Mtoto Happiness Rioba(10) aliyedaiwa kuzamia kwenye ndege kutoka
Dar es Salaam kwenda Zanzibar bila kugundulika, ametoweka tena nyumbani
kwao baada ya kukutanishwa na mama yake mzazi Sara Zefhania.
Happiness ambaye ni mkazi wa eneo la Mkokozi,
Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani inadaiwa ametoweka katika mazingira ya
kutatanisha.
Akizungumza na Mwananchi jana, Sara alisema
mwanawe alitoweka jana saa sita mchana na kutokomea
kusikojulikana.Alisema asubuhi mtoto wake aliamka salama bila tatizo
lolote na muda wote walikuwa pamoja kwa kuwa alikuwa na wageni kutoka
kituo cha televisheni cha ITV, waliomuahadi kumtembelea nyumbani kwa
lengo la kumuona Happiness.
“Aliamka vizuri tu na muda wote alikuwapo
nyumbani, lakini ilipofika saa sita mchana, nilipigiwa simu na waandishi
wa habari wa ITV kuwa nikawachukue katika kituo cha daladala... kabla
sijaondoka nilimwambia mwanangu nakwenda kupokea wageni, lakini
niporejea nyumbani na wageni hatukumkuta,” alisema Sara.
Alisema baada ya kumkosa alianza kumtafuta
akishirikiana na waandishi hao pamoja na majirani, lakini hawakufanikiwa
kumpata ndipo alipotoa taarifa kwa mjumbe wa Serikali za Mitaa na
kuwataarifu ndugu, jamaa na marafiki.
Aidha, aliongeza mwanawe alipokuwa Zanzibar
alifanya mambo ya ajabu likiwamo kuongea na paka, kula chakula kwa
kutumia mkono wa kushoto, kutokuongea na watu pamoja na kutoweka katika
mazingira ya kutatanisha.
Alifafanua kuwa walipofika nyumbani wakitokea
Zanzibar alianza kumdadisi kutaka kujua alifikaje huko na je kweli
alipanda ndege, alisema baba yake ndiye alimuita ili akaishi naye huko.
No comments:
Post a Comment