Wakati Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakichachamaa wakisema
hawatakubali Bunge hilo kuingiliwa na mhimili wa Mahakama, Mahakama hiyo
imejiweka kando na tuhuma hizo.
Sakata hilo lililotawala kikao cha Bunge hilo jana lilitokana na madai
yaliyoibuliwa juzi na wabunge wa kupinzani unaoundwa na vyama vya CUF,
Chadema na NCCR-Mageuzi.
Wabunge hao Tundu Lissu (Chadema), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Habib
Mnyaa (CUF) waliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma juzi kuwa
wamepata taarifa za uhakika kuwa Mahakama imeandika barua ikiritaarifu
Bunge lisijadili kashfa ya uchotaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka
akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania.
Wabunge hao, walisema kuwa hatua hiyo ni kuingilia uhuru wa mhimili wa
Bunge na kwamba lengo lake ni kutaka kukwamisha ripoti ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili wahusika wasichukuliwe
hatua.
Msajili wa Mahakama Kuu, Amir Msumi, alipotakiwa kuthibitisha kama Mahakama imeandika barua hiyo kwenda Ofisi ya Spika wa
Bunge kuzuia suala hilo lisijadiliwe kwa kuwa kiko mahakamani, alisema
yeye na wasajili wenzake hawana taarifa kuhusu kuandikwa kwa barua hiyo.
“Labda unieleze hiyo barua imeandikwa na nani na lini, kama ni Jaji au
Msajili nitajie jina lake ili iwe rahisi kufuatilia, lakini hadi sasa
nimepekua kwenye kumbukumbu zetu sijaona barua hiyo,” alisema Msumi.
Aliahidi kwamba jana angewasiliana na wenzake wa Mahakma ya Rufani kama
kuna barua imeandikwa kutoka mahakama hiyo kwenda bungeni.
Hadi sasa hakuna mamlaka yoyote ya serikali iliyothibitisha rasmi kama
kuna barua iliyoandikwa na Mahakama kwenda Ofisi ya Spika wa Bunge.
Juzi Naibu Spika,Job Ndugai, alisema kuwa ofisi ya Spika haijapokea barua hiyo.
Hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakati akizungumza bungeni jana
kuhusiana na madai hayo, hakuthibitisha wala kukanusha kama kuna barua
iliyoandikwa na Mahakama kwenda bungeni kuzuia mjadala huo, zaidi ya
kusisitiza itumike busara ili kuepusha mihimili hiyo kuingiliana katika
majukumu yao kwa mujibu wa Katiba ya nchi.
Chanzo: Nipashe
No comments:
Post a Comment