KUNA kila
dalili za Baraza la Mawaziri la Serikali ya Rais Jakaya Kikwete
kuvunjika tena baada ya ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kashfa ya uchotwaji fedha zaidi ya sh.
bilioni 200, kwenye akaunti ya Tegeta Escrow zilizohifadhiwa katika
Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kubainisha kuwa fedha hizo zilitolewa
kinyume na taratibu.
Kashfa hii
nzito ni mfululizo wa nyingi zilizotokea chini ya utawala wa Rais
Kikwete na hivyo kusababisha mawaziri kadhaa kuachia ngazi akiwemo
aliyekuwa Waziri wake Mkuu, Edward Lowassa aliyejiuzulu Februari 7,
mwaka 2008, kufuatia kashfa ya zabuni tata kwa kampuni hewa ya kufua
umeme ya Richmond.
Vigogo wa
serikali wanaotajwa kuhusika katika kashfa hii ni Waziri wa Nishati na
Madini, Prof. Sospiter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi,
Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof.Beno
Ndullu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema na
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Wadadisi wa
kisiasa wanabashiri kwamba kashfa hii huenda ikiwa mwiba wa kuking’oa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015,
ikiwa vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
vitadumu katika muungano wao na kuwaeleimisha wananchi madhara ya
ufisadi huo.
Kashfa kama
hii iliwahi kuking’oa chama tawala cha KANU cha nchini Kenya mwaka 2002,
ambapo kwa mujibu wa taarifa zilizopo, mmiliki wa Kampuni ya PAP
inayodai kuinunua Kampuni ya IPTL, Habinder Singh Sethi, anatajwa
kuhusika katika kashfa kubwa ya ufisadi nchini Kenya ya Goldenberg,
uliogharimu takribani dola milioni 600.
Ufisadi huo
pia ulihusisha mahakama, watendaji, viongozi na wanasiasa wakubwa nchini
humo, ikiwemo familia ya aliyekuwa Rais wa wakati huo, Daniel Arap Moi,
ambapo katika uchaguzi mkuu wa 2002, vyama vya upinzani kupitia
muungano wao wa National Alliance of Rainbow Coalition (NARC) chini ya
mgombea wake Mwai Kibaki, kwa kutumia kashfa hiyo, vilifanikiwa
kuking’oa Chama tawala cha KANU.
Kwa mujibu
wa ripoti ya CAG ambayo imekabidhiwa kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC) kwa ajili ya kuipitia na kuwahoji watuhumiwa, fedha za
Escrow sh. bilioni 306 ni matokeo ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco)
kulipishwa capacity charge zaidi ya kiwango kinachotakiwa kulipwa.
Ripoti hiyo,
inasema kwamba Tanesco walipaswa kurejeshewa sh. bilioni 321
zilizolipwa zaidi kwa IPTL kati ya mwaka 2002 hadi 2012. Kwa maana hiyo,
Escrow ni fedha za umma. Hii ni kinyume na kauli zilizokuwa zikitolewa
na viongozi mbalimbali wa serikali ya Rais Kikwete wakiwemo Waziri Mkuu,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Nishati na Madini kwamba
fedha hizo ni za mmiliki wa Kampuni ya IPTL.
Kwa mara
kadhaa, Waziri Muhongo amenukuriwa na vyombo vya habari akitamba na
kuwabeza wabunge waliosimama kidete kuhakikisha fedha za Escrow
zinarejeshwa, akidai kwamba ushahidi waliowasilisha bungeni kwa Spika wa
Bunge, Anne Makinda kuonesha kwamba fedha hizo ni za umma, ni
vipeperushi feki kwani yeye anao ushahidi wa makaratasi ya kujaza gari
zima la tani moja kuthibitisha kuwa fedha hizo sio za umma.
