MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amekunjua
upya makucha yake yaliyowahi kurarua viongozi wenzake akiwa katika
NCCR-Mageuzi na TLP, na sasa amefukuza hadharani madiwani wawili wa
chama chake waliounga mkono nia ya Mbunge wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia,
ambaye ametangaza kugombea ubunge wa Vunjo.
Mrema amewavua uanachama wa TLP, Meja Mstaafu Jesse Makundi,
aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya Mrema; na Yorolanda Lyimo,
Diwani wa Kilema Kaskazini.
Jimbo hilo linawakilishwa na Mrema tangu 2010, na amesema mara kadhaa
kwamba hataki kusikia mtu akitaka ubunge katika jimbo lake. Tayari
amemlalamikia Mbatia kwa rais na katika Bunge Maalumu la Katiba.
Kilichowaponza Makundi na Lyimo ni kushiriki harambee iliyoongozwa na
Mbatia ya ujenzi wa maabara na mabweni katika shule za Sekondari za
Pakula, Kiluani na Mwika, mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika harambee hiyo, Makundi alisema anatambua uwezo wa Mbatia na
kwamba, kwa sababu hiyo, anamuunga mkono katika azima yake ya kuwa
mbunge mwakani.
Alisema kwa kuwa alipokea tochi ya kumulikia wana Vunjo kutoka kwa
Mbatia, ameona ni busara kuirudisha kwa yule aliyemkabidhi tochi hiyo.
“Leo nimefikia uamuzi ambao naamini ndio hitaji la wana Vunjo, kwa
kuwa Jimbo hili nililipokea kutoka kwa Mbatia na kwa kuwa yeye ndiye
aliyenikabidhi hii Tochi, natamka hadharani kuwa Mbatia ndiye chaguo
langu, yeye ndiye atakayemulika wana Vunjo,” alisema Makundi.
Yorolanda naye alidai kuwa uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni wa Mungu.
“Tunamuomba Mungu amuinue aweze kuwa Mbunge wetu. Mimi ni Diwani wa
TLP, nina Mbunge wangu, namuheshimu sana (Mrema), lakini namuomba Mungu
amteue Mbatia chaguo letu Wana Vunjo.
Nafahamu wapo watakaonukuu maneno
yangu lakini kama mbaya acha iwe mbaya,” alisema.
Mrema amekerwa na kauli hizo, akawavua uanachama akidai wameonyesha
utovu wa nidhamu na wamekiuka katiba ya chama chao kuunga mkono mtia nia
wa ubunge wa chama kingine, katika jimbo lake ambalo naye ameshatangaza
kuwania nafasi hiyo tena mwakani.
Alikuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye Kijiji cha Mwanjeni, Kata ya Mwika Kusini.
Hata hivyo, Makundi amesema uamuzi wa Mrema ni batili, kwani mwenyekiti wake huyo hana mamlaka hayo.
Mrema amekuwa analalamikia hatua ya Mbatia kutaka ubunge wa Vunjo,
akisema kinachomtia kiburi ni ubunge wa kuteuliwa aliopewa na Rais
Jakaya Kikwete.
Analaumu pia vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF vinavyounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambavyo vimetangaza kuweka mgombea mmoja
mmoja kila jimbo kwa ushirikiano.
Hata hivyo, UKAWA haijatangaza mgombea wa Vunjo. Licha ya Mbatia,
yupo mtia nia mwingine kutoka CHADEMA, John Mrema, ambaye naye
ameshatangaza kugombea ubunge huo, akisubiri uamuzi wa mwisho wa UKAWA.
Lakini Mrema amekuwa anamshambulia Mbatia kwa kuwa ndiye amekuwa anafanya mikutano ya mara kwa mara.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Tanzania Daima hivi karibuni,
Mbatia, malalamiko ya Mrema hayana msingi wowote, na kwamba hatajibizana
naye.
“Siko tayari kujibizana na mtu. Kuna kazi kubwa mbele yetu. Tuelekeze
nguvu zetu kuwatumikia Wana Vunjo. Mkutano wa Septemba ndio unaomtesa.
Nyinyi ni mashahidi. Tangu Septemba 6, sijafanya mkutano wowote.
Kulalamika kwake ni sawa na kulalamikia kivuli. Kivuli chake
kinamuhukumu. Mimi siko tayari kumjibu,” alisema Mbatia.
Kati ya 1995 na 2005, Mrema akiwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na
baadaye TLP, aliwahi kuthubutu kutimua viongozi wenzake kwa mtindo huo.
Miongoni mwao ni aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wake, Harold Jaffu na
Thomas Ngawaiya, ambao aliwaitia Kamati ya Utendaji na kuwashitaki kwa
kuwashitukiza, baada ya kugundua wamepunguza utii wao kwake.
Kabla ya hapo, alijaribu kufukuza Kamati Kuu ya NCCR-Mageuzi,
akiishitaki kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu kwamba kamati hiyo ilikuwa
haimsaidii kufanya kazi. Kati ya wajumbe 22 wa kamati hiyo, aliungwa
mkono na wajumbe saba tu.
Kamati Kuu, ikiongozwa na Mabere Marando, ilikataa kufukuzwa na
Mrema, na baadhi yao (Ndimara Tegambwage na Profesa Mwesiga Baregu)
wakamshauri ajiuluzu akagoma; kukazuka mtafaruku mkubwa ulioenea kwa
njia na sura mbalimbali, na hatimaye ukasambaratisha chama hicho.
Aliwahi pia kuthubutu kuwafukuza Balozi Paul Ndobho na Steven Wassira
aliokuwa nao NCCR-Mageuzi, akiwatuhumu kwamba walikuwa wanafanya njama
za kumwengua asigombee urais, walipokuwa wanamshawishi aliyekuwa Katibu
Mkuu wa CCM, Horace Kolimba (sasa hayati) ajiunge na NCCR-Mageuzi.
Baadaye Mrema alikimbilia TLP mwaka 1999, na kwa staili hii,
alifukuza viongozi wote wa Mkoa wa Kagera wa chama chake, siku
alipokwenda kumzika aliyekuwa mbunge pekee wa chama hicho wakati huo,
Phares Kabuye, wa Biharamulo Magharibi.
Sababu ya kuwafukuza ni kwamba waliunga mkono hoja ya upinzani kuweka
mgombea mmoja wa CHADEMA dhidi ya CCM katika uchaguzi mdogo.
Wajuzi wa siasa za Vunjo ndani ya TLP wanasema Makundi ndiye alikuwa
kisiki muhimu katika ngome ya kisiasa ya Mrema jimboni; na kwamba kwa
kuthubutu kumvua uanachama ni sawa na Mrema kuhatarisha ubunge wake,
mithili ya mtu anayekata tawi alilokalia.
No comments:
Post a Comment