ALIYEKUWA
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba,
amesema ni vyema Bunge Maalumu la Katiba likasitishwa kwani Katiba bora
haiwezi kupatikana kwa muda wa wiki mbili.
Kauli
hiyo ya Jaji Warioba imekuja siku moja baada ya Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), kumtaka Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta,
kulisitisha, huku mwenyewe akisema litaendelea na hadi kufikia Oktoba 4
Katiba inayopendekezwa itapatikana.
Jaji
Warioba alieleza kushangazwa kwa haraka waliyokuwanayo wajumbe wa Bunge
hilo wakati wanajua kuwa Katiba haiwezi kupatikana kwa muda uliobaki.
Alisema
wiki mbili au tatu zilizobaki ni chache mno na kwamba Katiba mpya
haiwezi kupatikana, hivyo ni vyema sasa busara ikatumika kulisitisha.
“Mimi
sizungumzii kauli ya Ukawa, lakini natoa maoni yangu kwamba sidhani
kama watamaliza kwa kipindi hiki kifupi, kuna mambo hawawezi kupata kwa
muda huu mfupi.
“Ninachotaka
watumie tu busara waliahirishe… sijui haraka yao hii ni ya nini.
Kwanini wanashindwa kuelewa kuwa Katiba ni suala la maridhiano?” alihoji
Jaji Warioba.
Kwa
upande wake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Augustino
Ramadhani, alikataa kuzungumzia chochote juu ya suala hilo, akisema
tangu Rais Jakaya Kikwete alizindue Bunge hilo, alijitoa kuzungumzia
suala la Katiba.
“Kama
umefuatilia nilishajitoa tangu siku Rais Kikwete anazindua Bunge la
Katiba, nilijitoa kabisa, sitaki kabisa kuzungumzia Katiba tena,”
alisema Jaji Ramadhani.
Alipotakiwa kueleza sababu za yeye kujitoa kuzungumzia Katiba, alisema: “Ni uamuzi wangu.”
CHEYO NA UKAWA
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), John
Cheyo, alisema Bunge hilo haliwezi kusitishwa wala kuongozwa kwa matakwa
ya watu waliopo barabarani.
Akizungumza
wakati akichangia majadiliano ya jumla ya mchakato wa Katiba mpya,
alisema makubaliano yaliyofikiwa baina ya TCD na Rais Kikwete, ni
kuhakikisha Bunge hilo linapata Katiba mpya iliyopendekezwa na wananchi.
Cheyo alisema kuwa Bunge hilo linaendelea na kazi yake kwa mujibu wa sheria.
Alisema maandamano yanayotarajiwa kufanywa na vijana wa vyama vinavyounda Ukawa, hayatasaidia lolote.
Alielezwa
kushangazwa kwake na matamko ya Ukawa na kueleza kuwa ukweli wa kile
kilichojadiliwa upo kwenye video ambayo inaonyesha kila mmoja
alivyochangia majadiliano hayo.
“Katiba
itakayodumu ni ile ya maridhiano, lakini katika maridhiano haina maana
kwamba wanaokaa kuzungumza lazima wang’ang’anie upande wao.
“Wanaokaa
kuzungumza maana yake wanatafuta ni vitu gani ambavyo wanaweza
kuvizungumza, na ni vitu gani ambavyo vinaweza hata kuwekwa pembeni kwa
sasa, lakini baadaye vikaja kushughulikiwa kwa mazingira ya wakati huo,
hili tumejifunza tulipokuwa tunazungumza na Mheshimiwa Rais juu ya
mchakato wa Katiba na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Mheshimiwa
Rais amekuwa ni mfano mzuri wa kukubali kushauriana, na kama Katiba
tunavyoizungumza hapaswi hata kukubali, lakini amejiweka chini akakaa
kitako na viongozi wa TCD na viongozi wanaojiita Ukawa,” alisema Cheyo.
Aliongeza
kuwa katika mkutano wa kwanza uliochukua muda wa saa nne, majadiliano
yalikuwa ni namna gani Katiba itapatikana na Uchaguzi Mkuu utafanyikaje
na si vinginevyo.
