye ramani ya kuipatia pesa za kigeni nchi yetu.

Nae Robert Kileo afisa habari wa Ukiriguru amesema kuwa Kutokana na umuhimu wa viazi lishe Kituo cha utafiti wa Kilimo Ukiriguru  kikishirikiana na TAHEA kwa pamoja wamebuni mpango wa  kuhamasisha wakulima na wananchi kwa ujumla ili wafahamu umuhimu wa zao hilo.



Kileo alisema kwakuwa Tanzania ipo katika kufanya mapindizi ya kijani na kilimo kwanza inatakiwa kila sekta katika serikali kuunga mkono jitihada za wakulima ili kufanya kazi yakilimo iwe ajira kwa watanzania wengi ambao kilio chao kikubwa sasa ni ukosefu wa ajira nchini. 

Wataalam kutoka katika vituo hivyo wanasema kuwa, mbali na kuwaelimisha kuhusu faida zake pia wakulima wanaelimishwa umuhimu wa usindikaji wa viazi lishe na uendelezaji wa masoko katika mikoa ya kanda ya ziwa
Hivyo  serikali inapaswa kuingilia kati katika kuhamasisha wananchi kulima zao hilo, kutafuta masoko kwa ajili ya wakulima ambao wamekwishaanzisha kilimo hicho na kuwataka wananchi ambao bado hawajajiunga wafanye hivyo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Ushauri mwingine kwa serikali ni kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kukibadilisha kilimo cha viazi lishe ili kiwe cha kisasa na cha tija pamoja na kumwezesha mkulima mdogo kumiliki ardhi  na kuanzisha vituo vya kumsaidia.

Baadhi ya bidhaa zitokanazo na vizi lishe

ILIYOKUWA BAR SASA NI KANISA

 

Baa iliyopo Sinza-Lion jijini Dar ambayo imegeuzwa kuwa kanisa.
WAKATI matukio mengi ya kushangaza na kushtukiza yakiendelea kutokea kila siku duniani, neno la Mungu nalo linazidi kushika kasi kufuatia baa moja iliyopo Sinza-Lion jijini Dar kugeuzwa kuwa kanisa.Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baa hiyo maarufu iitwayo The Don, ukumbi wake ambao ulikuwa ukitumika kwa watu kupiga ulabu, hivi sasa unatumiwa na waumini wa kanisa linalojukana kama Impact International Christian Centre kupata mahubiri. Lakini cha kushangaza ilibainika kwamba katika maandishi makubwa yanayolinadi jina la baa hiyo, chini yake ndipo limewekwa bango linaloonyesha kanisa hilo, kitu ambacho kwa mtu mgeni, ni vigumu kuelewa mara moja.

MWAAFUNZI WA TANZANIA AIBUKA KIDEDEA TUZO ZA ISHA SADC


Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza mwanafunzi wa kidato cha nne Neema Steven Mtwanga(16) anayesoma katika shule ya sekondari Naboti Makambako,Njombe baada ya kuibuka mshindi wa kwanza katika utunzi wa insha katika shindano lililoandaliwa na Jumuiya ya uchumi ya maendeleo kusini mwa Afrika(SADC).Rais Kikwete alimpongeza mwanafunzi huyo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa wakuu wa nchi za SADC unaofanyika katika mji wa kitalii wa Victoria Falls, nchini Zimbabwe ambapo mwanafunzi huyo aliandika insha inayohusu mabadiliko ya tabia nchi.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete(kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wakuu na wawakilishi wa nchi za Jumuiya ya uchumi kusini mwa Afrika SADC muda mfupi baada ya ufunguzi wa mkutano wa 34 wa jumuiya hiyo uliofanyika katika hoteli ya Elephant Hills mjini Victoria Falls Zimbabwe leo.Katikati ji mwenyeji wa Mkutano huo Rais Robert Mugabe na mkewe Grace Mugabe(picha na Freddy Maro)

WATU WAWILI WAFARIKI PAPO HAPO BAADA YA KUGONGWA NA GARI ILIYOBEBA MAITI 10.


