Aliyekuwa
Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Charles Ekelege
amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwenda jela miaka mitatu
na kuilipa serikali Dola 42,543 za Kimarekani, baada ya kupatikana na
hatia ya makosa matatu ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa
asilimia 50.
Kadhalika,
Ekelege anadaiwa kutoa asilimi hiyo ya punguzo la tozo ya utawala kwa
Kampuni mbili Kampuni ya Jaffar Mohamed Ali Garage na Kampuni Quality
Motors na kulisababishia shirika hilo hasara ya dola hizo.
Hukumu
hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi Augustina Mmbando baada ya kupitia
ushahidi wa pande zote mbili na mahakama yake kumuona mshtakiwa bila
kuacha shaka ana hatia.
Hakimu
alisema ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ulieleza mahakama
kwamba mshtakiwa kupitia wadhifa wake alifanya maamuzi bila kinyume na
sheria za TBS zinazomwelekeza kuwasilisha masuala yote ya kiutendaji
kwenye Bodi ya Wakurugenzi.
Alisema
kitendo cha kutoa msamaha kwa kampuni hizo bila kuacha shaka moja kwa
moja mahakama imeona alitumia madaraka yake vibaya.
“Kwa
upande wa shitaka la pili, kiongozi yeyote katika Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania anapokuwa madarakani ni kwa ajili ya maslahi ya
taifa, lakini mshtakiwa alikosa uzalendo na kutumia madaraka yake vibaya
kuhujumu uchumi” alifafanua hakimu kuhusu ushahidi wa Jamhuri.
“Mahakama
inamuona mshtakiwa ana hatia katika kosa hili la pili la kujumu uchumi …
pia mshtakiwa amesababisha watanzania waliompa dhamana kukosa kula keki
ya taifa lao kwa kujinufaisha yeye binafsi” alisema hakimu huyo na
kuongeza kuwa.
“Katika
ushahidi uliotolewa na mshtakiwa alikiri kufanya maamuzi bila kupata
baraka na kibali cha Bodi ya Wakurugenzi na kwamba aliidanyanya
mahakama” alisema Hakimu Mmbando.
Akifafanua
zaidi alisema mshtakiwa alidai kuwa katika kutoa maamuzi pinguzo kwa
kampuni hizo alishirikisha menejimenti na kwamba shirika lilikuwa na
utaratibu wa kufanya kikao kila siku asubuhi.
Hata
hivyo, shahidi wa pili wa utetezi Thomas Mlugulu alishindwa kuieleza
mahakama wajumbe waliokuwa wakihudhuria kikao cha cha asubuhi cha
shirika kwa kila siku zaidi ya kumtaja Betwel Matemba ambaye alishakufa
na hawezi kufika mahakamani.
Alisema
ushahidi wa utetezi ulikuwa dhaifu kushindwa kukanusha ushahidi wa
Jamhuri ulioweza kuithibitishia mahakama ukweli kuhusu mashitaka
yanayomkabili Ekerege.
Hakimu
alisema mahakama pia inamtia hatia mshtakiwa kwa shitaka la tatu la
kuisababishia serikali hasara ya dola hizo na kuwasababishia watanzania
kukosa kula keki ya taifa lao.
Hakimu Mmbando alitoa nafasi kwa mawakili wa pande zote mbili kutoa hoja kabla ya kusoma adhabu.
Mwendesha
Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Janeth Machulya, alidai kuwa kulingana na makosa aliyotiwa hatiani
mshtakiwa kwamba alipewa dhamana na rais pamoja na watanzania lakini
aameshindwa kuwa mzalendo.
“Kwa
kuwa mshtakiwa ameshindwa kuwa mzalendo kwa mamlaka aliyopewa na
wananchi, tunaomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa vigogo
wote wanaopewa madakara na kuyatumia vibaya,” alidai na kuongeza.
“Mheshimiwa
kwa kosa la uhujumu uchumi mahakama izingatiee utoaji wa adhabu
kulingana na sheria ya kosa hilo inavyoelekeza” alisema Machulya
aliyeongoza mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo na mahakama kumtia
hatiani kigogo huyo.
Wakili wa utetezi Majura Magafu alidai kuwa mahakama imuonee huruma mshtakiwa kwa sababu ana familia inamtegemea.
Pia, wakili huyo alidai kuwa mshtakiwa anajutia makosa aliyofanya na kwamba akipewa nafasi hawezi kurudia.
Hukumu hiyo iliyoanza kusomwa saa 6:20 mchana hadi saa 8:10 hakimu aliahirisha kwa nusu saa kabla ya kusoma adhabu.
Saa 8:49 mahakama iliyoketi chini Hakimu Mmbando ilianza shughuli zake.
Akisoma
adhabu hiyo, hakimu alisema Viongozi wote wa serikali wako juu kwa
ajili ya kulinda maslahi ya taifa ili kulinda na kuangalia nchi na mali
zake, siyo kuongoza kwa matakwa ya kiongozi husika.
“Mshtakiwa
unastahili kuhukumiwa ili kuwa mfano kwa viongozi wengine wanaochezea
keki ya taifa hili kwa manufaa yao binafsi… unakwenda jela mwaka mmoja
kwa kosa la kwanza, mwaka mmoja kwa kosa la pili na mmoja mwingine kwa
kosa la tatu na ailipe serikali fedha alizoisababisha hasara” alisema
Hakimu Mmbando.
Baada ya hukumu kusomwa;
Mshtakiwa
alianza kububujikwa na machozi huku watu wanaodaiwa kuwa familia yake
wakiangua vilio kwa sauti wakati mpendwa wao akiwa chini ya ulinzi
tayari kwenda gerezani kuanza kutumikia kifungo.
Watu
mbalimbali waliokuwa katika viunga vya mahakama hiyo walimzunguka
mshtakiwa huyo huku kila mmoja akisema lwake’jamani jela ni jela’
wengine ‘tatizo hizo fedha alizoambiwa alipe anazo au alishakula zote’
walisikika wakizunguma.
Mapema
Mwaka 2012, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami
aliondolewa katika wadhifa huo kutokana na kashfa ya kutoa punguzo la
tozo na baadaye Mei 21, mwaka 2012, mshtakiwa alisimamishwa kazi kama
Mkurugenzi wa TBS ili kupisha uchunguzi na hatimaye jana kuhumiwa.
Katika
kesi ya msingi, Ekelege anadaiwa kuwa kufanya matumizi mabaya ya
madaraka kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la tozo ya utawala kwa kampuni
hizo mbili.
Pia,
ilidaiwa kuwa Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi
za TBS zilizopo wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu
Ekerege alitumia madaraka yake vibaya.
Ilidaiwa
kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa punguzo la
asilimia 50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya baraza la
utendaji la TBS kinyume cha sheria namba 2 kifungu kidogo cha (3) ya TBS
ya mwaka 2005.
Ilidaiwa
kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za
Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. Milioni 68,068,800.
Upande
huo wa Jamhuri ulidaiwa shitaka la pili, katika tarehe na mahali pa
tukio la kwanza, mshtakiwa alilisababishia shirika kupata hasara ya
fedha hizo.
Charles
Ekelege akiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam leo ambapo
alihukumiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja baada ya kupatikana na
hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kulipa faini ya sh.milioni 68.
Hapa
Ekelege akiwa amekaa nje ya Mahakama hiyo na familia yake kabla ya
kuhukumiwa.
Ekelege akiteta jambo na familia yake akiwa Mahakamani hapo.
Askari polisi akiwa na familia ya Ekelege (wa pili kulia), wakati akitoka kwenye mahakama hiyo.