ZAO la muhogo ni miongoni mwa mazao
yasiyopewa kipaumbele kikubwa hapa nchini katika ulaji na kibiashara pia huku wanasansi na watafiti wakizidi
kulitangazia neema zao hilo.
Zao hilo ambalo limekumbwa na
maswahibu ya magonjwa ambayo yalipelekea wakulima kukata tamaa ya kulima zao
hilo limeonekana ni zao lenye manufaa kwa wakulima ikiwa watafuata maelekezo ya
kilimo bora na watafiti wa kilimo
Hata hivyo imebainika kuwa zao la
muhogo licha ya kwamba linalimwa kwa wingi hapa nchini lakini faida yake
haijaonekana kutokana na jinsi linavyoandaliwa na kusababisha mkulima kupata
faida kidogo.
Hivi sasa imebainika kuwa zao hilo
ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa kutokana na kuonekana lina matumizi
makubwa katika shughuli za viwandani ikiwa ni pamoja utengenezaji wa sabuni ya unga, pipi, dawa, juisi tambi,bisukuti,mafuta ya lishe,keki, kuni, mboga,nguo
pamoja na bidhaa nyingine nyingi.
Hayo yalibainishwa na Bi Mariam
Mtunguja ambapo alisema Tanzania inaagiza wanga (starch) kutoka nje wakati
uwezekano wa kuwa na bidhaa hiyo hapa nchini ni kubwa. “ Nashangaa kuona
viwanda vingi hapa Tanzania vinaagiza wanga kutoka nje ya nchi kwa bei ghali
wakati uwezo wa kupata wanga kwa wingi upo kwa kutumia zao la mhogo”.
Bi Mariam Mtunguja akiendelea na
kazi ndani ya maabara za MARI Dar es salaam
Hivyo yeye kama mwanasayansi na mtafiti
ameamua kuingia maabara na kufanya utafiti wa aina gani ya muhogo ambao una
kiasi kikubwa na bora cha wanga ili kuwashauri wakulima na wafanyabiashara
kulima zao hilo kwa manufaa yao na serikali kwa ujumla.
Alisema kuwa yeye ameamua kufanya utafiti huo ili kupata muhogo
wenye kukidhi vigezo vya wanga inayotumika viwandani ili wakulima wa zao hilo
wanufaike na kilimo cha zao hilo.
“ Utafiti huu utakamilika mwezi wa
tisa ambapo tayari itakuwa imefahamika ni aina gani ya muhogo inatakiwa kulimwa
kwa ajili ya uzalishaji wa wanga inayohitajika viwandani” alisema Bi Mariam
Mtafiti huyo alisema kazi itabakia
kwa serikali kutafuta masoko kwani anahakika wakulima wanalima mazao lakini
hawana pa kuyapeleka kutokana na kutokuwa na masoko ya uhakika ya mazao yao.
Kwa habari hii ni neema kwa zao la
muhogo ambalo kila ufikapo msimu wa kilimo lenyewe halifikiriwi kulimwa kama
ilivyo mazao ya mahindi, mpunga Maharage na mengineyo kwani muhogo hulimwa kama
zao la kuzuia njaa kutokana na uwezo wake wa kustahimili ukame hivyo wengi
hulima kwa tahadhali na si kwa faida kama ilivyo kwa mazao mengine.
Hivyo kama wazalishaji
wa viwandani wakiamua kukaa na wakulima wakapeana elimu ya kusindika unga wa
muhogo unaotakiwa kwenye viwanda vyao, Tanzania inaweza kumaliza tatizo la njaa
na umasikini kwa wakati mmoja.
Akiongea na mwandishi Bwana Athumani
Idd mkulima wa mihogo katika kijiji cha Gwata mkoani Pwani alisema “serikali
itutafutie soko la mihogo ili tunufaike kwani zao hili ni chanzo cha ajira kama
ilivyo kwa mazao mengine”. Amesema kuwa huwa wanapata faida kiasi wakati wa
mfungo wa waumini wa kiislam kwakuwa hutumia mihogo kwa ajili ya kuandaa futari
vinginevyo kwao wao ni hasara tuu ila hulima kwa kuwa hawana ajira nyingine
zaidi ya kilimo.
Nae Bwana Richard Kasuga afisa
mawasiliano wa wizara ya kilimo na chakula alisema kuwa serikali inasubiri
matokeo ya utafiti huo ili watakapo anza kutangaza bidhaa ya unga huo wawe na
ukakika ya kuwa bidhaa hiyo ipo. “hatuwezi kutafuta masoko bila kuwa na uhakika
wa bidhaa hiyo kuwepo, hivyo pindi
utafiti utakapokamilika watatujulisha ndipo tutukapoanza kutangaza kwa wenye
viwanda na nchi zingine wanaotumia bidhaa hiyo.
Hivi sasa zao
la muhogo limezidi kupata umaarufu zaidi, ambapo kadri siku zinavyosogea
linabadilika na kuwa zao la kibiashara hii ni kutokana na tafiti
zinazoendelea kufanywa hapa nchini.
Julias
James kijana anayejishughulisha na kilimo cha
mihogo mkoani Pwani alisema “tangu nizaliwe sijawahi ona zao ambalo kila
sehemu ya zao ni faida kama mhogo, mzizi ni chakula, shina ni kuni wakati majani
ni mboga, jamani kwani twataka kitu gani kifanyike”. Hakuishia hapo bali
alizitaja faida ya kulima zao hilo ambapo alisema ni zao linalostahimili ukame
na halihitaji rutuba nyingi hivyo kumpa urahisi mkulima kwa kumpunguzia
gharama.
Nae
mkulima wa mboga mboga katika eneo la mchicha
jijini Dar es salaam ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema kuwa
anatamani sana kama serikali ingeruhusu wakulima wapewe mbegu mpya za mihogo
kwani tangu watangaze kuwa utafiti wa kupatikana kwa mbegu mpya isioathiriwa na
magonjwa umefanikiwa hatuioni madukani sasa nini faida ya kututangazia”? aliuliza swali ambalo lilikosa mtu wa
kulijibu.
Tanzania tumekuwa tukiachwa nyuma na
nchi kama kama vile Afrika ya kusini, Nigeria,Ghana, na zingine za
ulaya kama vile Italia, Thailand na kwingineko ambako kuna viwanda vikubwa kwa
ajili ya kusindika mihogo na kufanya wakulima wa nchi hizo kunufaika na kilimo hicho.
Ikumbukwe
yakuwa katika kuijenga Tanizania salama bila njaa ni lazima kanuni za kilimo bora zifuatwe, matumizi ya
mbegu bora, bila kusahaku kufuata utabiri wa hali ya hewa ili kuenenda sawa na kauli mbiu
ya kilimo kwanza na si kwanza kilimo.
No comments:
Post a Comment