 Watu wawili wamefariki dunia papo hapo baada ya gari aina ya Land Cruser ilikuwa imebeba maiti 10 zikitokea hosiptali ya taifa Muhimbili kwenda hospitali ya St Francis Ifakara kugonga wapanda pikipiki katika eneo la Mtego wa simba Mikese mkoani Morogoro
Maiti zilizokuwa zinapelekwa hospitli ya St Fancis Ifakar kwa lengo la kufanya utafiti 

Gari lililosababisha ajali toyota Land Cruser 

 Mwili wa mmoja waliofariki katika ajali hiyo 
Pikipiki iliyosababishiwa ajali na kutoa uhai wa watu wawili waliokuwa wanakwenda shamba
Akizungumzia tukio hilo kwenye  eneo la tukio mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Bonifasi Mbao amesema gari hiyo ikiendeshwana dereva Pankrasi Pasco mkazi wa ifakara iliwagonga wapanda pikipiki Shaban Rajab na Ally Benulo wakazi wa Mikese na kufariki dunia papo hapo na chanzo cha ajali  mwendo kasi na dereva anashikiliwa na jeshi la polisi, kuhusu maiti 10 zilizokuwemo katika gari hiyo amesema zilikuwa zikipelekwa hospitli ya St Fancis Ifakar kwa lengo la kufanya utafiti na mafunzo ambapo wanafanya mawasilino ya kuzifikisha katika hospitali hiyo.
Nao wananchi walioshuhudia tukio hilo wameeleleza chanzo cha ajali hiyo ni mwendo  kasi huku wakilalamikia matukio ya ajali nyingi katika eneo hilo kutokana na kona na kuomba serikali kuweka matuta  na vibao vya tahadhari.

SAMAKI MKUBWA AVULIWA MTO AMAZO



Samaki aliye na urefu wa mita tatu aliyekuwa maarufu katika mto Amazon amevuliwa hadi ameangamia

Watafiti wamedhihirisha kuwa samaki huyo mkubwa hapatikani tena katika maeneo aliyokuwa maarufu.

Imebainika sasa kuwa samaki wa Arapaima alipatikana katika maeneo 8 kati ya 41 zilizofanyiwa utafiti, na idadi ya samaki huyo ilikuwa ndogo sana kuliko ilivyokuwa inatarajiwa.

Wavuvi walipewa mafunzo jinsi ya kuhesabu samaki hao ili kufanikisha utafiti huo mkubwa.

Watafiti walikata kauli kuwa athari za uvuvi kwa samaki wa kitropiki zilikuwa mbaya zaidi ya ilivyoaminika hapo awali.

Matokeo ya utafitihuo yaliripotiwa kwa shirika la uhifadhi wa mazingira yanayozalisha viumbe vya majini ''Aquatic Conservation: Freshwater and Marine Ecosystems''.

Arapaima huweza kuwa na uzani wa kilo 181 na ni mojawapo ya samaki wakubwa zaidi wanoishi katika maji yasiyo na chumvi.
 
 Samaki mkubwa zaidi wa maji matamu Arapaima. 

Samaki hao hupumua hewa sawa na binadamu, hivyo basi huibuka kutoka majini kupumua kila baada ya dakika kati ya 10-15 hivyo basi huwa ni rahisi kuwakamata.

Ukubwa wa Arapaima huvutia wavuvi kuwawinda na aghalabu huwanasa kwa kutumia chusa au nyavu za uvuvi.

Karne moja iliyopita, idadi ya Arapaima ilikuwa kubwa katika mto wa Amazon, lakini watafiti wanasema kuvua kupita kiasi kumesababisha idadi hiyo kupungua kwa kiwango kikubwa sana.

Hapo awali, utafiti nadharia ulitabiri kuwa uvuvi hauwezi kuangamiza aina fulani ya samaki majini kwani wavuvi huenda kuvua maeneo tofauti idadi ya samaki inapopungua katika eneo moja.

Wanasayansi, wakiongozwa na Leandro Castello, kutoka Virginia Marekani, walitaka kufahamu afya ya samaki wa Arapaima walioko eneo la chini la Amazon.

Aidha walitaka kugundua iwapo shughuli za uvuvi ziliunga mkono au kupinga utabiri wa nadharia tofauti.

Kuna nadharia zinazopendekeza kuwa samaki wakubwa, walio ghali, na ambao ni rahisi kukamatwa huweza kuvuliwa na kuisha majini, huku nadharia zingine zikipinga msimamo huo.

Watafiti hao walihoji wavuvi 182, walioaminika kuwa magwiji na wenzao, katika jamiii 81, zinazoishi katika eneo la kilomita 1,040, la Amazon.

Shughuli hiyo ilijumuishwa hesabu ya Kulifanywa ya samaki katika jamii 41 kati ya jamii zilizohojiwa.

Wavuvi nane walifunzwa kuhesabu idadi ya Arapaima pindi tu walipotokea majini.

