Na Mathias Canal
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeanza mikutano yake ya
nchi nzima kama ilivyotangazwa na katibu mkuu wa chama hicho Dkt
Wilbroad Slaa, hivi karibuni alipozungumza na vyombo vya habari ofisini
kwake Jijini Dar es Salaam.
Chadema kimeridhia kufanya mikutano nchi nzima ambapo katika mkoa wa
Iringa mkutano huo ulianza jana katika viwanja vya Mlandege kwa
kuhutubiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu mwenyekiti wa
CHADEMA Prof Abdalla Safari
Akizungumza na mamia ya watu waliojitokeza katika mkutano huo ambao
imeelezwa kuwa haujawahi kutokea mkutano kuwa na wimbi la watu kama hao,
amesema kuwa ukombozi wa nchi ya Tanzania umetokana na damu ya
watanzania hivyo hakukuwa na sababu ya watanzania kuishi maisha ya
umasikini kama ilivyo kwa nchi kama hii yenye rasilimali nyingi ikiwa ni
pamoja na misitu, madini na ardhi ya kutosha.
Safari alisema kuwa wananchi wa Botswana wanafaidika na madini ya
nchi yao kwa serikali kukusanya 70% ya madini huku nchi kama Tanzania
ikichukua 5% ya madini, hivyo ni dhahiri kuwa Uwezo duni wa kufikiri kwa
viongozi wa Tanzania ndio sababu ya umasikini wa Watanzania na utajiri
wa wananchi wachache (Mafisadi).
"Pia nawaahidi kwamba UKAWA tumeridhia kusimamisha mgombea mmoja
kwenye uchaguzi kuanzia ngazi ya serikali za mtaa hadi Taifa, lakini
kubwa zaidi tunataraji kwenda mahakamani kuzuia mchakato wa katiba
kukusanya maoni ya wananchi" Alisema Safari
Hata hivyo Katibu mkuu wa CHADEMA Taifa, Dkt Wilbroad Slaa amesema
kuwa kuna daftari la mkazi linapita mtaani hivyo wananchi wanapaswa
kujiandikisha kwa wingi ili wawe na uwezo wa kupiga kura sambamba na
kujitokeza kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa.
"Mnapaswa kutambua kuwa siku 21 kabla ya kupiga kura ni muda wa
kujiandikisha hivyo kila mmoja ajiandikishe na kuhamasisha wengine,
nachukua nafasi hii kuwakumbusha kuwa uzembe wa wanachadema ndio ushindi
wa CCM" Alisema Slaa.
Slaa alisema kuwa CCM imeshindwa kutoa elimu bure kwa watanzania
kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu tangu waingie madarakani hivyo
wasitegemee kufanikiwa kwa kipindi kifupi kilichosalia.
Naye mbunge wa Jimbo la Iringa mjini Mch Peter Msigwa alijibu mapigo
ya Katibu mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana alipozuru Mkoani Iringa
hivi karibuni, alisema katibu huyo alitumia muda mwingi katika mkutano
wake kumzungumzia badala ya kuzungumzia maendeleo ya nchi.
"Nilishinda kwa ushindi mnono mwaka 2010 kwenye uchaguzi mkuu hivyo
nawaomba msikubali kupotoshwa na propaganda ya kwamba nilishinda baada
ya CCM kujichanganya, tuna mambo mengi ya kuzungumza lakini tutaendelea
kuonana mara kwa mara kwani muda wetu hautoshi, wapo waliosema mimi na
Chiku Abwao tuna ugomvi hivyo ni rahisi kukomboa Jimbo la Iringa Mjini,
hilo lisahaulike naamini mmemsikia wenyewe Chiku alichokisema"
Msigwa alisema kuwa kuhusu mfuko wa jimbo ameanza kupita kila Kata
ili kutoa ufafanuzi kwa kina kwa kile kilichofanyika hatimaye watanzania
kutopotoshwa na baadhi ya wanasiasa.
Kwa upande wake Salumu Mwalimu ambaye ni Naibu Katibu mkuu wa Chadema
Zanzibar amesema kuwa, Chadema kinaamini katika vijana ndio maana wengi
wao ni viongozi na ufanisi wa hoja unaonekana.
Mwalimu alitumia nafasi hiyo pia kumuomba ruhusa Katibu mkuu wa chama
hicho ili kurejea tena mkoani Iringa kabla ya uchaguzi wa serikali za
mitaa lengo ikiwa ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa
kujiandikisha na kujitokeza katika kuwania nafasi za serikali za mtaa.
Viongozi wengine waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na
Patrick Ole Sosopi Makamu Mwenyekiti BAVICHA Taifa sambamba na Chiku
Abwao Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa.
No comments:
Post a Comment