Wednesday, August 20, 2014

IKULU YAKANUSHA JK KUHOJIWA NA OBAMA KUHUSU FEDHA ZA IPTL

 
 
MKURUGENZI wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu amekanusha madai yaliyotangazwa hivi karibuni kwamba, Rais Jakaya Kikwete amehojiwa na Rais wa Marekani, Barack Obama, kuhusu fedha za kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam jana kukanusha taarifa hizo zilizotolewa na moja ya gazeti la kila siku nchini, (si Habarileo), Rweyemamu alisema katika ziara ya Rais nchini Marekani hivi karibuni, hakukutana kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Obama.
Kwa mujibu wa Rweyemamu, katika ziara hiyo ambayo Rais Kikwete alihudhuria Mkutano wa Viongozi wa Bara la Afrika na Marekani, alikutana na Mkurugenzi mpya wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

“Rais pia alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na katika mikutano yote hiyo hakuna jambo lolote linalohusu IPTL lililojadiliwa wala kuulizwa.

“Huu ni uongo na ni habari ya kutungwa na habari kama hizi huandikwa kwa ajenda, sasa sijui hawa wenzetu waliandika kwa ajenda zipi,” alifafanua.
Alisema masuala yote yanayohusu kilichojiri katika mkutano huo na namna Tanzania ilivyonufaika katika sekta mbalimbali, yatabainishwa hivi karibuni na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Hoja ya kuchukuliwa kwa karibu Sh bilioni 20 IPTL katika akaunti ya Escrow iliyokuwa BoT, iliwasilishwa bungeni hivi karibuni na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), akidai kuna wizi umefanyika.

Kutokana na hoja hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa ufafanuzi kwamba uamuzi wa kuingiza takribani Sh bilioni 20 katika akaunti ya Escrow, haukuwa wa kificho kwa kuwa fedha hizo zilikuwa za IPTL na zilitolewa na kukabidhiwa kwa kampuni hiyo ya kufua umeme, kwa uamuzi wa Mahakama.

Alifafanua kuwa suala la IPTL ni la muda mrefu tangu 1994, wakati huo Serikali baada ya kuona lipo tatizo la umeme, ilitafuta mtu aliyekuwa tayari kuzalisha umeme.

Mkataba ulionesha umeme utakaozalishwa utauzwa katika Shirika la Umeme (Tanesco) na ulikuwa na sehemu mbili kwa maana ya malipo ya uwepo wa mtambo na pia uzalishaji.

Wakati wakiendelea kuzalisha umeme, Pinda alisema kulitokea mgogoro upande wa Tanesco na IPTL, kuhusu kodi inayopaswa kulipwa na baadaye ukazaa kesi iliyopelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

Wakati mgogoro huo ukiendelea, Pinda alisema Serikali ililazimika kufungua akaunti ya Escrow na fedha kutoka Tanesco zikawa zikilipwa kwenye akaunti hiyo.

Alisema fedha zilizokuwa zimewekwa kwenye akaunti hiyo, ni za IPTL na katika uamuzi wa Mahakama ikaamriwa fedha hizo zipelekwe IPTL kwa kuwa ni fedha zao.

“Fedha hizo zikapelekwa IPTL, jambo tunalopaswa kama wabunge kujiridhisha nalo ni je, VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ipo kweli au haipo?,” alisema Pinda.

Alisema baada ya kesi kumalizika, Tanesco na IPTL walikaa wakatazama kiasi kinachodaiwa, wakafika mahali wakakubaliana ni kiasi gani cha fedha kilipwe. Alisema kwa upande huo, kama kuna masuala yanaweza kupatiwa majibu bila mjadala na kuvutana.

“Kubwa ni pale zogo limejikita zaidi kwenye kuondoa fedha kutoka akaunti ya Escrow kutoka Benki Kuu kupeleka IPTL na maswali ambayo yamejitokeza kwamba kodi haikulipwa, ufisadi upo, unajiuliza wa nini kama fedha ile ilikuwa ni fedha yao,” alihoji Pinda.

Kutokana na hali hiyo, Pinda aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza na kujiridhisha kama kweli upo uchotaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti hiyo, uchunguzi ambao matokeo yake hayajatoka mpaka sasa.
CHANZO: Habari Leo

No comments:

Post a Comment