Matokeo ya hesabu hiyo ni kuwa idadi ya Arapaima ilikuwa imepunguka katika asilimia 57% ya eneo la utafiti, Arapaima hawakuwepo katika asilimia 19% ya eneo hilo, na walivuliwa kupita kiasi katika asilimia 17% ya eneo hilo la utafiti, huku asilimia 5% tu wakifanya uvuvi unaokubalika.

Kwa 2% ya jamii zilizofanyiwa utafiti, samaki hao hawakuvuliwa.

Thursday, August 14, 2014

UGONJWA WA EBOLA' WASABABISHA TAFRANI SHINYANGA



Wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, kwa siku mbili mfululizo walikumbwa na kiwewe, baada ya kuenea uvumi kwamba kuna mgonjwa wa mwenye homa hatari ya ebola, aliyefikishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. 
Taarifa za kuwepo kwa mgonjwa huyo, zilidai kuwa mgonjwa huyo alitoka katika moja ya mitaa ya Manispaa ya Shinyanga na  alikuwa akitokwa damu puani na mdomoni kabla ya kuzimia.
Akizungumzia hali hiyo jana, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Ntuli Kapologwe alisema mgonjwa huyo ambaye alikuwa akitokwa damu mdomoni na puani, alifika hospitalini hapo juzi na baada ya kufika wauguzi na madaktari walitaharuki.
Kwa mujibu wa Dk Kapologwe, mgonjwa huyo alipelekwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), huku baadhi ya wauguzi na madaktari wakimkimbia hali iliyotia hofu kwa baadhi ya wahudumu na hata wagonjwa hospitalini hapo.
Hata hivyo, Dk Kapologwe alisema baada ya uchunguzi wa awali, ilibainika kuwa mgonjwa huyo ana matatizo ya kutokwa damu mara kwa mara na hajaambukizwa virusi hao wa ebola.
Akielezea namna mkoa ulivyojiandaa kukabiliana na ugonjwa huo uliokwishaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi, Dk Kapologwe alisema waganga wakuu katika halmashauri zote sita za wilaya mkoani Shinyanga, wameshajiandaa.
Alisema wamekubaliana atakapogundulika mtu mwenye dalili za ugonjwa huo, taarifa itolewe mara moja katika ngazi ya mkoa, ambako kuna timu maalumu ya wataalamu iliyoandaliwa kushughulika na ugonjwa huo hatari.
Baada ya taarifa kutolewa kwa mujibu wa Dk Kapologwe, timu hiyo itathibitisha kama mgojwa ana dalili zote za ebola na taarifa kutolewa kwa umma.
Wakati ugonjwa huo ukisababisha kiwewe mkoani Shinyanga,   mkoani Kagera, Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe ameshauri wakazi wa mkoa huo kuwa macho na tayari kutoa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyo jirani waonapo mtu mwenye dalili  za ugonjwa huo. 
Alitoa mwito huo kupitia kwa waandishi wa habari aliozungumza nao jana ofisini kwake mjini hapa, baada ya kuibuka taarifa kuwa Rwanda kulikuwa na mtu anayehisiwa kuwa na ebola. 
Hata hivyo, Waziri wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho alisema juzi kuwa mwanafunzi mmoja wa Ujerumani aliyefika nchini humo akitokea Liberia,  alihisiwa kuwa na ugonjwa huo lakini baada ya sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za kimataifa, hakukutwa na ugonjwa huo.
Massawe alisema Mkoa wa Kagera unapakana na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki na pia upo mwingiliano wa watu na shughuli mbalimbali za kijamii. 
Alisema nchi jirani zikipata mlipuko wa ugonjwa huo, upo uwezekano wa kuvuka mipaka na kuingia mkoani Kagera, hivyo ni  wajibu wa kila mmoja kutoa taarifa akiona mtu anayedhaniwa kuwa na ugonjwa huo. 
Dalili za ugonjwa huo unaoenezwa na virusi vya ebola ni pamoja na  kutokwa na damu sehemu mbali mbali za mwili, kuumwa na kichwa, mwili kuishiwa nguvu, maumivu ya misuli na hatimaye kifo.
Ugonjwa huo unaambukizwa kwa kugusa damu na majimaji ya mgonjwa pamoja na kugusa vifaa au nguo za mgonjwa.
Massawe alisema Kagera wamechukua hatua kwa kuweka mikakati kuhakikisha mlipuko wa ugonjwa  hauingii nchini  kupitia mipakani.  
Miongoni mwa halmashauri ambazo zimeelekezwa kuchukua hadhari kutokana na kuwa mpakani mwa nchi, ni wilaya ya Bukoba, Missenyi, Karagwe, Kyerwa na Ngara.