Waziri
Muhongo na Katibu wake, Maswi wamekuwa wakiwatuhumu wabunge David
Kafulila wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi) na Zitto Kabwe wa Kigoma
Kaskazini (CHADEMA) kwamba wamehongwa na aliyekuwa Mwanasheria wa
Tanesco, Nimrod Mkono kushupalia sakata hilo ili kukwamisha bajeti ya
wizara hiyo ya 2014/2015.
Kashfa ya
Escrow imeghubikwa na utata ambapo Harbinder Sing Sethi, anadai alinunua
asilimia 70 ya hisa za Mechmar kwa kiasi cha sh. milioni 500 ($300,000)
ndani ya wiki tatu tu tangu hisa hizo kuuzwa kwa kampuni moja ya Visiwa
vya Uingereza vya Virgin kwa sh. milioni sita.
Lakini barua
ya TRA Mkoa wa Ilala, iliyosainiwa na Meneja, Paschal Kabunduguru,
yenye kumbukumbu nambari TRA/DR/ILA/RE/175 ya tarehe 15/11/2013,
inaonyesha kuwa kampuni ya Mechmar ya Malaysia iliuza hisa zake asilimia
70 katika kampuni ya IPTL kwa kampuni ya Piper Links investment limited
mnamo tarehe 9/9/2013 kwa thamani ya sh. 6,000,000 (milioni sita).
Nyaraka za
malipo ya kodi kwa mujibu wa barua hiyo inaonyesha Mechmar walilipa kodi
ya ongezeko la mtaji sh. 596,000 na kodi ya stempu ya sh. 180,000 mnamo
tarehe 6 Disemba 2013 katika Benki ya CRDB Tawi la Waterfront.
Katika hali
inayotia mashaka, kampuni ya Piper Links nayo, kwa mujibu wa nyaraka
toka TRA, ikauza hisa zake kwa Kampuni ya Pan Africa Power Solutions
mnamo tarehe 30 Oktoba, 2013, takribani wiki tatu tangu kununuliwa kwa
hisa hizo toka kwa Mechmar.
Kwa mujibu wa barua ya TRA, kodi iliyolipwa ni ya ongezeko la mtaji sh. 47,940,000 na ushuru wa stempu sh. 4,800,000.
Malipo ya
kodi hiyo yalilipwa siku ile ile ambayo Mechmar walilipa yaani Disemba
6, 2013, jambo linalozidi kuzua utata mkubwa kuhusu mhamala huo.
Pengine
kinachotia shaka zaidi ni kwamba nyaraka zote mbili toka TRA ziliandikwa
siku moja, na zote zina kumbukumbu namba zinazofanana licha ya ukweli
kwamba zilikuwa zinakwenda kwa makampuni mawili tofauti, moja ikiwa
Malayasia, na nyingine ikiwa visiwa vya Uingereza vya Virgin.
Pia nyaraka
hizi toka TRA, zinapingana na kauli ya Sethi ambaye amenukuliwa na
vyombo kadhaa vya habari akidai kwamba alinunua hisa asilimia sabini za
Mechmar mwaka 2010, toka kampuni ya Piper Link—mwaka mmoja kabla ya PAP
kuanzishwa.
Wachambuzi
wa masuala ya kiuchumi wanasema kwa mujibu wa Sheria ya kodi ya Mapato
ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho katika Sheria ya Fedha ya
mwaka 2012, mauzo yeyote ya hisa au mali ambazo zipo Tanzania mauzo yake
lazima yathibitishwe na Wizara husika baada ya kodi zote kulipwa.
Nyaraka hizi
zinaonesha kuwa mauzo ya IPTL kutoka Mechmar kwenda PiperLink na kutoka
PiperLink kwenda PAP yote yamelipiwa kodi siku moja tena baada ya
malipo ya fedha za Escrow kwenda PAP Disemba 5, 2013.
Kwa
kuzingatia nyaraka hizo, ni dhahiri kuwa mpaka kampuni ya PAP ilipokuwa
inalipwa fedha za Escrow hawakuwa na umiliki wa hisa za IPTL. Hata amri
ya mahakama ilipotolewa kuwa PAP wapewe mali za IPTL, kampuni hiyo
haikuwa na umiliki wa wowote wa IPTL.