Moja ya mambo yaliyokubalika ni Bunge la Katiba lipate Katiba inayopendekezwa na wananchi kama ilivyokusudiwa.
“Pia
tulikubaliana kwa hali halisi ya muda tulionao haiwezekani mchakato
mzima ukamalizika, na maana ya kumalizika mchakato ni kura ya maoni ya
wananchi na ndio wenye Katiba,” alisema.
Cheyo
alisema katika makubaliano hayo, viongozi wote waliafikiana kuwa awamu
ya Bunge Maalumu imalize kazi yake kama ilivyokuwa kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
“Bunge
hili haliendeshwi kwa amri ya mtu aliyepo barabarani, linaendeshwa kwa
mujibu wa sheria ambayo inasema uhai wa Bunge ni Oktoba 4, mwaka huu,
wote tulikubaliana,” alisisitiza Cheyo.
Alisema si rahisi Rais akurupuke na kuliahirisha Bunge hilo kwa shinikizo lolote kwa sababu sheria imeweka wazi ukomo wake.
Aliwataka
viongozi wa Ukawa kukubaliana na tamko alilolitoa mbele ya vyombo vya
habari, ambalo lilipatikana baada ya makubaliano.
Aidha
aliwataka wajumbe wenzake kujiamini na kwamba ripoti itakayotolewa na
Kamati ya Uandishi ndiyo itakuwa Katiba inayopendekezwa.
“Na
kwa sababu yoyote ile, huko nje kuna anayeamini vingine, anaweza
kuamini Serikali tatu, na haipo, mimi sitaki, anaamini Kadhi na haipo
hiyo ni shauri yako…,” alisema Cheyo.
TEC YAWASHANGAA UKAWA
Makamu
wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu
Severine Niwemugizi, alisema Ukawa walikuwa na kikao cha maridhiano na
Rais Kikwete, hivyo walikuwa na nafasi ya kumtaka asitishe Bunge.
Alisema
badala yake walitoka kwenye kikao hicho na kuanza kulalamikia wananchi
huku wakiwaambia waandamane ikiwa Rais Kikwete atashindwa kusitisha
shughuli hizo.
“Inashangaza
kuona Ukawa wanalalamika nje ya kikao wakati walikuwa na nafasi kubwa
ya kumwambia Rais Kikwete asitishe Bunge mara baada ya kumalizika kwa
kikao chao, badala yake wameamua kuja kwa wananchi na kuanza kulalamika.
“Kwani
katika hicho kikao hawakuwa na makubaliano? Na kama ni hivyo kwanini
walikubali kutumia Katiba ya mwaka 1977 kwa ajili ya Uchaguzi wa
Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani?” alihoji.
Alisema
katika kikao hicho Ukawa na Rais Kikwete waliingia makubaliano ya
kusitisha mchakato wa Bunge hadi mwaka 2016 ikiwa Rais ajaye atakubali
kuendelea nao.
“Nimewashangaa
sana wajumbe wa Ukawa, kwa sababu walikuwa na nafasi kubwa ya
kuwasilisha malalamiko yao kwa Rais na kuingia makubaliano ya kusitishwa
kwa shughuli hizo, lakini baada ya hapo wanakuja kwa wananchi na kuanza
kulalamika huku wakidai kuitisha maandamano, kwani hawakuwa na nafasi
ya kumwambia rais malalamiko yao,” alisema.
MBOWE
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, alisema hakuna sababu ya kuharakisha mchakato huo na
kuwa hata ikibidi baada ya miaka 100, Katiba bora itapatikana.
Alisema jambo muhimu ni Katiba kukidhi mahitaji ya Watanzania na izingatie maoni yao.
“Hatuwezi
kuvumilia kuona uchakachuaji wa fedha, unyanyasaji, na ukatili.
Yanayoendelea kwenye Bunge la Katiba ni unyama na wizi,” alisema Mbowe.
Taarifa hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam na na Rachel Mrisho, Dodoma.
No comments:
Post a Comment