Vigogo wa Baraza la Wanawake la Chadema
(Bawacha), watachuana katika kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa
baraza hilo baada ya jana baadhi ya wanawake kujitokeza kumchukulia fomu
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.Mbunge huyo
anaungana na Mbunge wa Viti Maalumu, Chiku Abwao na wanachama wengine,
Lilian Wasira na Sophia Mwakagenda ambao nao wamesharejesha fomu kuwania
nafasi hiyo inayoshikiliwa na Suzan Lyimo.Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Agosti 30 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Septemba 11, mwaka huu.
Wanawake
zaidi ya 30 kutoka Kinondoni, Kawe, Pwani na Ubungo jana saa 5.20
asubuhi, walifika katika ofisi za Bawacha jijini Dar es Salaam
kumchukulia fomu Mdee wanayedai kuwa ndiye anayestahiki kuliongoza
baraza hilo kutokana na msimamo wake wa uongozi wa kutotaka kuyumbishwa.
“Tumekaa
na kutafakari ili kumpata mwanamke atakayeweza kuliongoza baraza hili
kwa kututoa hapa tulipo na kutupeleka mbele zaidi, tumeona Halima Mdee
anatufaa zaidi ndiyo maana tumeamua kuja kumchukulia fomu,” alisema Felister Njau, Katibu Mwenezi wa Jimbo la Kawe.
Huku akishangiliwa na wenzake alisema, “Tunakwenda kumtafuta sehemu yoyote alipo ili tukamkabidhi hii fomu na tutamwomba akubali ombi letu.”
Msafara
wa wanawake hao wakiwa na fomu yao mkononi ukiongozwa na Mwenyekiti wa
Wazee Kata ya Kunduchi, Elefedina Mali ulikwenda makao makuu ya chama
hicho ambako walimkuta Mdee na kumkabidhi fomu hiyo.
Huku akibubujikwa na machozi, Mdee (pichani) alisema; “Nimewaelewa naombeni nikajitafakari kwanza, nitawaeleza nitakachoamua.” Wanawake hao pia walichangishana fedha Sh53,000 walizomkabidhi Mdee kwa ajili ya kurejeshea fomu hiyo.
No comments:
Post a Comment