Pia katika
hati za kuhamisha hisa ambazo ziliidhinishwa na TRA mkoa wa Ilala,
mwandiko ulipo unafanana sana na mwandiko wa nyaraka za malipo ya kodi,
CRDB, tawi la Water Front—jambo linaloonyesha kwamba mtu mmoja huyo huyo
ndiye aliyeandika nyaraka zote hizi.
Utata
mwingine ni kuwa iweje kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa na hisa
asilimia 30 katika IPTL ilipwe dola za Kimarekani milioni 75 wakati
Mechmar iuze asilimia 70 kwa sh. milioni 6 tu na PiperLink iuze kwa dola
laki tatu tu ndani ya wiki tatu.
Serikali
kupitia kwa Mwanasheria Mkuu wake, Jaji Fredrick Werema, Waziri wa
Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliachim
Maswi, wamekuwa wakisisitiza kwamba fedha hizo zilitolewa kwa kuzingatia
hukumu ya MahakamaKuu.
Hukumu hiyo
ya Jaji John Utamwa inapingwa na Kafulila na wadau wengine kuwa
imetafsiriwa visivyo, kwani hakuna popote alipotaja Akaunti ya Escrow,
ingawa katika muhtasari wa kikao kati ya Tanesco, IPTL na Wizara ya
Nishati na Madini, ndipo wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba
fedha zote za akaunti hiyo zipewe Kampuniya PAP.
Kupitia
barua kumb. No. SAB.88/417/01/5 ya Oktoba 21, 2013, Katibu Mkuu wa
Nishati na Madini Maswi alimwandikia Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania
(BoT), Prof. Benno Ndulu akimtaka aruhusu fedha hizo katika Akaunti ya
Tegeta Escrow.
Hata hivyo,
sehemu ya ripoti ya CAG kuhusu kashfa ya uchotwaji wa fedha hizo
inathibitisha kuwa TRA walibaini kuwa msingi wa ukokotoaji wa kiwango
cha kulipa kodi ya Ongezeko la Mtaji ulitokana na nyaraka zenye taarifa
zisizo sahihi, jambo lililochangia kutolipwa kodi ya kiasi cha sh.
8,682, 521,100.
Utawala wa
Rais Kikwete umeghubikwa na kashfa nzito za ufisadi na ukiukwaji wa haki
za binadamu kwa kipindi chote cha miaka tisa, lakini mara zote kumekuwa
na kigugumizi cha kuwang’oa watuhumiwa mpaka pale Bunge lilipoingilia
kati.
Kashfa
zilizotikisa ni ile ya ununuzi wa rada mbovu kwa gharama kubwa hadi
serikali ya Uingereza ikaingilia kati kushinikiza kampuni iliyouza rada
hiyo irudishe chenji kwa Tanzania, pia ipo ile ya EPA iliyoaiandama
serikali mwanzoni mwa utawala wa Kikwete ambapo baadaye aliyekuwa Gavana
wa BoT, Daud Balali alifariki bila kuchukuliwa hatua.
Sakata
lingine ni kampuni hewa ya Richmond mwaka 2008, ambapo mbali na Lowassa,
mawaziri wengine waliong’oka ni Dk. Ibrahim Msabaha na Nasir Karamagi
waliopata kuwa mawaziri wa Wizara ya Nishati na baadaye Baraza la
Mawaziri lilivunjwa na kuundwa upya kwa Mizengo Pinda kuteuliwa kushika
wadhifa wa Waziri Mkuu ambaye naye kashfa ya Escrow huenda ikamwondoa.
Zipo pia
kashfa za uchangishaji fedha kinyume cha taratibu ndani ya Wizara ya
Nishati na Madini iliyomhusu aliyekuwa Katibu Mkuu wake, David Jairo na
kisha uchotwaji wa fedha uliyoihusisha kampuni ya Pan African Energy
zaidi ya sh. bilioni 110, tuhuma ambazo ziliwangoa Jairo na Waziri wake,
William Ngeleja.
