Thursday, November 20, 2014

WAKULIMA BAGAMOYO WASIFIA MBEGU MPYA ZA MIHOGO.




Wakati tafiti mbalimbali zikiendelea kufanyika katika kituo cha utafiti cha MARI (Mikocheni Agricultural Research Institute)ili kulikomboa zao la Mhogo kutoka katika janga la magonjwa yaliyolikumba zao hilo,  wakulima wamendelea kusifia mbegu mpya ambazo zinaendelea kutolewa na kituo hicho kwa sasa
 Sambamba na hilo, wakulima wa mihogo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamesifia ubora wa  mbegu mpya ya mihogo itokayo MARI kuwa ni mbegu bora, ikomaayo haraka, isiyo na magonjwa na pia inazaa sana tofauti na mbegu za zamani.
Wakiongea na mwandishi kwa nyakati tofauti walisema mbegu walizokuwa wakizilima hapo awali zilikuwa ni pamoja na Jota ambayo ilikuwa inakuwa ni ndefu  na inalewesha sana ukila kwa wingi, Mzungu, yenyewe ni nyekundu kwa muonekano ambayo pia hulewesha, mbegu ya Kiruthungu na Kinyafu ambazo zenyewe ni michungu sana iliwapo. Pia walisema mbegu hizi zilikuwa zinachukua mda wa miezi minne hadi mitano kukomaa kitu ambacho ni tofauti na mbegu ya sasa.
 
Walisema kuwa mbegu za sasa wamezipa majina ya Mwanamtwa, Mzuri kuonja, Kibangameno, Magimbi na kilokote, huku wakizingatia radha na uzuri wa mbegu hiyo.
Wakitofautisha mbegu mpya  walisema mbeguu mpya zote si chungu kwa kula, hukomaa ndani ya miezi mitatu mpaka mine na huzaa mihogo mikubwa kitu ambacho ni tofauti na za zamani.
“Mihogo ya siku hizi ni mitamu hata kwa kutafuna ikiwa mibichi tofauti na ile mingine ni michungu, na pia ukiipika inaunga sana mpaka inavutia wakati wa kula” alisema Ibrahim Ramadhani
Hata hivyo wananchi hao wameiomba serikali kuanzisha vipindi na majarida yanayotoa elimu ya kilimo katika vituo vya redio mbalimbali na magazeti kwani bila elimu watu wengi hufanya  tofauti na baadae kulaumu kilimo pale wanapopata hasara shambani.
“Serikali inatakiwa kurudisha vipindi vya kilimo kwani wameziacha redio zinapiga mziki asubuhi hadi asubuhi hakuna faida badala yake vijana wanaacha kufanya kazi na kukaa vijiweni kusikiliza miziki. Inatakiwa wawaambie wenye vituo vya redio kuwa na vipindi vya kilimo ili kuwabadirisha vijana wanaosubiri ajira maofisini wajue kuwa hata kilimo ni ofisi kama ofisi zingine” alisema mzee Frank Shaban.
Wakati huo huo mwandishi aliwasihi wakulima hoa kutunza mbegu hizo kwani mbegu walizopewa ni mbegu zisizokuwa na magonjwa hivyo wanatakiwa kutunza vizuri ili kupata mazao mazuri na bora kwa manufaa zaidi.
Ikumbukwe kuwa zao la muhogo lilikumbwa na magonjwa ya mnyauko fuzari pamoja na batobato ambayo yalisababisha zao hili kuwa hatarini kutoweka kitu ambacho kiliwafanya watafiti kuingia maabala na kutafuta ufumbuzi ili kukomboa mikoa inayotegemea zao la mihogo kwa chakula.
Mpaka sasa njia pekee inayotumika kuzalisha mihogo isiyokuwa na magonjwa ni tissueculturee (uzalishaji wa chupa) na njia hii haiufanyi mmea kuwa kinzani na magonjwa hivyo njia pekee ya kufanya mbegu mpya kudumu na kuzaa vizuri ni mkulima kutunza vizuri shamba lake ili kupata faida.

No comments:

Post a Comment