Tuesday, August 12, 2014

MJUMBE WA BUNGE MAALUM LA KATIBA APIGWA NA VIJANA WANAODAIWA KUWA MASHABIKI WA CHADEMA

 mjumbe-201
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta, akimjulia hali, mjumbe wa bunge hilo, kupitia kundi la wateule 201, Thomas Magnus Mgoli katika hospitali ya mkoa wa Dodoma ambako amelazwa kwa matibabu baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwenye mgahawa wa Lydia. PICHA: SELEMANI MPOCHI

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Thomas Markus Mgoli amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kushambuliwa kwa kipigo na watu wasiojulikana.

Thomas ambaye ni mjumbe wa bunge hilo kutoka kundi la 201 akiwakilisha Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), amelazwa wodi namba
18 ya daraja la kwanza, akipatiwa matibabu.

Akizungumza kwa tabu kutokana na kusumbuliwa na maumivu makali yanayotokana na kipigo hicho, mjumbe huyo alidai alivamiwa na watu hao wakati akitoka kununua bia kwenye baa iliyopo eneo la Area A, karibu na shule ya msingi Chamwino.

“Around saa 2 kwenda saa 3 usiku, nilikuwa kwenye maeneo ninayoishi, nikaingia kwenye baa ambako ni kawaida yangu huwa nakwenda kununua vinywaji na kurudi ndani, nikakutana vijana ambao huwa siku zote wanajitambulisha kwangu kuwa ni wanasiasa," alidai na kuongeza kuwa:

" Wakanihoji uhalali wangu wa kuwepo Dodoma kuendelea na bunge maalum la katiba, nilipokuwa naendelea kujieleza ndipo waliponivamia na kuanza kunipiga wakisema mimi ni kibaraka na hawatakubali tuendelee na haya tunayoyafanya.”

Alisema hakuna haja ya kuuana wala kuumizana ila ni vizuri ifike mahali, tukubali kwa kutokubaliana na tujenge misingi ya kukubaliana.

“Nina amini hivyo kwa sababu si mara ya kwanza nimewakuta pale baa, jana ilikuwa ni zaidi ya siku ya sita kukutana nao na kila siku
wamekuwa wakitengeneza mijadala na tunajadiliana. Namkumbuka aliyenipiga lakini hao wengine watatu siwajui kabisa, ”alisema mjumbe huyo.

SITTA AZUNGUMZA


 
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, akizungumza baada ya kumtembelea mjumbe huyo hospitalini hapo, alisema amenusurika kifo kwa kuwa alikuwa anaishi karibu na baa hiyo.

“Inabidi nitoe tahadhari kwa wajumbe wote kuanzia sasa kuhusu usalama wao, siyo utamaduni wetu kupigana na wale ambao wana njama zao za kukwamisha bunge la katiba tuko hapa kisheria, ijione tu kwamba wao ndiyoo wana haki na sisi pia tuna haki,”alisema Sitta.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanahojiwa watu watatu kwa mahojiano zaidi.

Misime alisema Mgoli aliripoti tukio hilo jana usiku akidai kuwa alikuwa baa na wenzake watatu wakaanza kubishana kuhusiana na mvutano unaondelea bungeni na baada ya kushindwa kuelewana, walianza kumshambulia kwa kipigo.

“Hadi sasa tunashikilia watatu tunawahoji ili kupata ukweli wa tukio hilo, siwezi kuwataja kwa sasa sipo ofisini,” alisema Kamanda huyo.



Alipotakiwa na NIPASHE kama tukio hilo linatokana na masuala ya kiasa, alisisitiza kuwa: “ Ninachojua tunawashikilia watuhumiwa watatu haijalishi ni wafuasi wa chama gani.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Mzee Nassor amethibitisha kupokelewa kwa majeruhi huo na kusema kuwa amefanyiwa vipimo na kuanza kupatiwa matibabu chini ya jopo la madaktari wa hospitali hiyo.

Imeandikwa na Godfrey Mushi; Salome Kitomari na Editha Majura, Dodoma.

No comments:

Post a Comment