Wafanyabisahara
jijini Mwanza leo wameanza mgomo wa kutofungua maduka yao kwa siku
zisizojulikana kwa kile walichodai Mkurugenzi wa jiji hilo, Hassan Hida
amekataa kukutana nao kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili.
Mgomo huo
utakuwa wa pili kufanyika baada ya mara ya kwanza kutokea wakati
wafanyabiashara hao wakigomea matumizi ya mashine za Stakabadhi za
Elekitroniki (EFD).
Hata hivyo
mgomo huu ulioanza leo hauhusishi tena mashine za EFD badala yake
umejikita katika matatizo yanayowakabili ambayo ni ongezeko la kodi ya
taka kutoka Sh 8,000 hadi 10,000, kutoza fedha za kuweka bidhaa zao nje
ya duka na mambo mengine ya kukamatiwa mali zao.
Uamuzi huo
ulifikiwa juzi katika mkutano mkuu ulioitishwa na Jumuiya ya
Wafanyabiashara Tanzania (JWT), mkoa wa Mwanza kwa lengo la kutoa
taarifa za mazungumzo kati ya Serikali juu ya matumizi ya mashine za
EFD.
Kabla ya
kufikia azimio la kutofungua maduka yao, Mwenyekiti wa JWT, mkoa wa
Mwanza, Christopher Wambura aliwaeleza wafanyabiashara hao jitihada
alizofanya za kukutana na mkurugenzi huyo mara zote ziligonga mwamba.
“Ndugu zangu
wafanyabiashara mliniagiza pamoja na viongozi wenzangu tutafute
suluhisho la matatizo yanayotukabili katika biashara zetu hapa jijini
Mwanza, wakati tunahangaika hapa kwetu, viongozi wa kitaifa wa JWT nao
walikuwa wanahangaika huko Dar es Salaam.
“Kwa bahati
nzuri uongozi wa kitaifa umefanikiwa kwenda Ikulu na kukutana na
wawakilishi wa Rais Jakaya Kikwete, baada ya hapo walikutana na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), ndio maana leo mnaona hakuna usumbufu juu ya mashine za EFD.
“Wakati
usumbufu wa EFD ukiwa umepotea, kero zetu zinazotukabili hapa Mwanza
bado hazitaki kutatuliwa na uongozi wa jiji, mkurugenzi anatukimbia kila
tunapopanga kukutana naye.
“Tumefanya
jitihada za kukutana na Mkuu wa Mkoa, Evarist Ndikilo, Mkuu wa Wilaya ya
Nyamagana, Baraka Koni na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji, Titto Mahinya wote
walionyesha jitihada za kutusaidia kukutana na mkurugenzi lakini
hatukukutana mpaka leo hii,”alisema.
Wambura alisema
pamoja na jitihada hizo, mara zote mkurugenzi amekuwa akiwaeleza
kutokuwa na nafasi ya kukutana nao kwa kile alichodai kubanwa na
majukumu ya kazi pamoja na kuwa nje ya mkoa kwa shughuli maalumu.
Pamoja na
masuala mengi yaliyozungumzwa hapo, wafanyabiashara na viongozi wao
walikubaliana kutofungua maduka yao hadi hapo mkurugenzi atakapokutana
nao huku wakisisitiza na kutoa onyo kwa wale watakaokiuka maazimio yao.
Mkurugenzi anena
Mpekuzi
ilimtafuta Mkurugenzi wa jiji hilo kwa njia ya simu, ambapo alisema yupo
nje ya ofisi, lakini amewataka viongozi wa JWT wakutane naye
kesho saa nne ofisini kwake.
“Nipo nje ya
ofisi, muda huu siwezi kuzungumzia mgomo huo, lakini nimewaomba
wafungue maduka yao halafu Viongozi wao wafike Ofisini kwangu
kesho saa nne tuzungumze,” alisema kwa ufupi.
TRA Mwanza
Kwa upande wa
Meneja wa TRA mkoa wa Mwanza, Jeremia Lusana amesema kitendo cha
wafanyabiashara hao kugoma kinasababisha hasara kubwa katika suala la
mapato huku akitishia kuwafungia lenseni za biashara zao.
“Tumechoka
kutishwa na mgomo wa wafanyabiashara hao, umefika muda wa kuangalia
namna ya kuwafungia leseni zao ili wakae nyumbani, biashara yao ina
manufaa kwao na sisi, kipindi kile tulipata hasara kwa sababu mgomo
ulishtukiza." Amesema Lusana
Lusana amesema
TRA haina uwezo wa kuwalazimisha kufungua maduka, hivyo watasubiri hadi
hapo watakapofungua ndipo watakapoendelea na shughuli zao ukusanyaji
mapato kwao.
No comments:
Post a Comment