Wananchi wakiwa katika foleni ya kuingia katika ukumbi wa mdahalo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph
Warioba akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere kuhusu Katiba inayopendekezwa na kufanyika jijini Dar es Salaam.
Mwanaharakati wa mambo ya vijana Humphrey Polepole na aliyekuwa
mjumbe wa Tume ya mabadiliko ya katiba akzungumza katika mdahalo huo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph
Warioba akizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu
Nyerere kuhusu Katiba inayopendekezwa na kufanyika jijini Dar es Salaam.
Waliokuwa wajumbe Tume ya Mabadiliko ya Katiba wameendelea kuikosoa vikali Katiba inayopendekezwa na kusema kwamba haitakuwa na manufaa kwa Watanzania.
Kadhalika, wamesema Muungano uliopo kwa sasa upo katika hatari ya kuvunjika na kwamba hali hiyo itasababishwa na Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba (BMK).
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba (pichani), akizungumza katika mdahalo wa kujadili katiba inayopendekezwa uliofanyika ukumbi wa City jijini Dar es Salaam jana, alisema Katiba hiyo imeondoa matarajio ya wananchi waliotegemea kupata katiba ya kuwakomboa katika miaka mingine 50 ijayo.
Alisema Muungano umefika hapa ulipo, umetokana na kudra za Mwenyezi Mungu na hekima za viongozi waliopita kwa kuuendesha kwa hekima licha ya katiba hiyo kubeba changamoto lukuki.
“Mimi nimeshangaa kuona waheshimiwa hawa wananitukana na kunikashfu eti nimemsaliti Mwalimu Nyerere, wanadiriki kutumia nguvu na maneno ya kashfa kupitisha katiba. Katiba haiwezi kupitishwa kwa namna hiyo, katiba ni maridhiano ambayo pia yanashirikisha maoni ya wananchi,” alisema Warioba na kuongeza:“Hata kama Nyerere angelikuwapo leo angeipinga Katiba hii inayopendekezwa.”
Warioba alisema hata kama wataipitisha kwa nguvu, lakini wanatakiwa kufahamu kuwa italeta matatizo baadaye na ni vizuri wafahamu kuwa hata kama itapita itakuwa na matatizo.
Humphrey Polepole, aliitaka serikali kusambaza Katiba inayopendekezwa pamoja na rasimu ya Tume hiyo kwa wananchi ili waisome na kuielewa kabla ya kuipigia kura ya maoni.
Kuhusiana na suala la elimu ya wabunge, alisisitiza kuwa ni vema wabunge wawe na elimu ya kidato cha nne, tofauti na katiba inayopendekezwa inayowataka wawe wanajua tu kusoma na kuandika.
Alisema endapo Katiba itapitishwa kama ilivyo kwamba wabunge wajue kusoma na kuandika pekee, itamuwia vigumu rais kupata mawaziri wenye elimu ya kutosha ya kusimamia shughuli za maendeleo ya nchi.
“Unawezaje kusema wabunge wawe wanajua kusoma na kuandika tu, isipokuwa mawaziri, je, wakichaguliwa wabunge wote ambao uwezo wao ni wa kusoma na kuandika tu, hao mawaziri watatoka wapi na shughuli za maendeleo wataendeshaje?” alihoji Polepole.
Kadhalika, alisema kuwa anashangaa mawaziri kuipigia chapuo Katiba inayopendekezwa na kuipinga serikali tatu, wakati hata wao walitoa maoni wakiitaka muundo wa serikali hizo.
“Mimi nilishiriki katika kikao cha kukusanya maoni ya mawaziri, walipendekeza serikali tatu, na hata baadhi ya mawaziri wakuu nao walipendekeza serikali hizo, na wasitake tufikie huko wanakotaka, wakibisha tunaweza kuwataja,” alisema huku walioshiriki mdahalo huo wakitaka awataje.
Kwa upande wake, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Katiba inayopendekezwa ni dalili ya kuvunjika kwa Muungano.
“Nilishangaa sana kuona wajumbe wa lililokuwa Bunge Maaluma la Katiba kufanya sherehe na marais kusherehekea malengo ambayo yameshindwa kufikiwa katika katiba inayopendekezwa, ambayo wananchi wakiisikia wanapata uchungu,” alisema Profesa Baregu.
Aliongeza: “Dalili inavyoonekana hivi sasa Katiba hiyo ndiyo itakuwa chanzo cha kuvunja Muungano huo na tutegemee, huko ndiyo tunakokwenda.”
Mohamed Mshamba, ambaye naye alikuwa mjumbe wa Tume ya Katiba, alisema Tume ilikusanya maoni ambayo yalilenga kulipatia taifa katiba bora, lakini lengo hilo limevurugwa baada ya kuondolewa vifungu vya msingi.
Mdahalo huo ulitawaliwa na ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi ambao walikagua kila alieingia katika ukumbi huo kwa kutumia vifaa maalum vya ukaguzi.
Pia, ndani ya ukumbi kulikuwapo na utulivu, tofauti na ilivyokuwa katika mdahalo uliopita ambao baadhi ya watu waliumia kutokana na vurugu zilizosababishwa na kikundi cha watu walisadikika kutoka Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapindiuzi (UVCCM).
Kutokana na idadi kubwa ya watu waliojitokeza katika mdahalo wa jana, ukumbi huo ulijaa na kupelekea polisi kuwazuia baadhi ya watu kuingia ndani kutokana na kukosekana na nafasi.
Hali hiyo ilisababisha askari polisi kupata changamoto ya kuwaelewesha wananchi hao ambao hawakutaka kukubali kubaki nje.
No comments:
Post a Comment