Tuesday, August 12, 2014

MADAKTARI BINGWA WA UPASUAJI WA MISHIPA YA FAHAMU, UBONGO KUTOKA MISRI KUTOA HUDUMA BURE MUHIMBILI

MADAKTARI bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, masikio na viungo kutoka nchini Misri wako nchini. Wamekuja kufanya kampeni maalumu ya afya, upasuaji na huduma mbalimbali kwa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI).

Chini ya kampeni hiyo, wagonjwa walioidhinishwa kufanyiwa upasuaji katika maeneo hayo, watapatiwa huduma na madaktari hao hadi Jumatatu ijayo.

Walianza kutoa huduma jana. Huduma ya upasuaji kwa madaktari hao, imeandaliwa na Shirika la Kimataifa linalojihusisha na utoaji wa misaada na huduma kwa jamii ya Al-Rahma International na African Relief Committee of Kuwait kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Othman Kiloloma alisema Tanzania ina upungufu mkubwa wa madaktari bingwa wa maeneo hayo, hususani ubongo na mishipa ya fahamu, ambapo kwa sasa wako watano.

“Licha ya upungufu wa madaktari wa maeneo hayo lakini waliopo wako MOI jambo ambalo husababisha kutofikiwa kwa wagonjwa wengi na ambao wana mahitaji ya haraka hususani wale walioko maeneo ya pembezoni,” alisema Dk Kiloloma.

Aliongeza kuwa wataalamu wengi, bado wako masomoni nchini Misri na Afrika Kusini.

Alisema kwa viwango vinavyotakiwa, daktari bingwa wa mishipa ya fahamu na ubongo, hutakiwa kuwaona wagonjwa 6,000 lakini kutokana na uhaba wa madaktari daktari mmoja hujikuta akiona wagonjwa milioni 11 hadi 12.

Akizungumza Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Masikio, Profesa Mohammed el Begermy alisema wamekuja nchini kwa lengo la kuokoa wagonjwa wa masikio, ambao wengine wamejikuta wakishindwa kusikia.

Alisema wana uwezo wa kufanya upasuaji, utakaowezesha mgonjwa kusikia tena, kwani asilimia 60 ya wagonjwa wasiosikia hukutana na hali hiyo kutokana na kushindwa kufikiwa na huduma stahiki, huku watoto wengine wakishindwa kutamka maneno kwa kushindwa kusikia.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Profesa Hussein Moharram alisema eneo hilo ni la kipekee ambalo huchukua muda mrefu kusomea na linahitaji kutoa huduma kubwa na za dharura.

“Kupata mtaalamu wa eneo hili, inahitajika kusoma takribani miaka 10 hadi 15 na kutokana na wanaosomea taaluma hiyo kutafuta njia ya mkato, hivyo husababisha wataalamu wa eneo hilo kuwa wachache kwani hata upasuaji wake huchukua muda mrefu kuanzia saa sita,” alisema.

Alisema kuwepo katika kampeni hiyo, kutasaidia kushirikiana na wataalamu wa Tanzania, kuongeza uzoefu na kuharakisha huduma kwa wagonjwa.

No comments:

Post a Comment