Hatua
ya kwanza ya ndoto ya kuzama katika elimu ya mabinti pacha walioungana
kiwiliwili, Consolata na Maria Mwakikuti (18) wa Kijiji cha Ikonda
wilayani Makete mkoa mpya wa Njombe, inatarajiwa kutimia Novemba mwaka
huu, wakati mabinti hao watakapofanya mtihani wa kuhitimu kidato cha
nne.
Itakumbukwa
kwamba walipokuwa wakimaliza elimu ya msingi mwaka 2009 kijijini kwao
Ikonda, walikuwa na umri wa miaka 13 na katika ndoto zao kwa pamoja
walisema wanataka kuwa wasomi waliobobea katika utaalamu wa kompyuta.
Lakini, kwa sasa, wanasema wanatamani kufanya kazi ya Ukatibu Muhtasi.
Wanafunzi hao mwaka 2010 walichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani, Dar es Salaam.
Kwa sasa wanasoma katika Shule ya Sekondari ya Maria Consolata iliyopo Kidabaga wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Shule
hiyo inamilikiwa na Kituo cha Nyota ya Asubuhi ya Wamisionari
Wakatoliki wa Italia, kinachosaidia kuwatunza watoto wanaotoka katika
mazingira magumu.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hii shuleni hapo hivi karibuni, walisema
wanafurahi kuwa miongoni mwa watahiniwa watakaofanya mtihani huo wa
kidato cha nne mwaka huu.
"Tunafurahi,
tunajiandaa tunasoma kwa bidii, mtihani uko karibu tunataka tufaulu
vizuri masomo yetu, ili ile ndoto yetu ya kuwa Makatibu Muhtasi itimie,"
walisema Maria na Consolata, ambao wanatumia baiskeli maalumu kuwapeleka darasani, ambako pia wana kiti maalumu.
Pacha
hao wameshangaza watu wengi kwa jinsi walivyo, ambapo kila mmoja ana
madaftari yake. Wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa,
mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
"Wala
hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika
kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia," anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.
Shule
hiyo ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne. Ilianzishwa mwaka
2006 na hivi sasa ina jumla ya wanafunzi 183. Wote wanaishi kituoni
hapo na wote wanatoka kwenye mazingira magumu.
Changamoto
kubwa iliyokuwa shuleni hapo ni ukosefu wa nishati ya umeme, ambapo
uongozi wa shule na kituo hicho unalazimika kutumia jenereta na
umemejua, jambo ambalo mapema wiki hii Wakala wa Nishati ya Umeme
Vijijini (REA), imewaondolea adha kwa kuwapelekea umeme.
Pacha hao walizaliwa mwaka 1996 wakiwa wameungana katika Hospitali ya Ikonda wilayani Makete mkoani Iringa.
Walifaulu
mtihani wa darasa la saba mwaka 2010, ambapo kila mmoja alipata alama
151, ingawa walitofautiana ufaulu kwenye masomo yao.
Katika
somo la Maarifa ya Jamii, Consolata alipata alama 29 na Maria alama 25,
kwenye somo la Kiingereza, Maria alipata alama 36 na kumzidi Consolata
aliyepata alama 34, wakati kwenye somo la Sayansi, Maria alimzidi
Consolata kwa kupata alama 31 dhidi ya 29.
Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliwapanga pacha hao kujiunga na kidato
cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jangwani jijini Dar es Salaam.
Hata
hivyo hawakujiunga na sekondari hiyo, kutokana na hali yao na pia
umbali kutoka Iringa hadi Dar es Salaam. Ndipo Wamisionari hao
wakawachukua mwaka 2011 na kuanza kidato cha kwanza.
Walizaliwa
kwenye Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996. Lakini, taarifa zao
hazikufahamika hadi pale walipoandikishwa kuanza elimu ya msingi Ikonda
na kutafutiwa mlezi wa kuwaangalia, baada ya wazazi wao kufariki dunia
wakiwa bado wadogo.
No comments:
Post a Comment