RAIA wa
nchi ya Ethiopia Dawita Alalo (25) amekufa alipokuwa akipatiwa matibabu
kwenye kituo cha afya cha Chalinze kata ya Bwilingu wilaya ya Bagamoyo
mkoani Pwani.Marehemu
alikuwa ni kati ya raia 48 wa nchi hiyo walikamatwa wakiwa kwenye msitu
wa kijiji cha Visakazi Ubena Zomozi tarafa ya Chalinze Agosti 22 mwaka
huu, baada ya kuingia nchini bila ya kibali.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha kaimu kamanda wa
polisi mkoani humo Mrakibu Mwandamizi (SSP) Athuman Mwambalaswa alisema
kuwa marehemu ni miongoni mwa wahamiaji haramu 11 waliokuwa wamelazwa
kituoni hapo wakipatiwa matibabu.
Kamanda
Mwambalaswa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 26 majira saa 7:30
usiku alipokuwa akipatiwa matibabu kituoni hapo baada ya kuugua ugonjwa
wa malaria.
Wakati huo huo mlinzi wa baa ya Silent Inn Jamat Mandama (55) amefariki dunia baada ya kunywa pombe nyingi bila ya kula chakula.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27 mwaka huu majira ya saa 1 usiku huko Umwe kata ya Ikwiri wilayani Rufiji.
Aidha alisema kuwa mlinzi huyo alikutwa amekufa akiwa lindoni kwenye baa hiyo.
No comments:
Post a Comment