Thursday, August 14, 2014

HATIMAYE YULE TRAFIKI FEKI APELEKWA MAHAKAMANI



MKAZI wa Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Robinson Mwakyusa (30), amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashitaka ya kujifanya askari wa Kikosi cha Usalama barabarani na kukutwa na vifaa vya Jeshi la Polisi.
 
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, alimsomea mshitakiwa mashtaka matatu mbele ya Hakimu, Devotha Kisoka na kusema kuwa  kabla Mwakyusa  kuachishwa kazi alikuwa ni askari mwenye namba F 2460,

Katika kosa la Kwanza, Kambakono alidai kuwa Agosti 2, mwaka huu, katika maeneo ya Chamazi Muhimbili, Wilaya ya Temeke, mshitakiwa alijitambulisha isivyo halali kwamba ni mwajiriwa wa sekta ya umma  kitengo cha jeshi la polisi Tanzania na kwamba ni ofisa wa Kikosi cha Usalama barabarani akiwa na cheo cha Stafu Sajini.

Alisema katika shitaka la pili, siku hiyo hiyo ya Agosti 2, katika Kituo cha Polisi cha Mbagala, wilaya ya  Temeke, mshtakiwa alikutwa na sare za polisi wa kikosi cha usalama barabarani, simu ya upepo aina ya Motorola GP 380 pamoja na beji iliyoandikwa ER Mwakyusa kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa alikutwa na vitu hivyo ambavyo ni mali ya jeshi la polisi, vinavyosadikiwa kuibwa au kupatikana isivyo halali.

Katika shitaka la tatu, mshitakiwa anadaiwa kukutwa maeneo ya Kijitonyama Mpakani B, wilaya ya Kinondoni, akiwa na nguo nne za kazi ya polisi, ambazo ni suruali tatu na mashati ya trafiki, koti moja la mvua la polisi, vikoti vinane vya trafiki vyenye mwanga, kofia ya trafiki ya Uhuru, bareti na mikanda minne mali ya jeshi hilo, ambavyo vinasadikiwa vimeibwa au kupatikana kwa njia isiyo halali.

Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na mwendesha mashtaka alidai upelelezi haujakamilika hali iliyomfanya hakimu Devotha kutoa masharti ya dhamana ambapo ni mshitakiwa kutia saini saini bondi ya sh. milioni 50 na awe na wadhamini wawili ambao nao watatia saini bondi hiyo kila mmoja.

Mshitakiwa alitimiza masharti ya dhamana na kuachiwa hadi Septemba mosi, mwaka huu, kesi itakapotajwa.

No comments:

Post a Comment