Wednesday, August 27, 2014

RAIS KIKWETE AWAITA UKAWA IKULU....ATAKA MAMBO YENYE UTATA YAWEKWE KANDO


RAIS Jakaya Kikwete amesema yupo tayari kukutana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili kunusuru mchakato wa Katiba mpya.
 Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kupinga hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kumtuma Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, kusaka suluhu na viongozi wa Ukawa.Akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe mjini Morogoro juzi, mara baada ya kusoma risala yao na kuunga mkono Bunge la Katiba, Rais Kikwete alisema    hana sababu ya kutokutana na viongozi waliosusia vikao vya Bunge. Alisema kutokana na hali hiyo, yupo tayari kukutana nao, na kwamba wanajua namna ya kukutana naye ili waweze kufanya mazungumzo yatakayoliwezesha taifa kupata Katiba mpya.
 
“Mimi sina tatizo la kukutana nao. Wanajua jinsi ya kukutana nami ili tuweze kutafuta namna ya kumaliza tofauti hizi.
“Mimi naishi kwa matumaini. Naamini kuwa tutafika mwisho vizuri. Mchakato ni mgumu, lakini barabara ndefu haikosi kona. Tukidhamiria kweli kweli tutafika tuendako vizuri,” alisema Rais Kikwete.
Alisema anasikitishwa na tofauti za viongozi wa siasa na kuleta mfarakano kwa taifa, hali ya kuwa tangu awali aliwaambia kuwa wakijiruhusu kushindana na kuviziana ni wazi mchakato wa Katiba utakwama.
“Niliwaambia kuwa Katiba inayotafutwa siyo Katiba ya CCM, ama ya Chadema, ama ya NCCR, ama ya CUF. Niliwaambia kuwa hii ni Katiba ya wananchi wa Tanzania. Ni vyema tukakubaliana kuwa yenye kutugawa tukayaacha kwa sasa na kukubaliana kwa yale ambayo hatuna tofauti,”alisema.
Awali akisoma risala ya wanafunzi kwa Rais Kikwete, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Boniface Juma, alisema wanaunga mkono mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuridhishwa na hatua iliyofikiwa.
 
“Mheshimiwa Rais, tunaridhishwa sana na hatua iliyofikiwa na Bunge Maalumu la Katiba, tunaamini kuwa mwafaka unawezekana kwa vipengele vingine vya Rasimu ya Katiba. Na imani yetu theluthi mbili za kupitisha Katiba Mpya inawezekana kupatikana,” alisema Juma.
 
TCD kuteta na JK
Wakati huo huo, taarifa kutoka Dodoma zinaeleza kuwa Ukawa watakutana wiki hii na Rais Kikwete kuzungumzia suluhu kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
 
Julai mwaka huu, Ukawa walikacha mazungumzo na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na hatimaye kugomea mchakato huo kwa kutohudhuria vikao vya Bunge hilo.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John Cheyo, alisema azimio la kutaka kuonana na Rais Kikwete ni baada ya mazungumzo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 23, mwaka huu na kuhudhuriwa na wenyeviti wa vyama vyote.
 
Cheyo alikataa kusema ajenda zitakazozungumzwa katika kikao hicho na Rais, lakini alisema jambo kubwa ni kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
 
Alisema kikao cha maazimio ya kukutana na Rais kiliwakilishwa na viongozi mbalimbali ambapo CCM, iliwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Kinana, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Makamu wake, Magdalena Sakaya na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
 
“Viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda TCD waliketi katika mkutano wa wakuu wa vyama ambapo kwa pamoja walijadili na kutafakari maendeleo ya mchakato wa Katiba mpya.
 
“Viongozi hao katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine, waliazimia kutafuta nafasi ya kuonana na Rais kwa lengo la kushauriana naye ambapo Rais amelipokea ombi hilo na ameahidi kuonana na viongozi hao mwisho wa wiki hii,” alisema Cheyo.
 
Hata hivyo, Cheyo, ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (UDP), alipoulizwa ni kitu gani wanakwenda kuzungumza na Rais wakati mchakato wa Katiba umefika mbali, na nini kimeonekana kimekwenda sivyo hadi kufikia hatua ya kuomba kukutana naye kwa mashauriano, alikataa kuzungumzia hilo.
 
Alisema ajenda za kikao hicho ni siri, na kwamba viongozi wa vyama, walikubaliana kutosema hadi pale mazungumzo hayo yatakapokwisha.
 
“Nimesema ni kuhusu mchakato wa Katiba, hayo mambo mengine mtajazia wenyewe, si mnayajua,” alisema Cheyo.
 
Katibu Ukawa anena
Akizungumzia uamuzi wa kukutana na Rais Kikwete, Katibu wa Ukawa ndani ya Bunge, Julius Mtatiro, alisema suala la maridhiano kwa nia ya kupatikana Katiba mpya ni jambo jema ambalo halina matatizo kwao.
 
“Sisi hatuna matatizo na kukutana na Rais na tunajua kuwa kuna utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa, hivyo endapo utashughulikiwa, tuko tayari kuonana na Rais ili tunusuru hali ya mvutano inayoendelea,” alisema Mtatiro.
 
Alisema kitendo cha Ukawa kususia mchakato huo ni kwa manufaa ya umma, kwani Katiba itakayoandikwa itakuwa ya Watanzania wote, hivyo ni vyema kuwa na Katiba ambayo itakubalika na wananchi.

No comments:

Post a Comment