Kashfa ya
Buzwagi nayo ilitikisa Bunge mwaka 2007, ambapo Zitto alimtuhumu Waziri
wa Nishati na Madini, Karamagi kuwa alikiuka utaratibu kwa kusaini
mkataba mbovu wa mgodi huo ikiwa hotelini nje ya nchi. Hata hivyo CCM
kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilimgeuzia Zitto kibao na
kumwadhibu kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge.
Pia zipo
kashfa za ripoti ya CAG mwaka 2012 na ripoti ya Kamati Teule ya Bunge
kuhusu utekelezaji wa oparesheni tokomeza mwaka 2013, ambapo mawaziri
Dk. Cyril Chami, Dk. Hadji Mponda, Omary Nundu, Mustafa Mkulo, Ezekiel
Maige, Dk. Athuman Mfutakamba, Dk. Lucy Nkya, Balozi Khamis Kagasheki,
Dk. Emmanuel Nchimbi, Shamsi Vuai Nahodha na Dk. Mathayo David
waling’oka kufuatia shinikizo la Bunge.
Wabunge CCM wakamia
Wakati PAC
leo ikianza kumhoji Jaji Werema kuhusu kashfa hiyo, wabunge wa CCM
wanatarajia kuwa na kikao maalum kwa ajili ya kujadili sakata hilo kabla
halijaingia bungeni Novemba 27.
Kashfa hiyo,
itabiriwa kwamba huenda ikamwangusha Waziri Mkuu, Pinda, kutokana na
wabunge wanaomuunga mkono Lowassa kujipanga kulipa kisasi cha yale ya
Richmond ya mwaka 2008.
Makamu
Mwenyekiti wa PAC, Deo Filikunjombe alilieleza gazeti hili kuwa kamati
yao imeshaanza kazi tangu jana, lakini leo itaanza kuhoji Jaji Werema
ambaye ni mmoja wa watuhumiwa.
Mwingine
atakayehojiwa ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na itaendelea na kazi yake kwa kuwahoji watu wengine kadri
itakavyoona inafaa.
Habari zaidi
kuhusu kamati hiyo iyopiga kambi nje ya viwanja vya Bunge, zinasema
kuwa itafanyakazi usiku na mchana na kukamilisha kazi yake ndani ya siku
tatu.
Kamati hiyo
inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA),
ilikabidhiwa ripoti hiyo juzi na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Mmoja wa
wabunge kutoka CCM, aliliambia gazeti hili kuwa tayari wameshajulishwa
kuwapo kwa kikao hicho kitakachofanyika siku yoyote wiki hii.
“Tutakuwa na
kikao wiki hii, sijui wanataka kutuambia nini. Kama kuwatetea
watuhumiwa itakuwa ngumu kwa sababu taarifa ya CAG inaonyesha wazi
kwamba Waziri Muhongo, Katibu Mkuu, Maswi na wengine waliotajwa
kuhusika, hawaponi. Sisi tutakuwa na nguvu gani kuwatetea? Alihoji.
Wabunge
wengi bila kujali vyama vyao, wamepania sana mjadala huo na kulitaka
Bunge litenge muda wa kutosha ili kila mchangiaji apate muda wa kutosha.
Mbunge wa
Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), jana aliomba mwongozo wa Spika kutaka
Bunge litenge zaidi ya siku moja ya mjadala wa kashfa hiyo ya IPTL.
Alisema kwa
jinsi hali ilivyo, inaonyesha kuwa wabunge wengi wanataka kuchangia,
hivyo aliomba mwongozo wa Spika ili Bunge liongeze muda zaidi wa
kuchangia.
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema anachukua mawazo hayo na kuyapeleka kwenye Kamati ya Uongozi ili waweze kufanya uamuzi.
CREDIT: TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment