Tuesday, October 14, 2014

KILIMO BORA CHA MANANASI KIMEBADIRI MAISHA YA WANAWAKE WA KIWANGWA NA FUKAYOSI WILAYANI BAGAMOYO.



Japokuwa kumekuwa na dhana ya kwamba mkulima ni mtu maskini na asiyeweza kufanya shughuli nyingine ya maendeleo, lakini kwao UFUMAKIFU wanajiuliza walikuwa wapi kufanya kilimo hiki tangu siku nyingi.
Akiongea na mwandishi wa habari Bi Farida Mrisho Pyara, mwenyekiti wa kikundi cha UFUMAKIFU (Umoja wa wanawake Kiwangwa na Fukayosi) alisema kuwa kilimo cha mananasi kimekuwa mkombozi kwao kwani tangu walipoanza kujishughulisha na kilimo hicho kama kikudi maisha ya wanakikundi wengi yamebadirika kutoka katika hali duni na kuwa bora zaidi.
Kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2012 na shirika la DotAfrika kwa madhumuni ya kuwakwamua wanawake kimaendeleo katika kazi zao, kina wanawake zaidi ya 50 wa umri tofauti tofauti. Walianza kwa kuwa na shamba la pamoja ambalo walilima wanachama wote kwa kupanda mbegu mpya kutoka chuo cha SUA ambazo walipewa na shirika hilo kama msaada.

Hata hivyo mwenyekiti huyo alidai kuwa baada ya kulima kama kikundi lakini lilikuwa ni darasa tosha kwao kwani walijifunza mambo mengi mapya ya jinsi ya kulima kilimo bora  na kutumia mbegu bora za mananasi kwa kupata mavuno bora kwa manufaa zaidi.

 Bi farida alisema shamba hilo ambalo lilikuwa kama ni shamba darasa kwao liliwapa mafunzo ambayo kwa sasa kila mwanakikundi ana shamba lake na analima kwa kutumia ujuzi uleule walioupata hapo awali na kila mmoja amefunguka na kutambua kuwa walikuwa wanadharau kilimo kwa kuwa walikosa elimu ya kutosha, ni jinsi gani wanaweza kufanya kilimo chenye manufaa kwao.
“Wanawake wengi tulikuwa tunafanya biashara ndogo ndogo huku tukiwaachia wanaume kwenda mashambani peke yao, matokeo yake wengi wetu tulibaki kuwa tegemezi na inakuwa hali mbaya zaidi ikitokea mwanaume kafariki. Lakini tangu tumeanza kikundi hiki wengi wetu tuna mashamba yetu binafsi ambayo hutupatia kipato cha kutosha” alisema Bi Farida. 
Hata hivyo alisema mpaka sasa kila mwanachama anashamba lake ambalo analilima mwenyewe kama shamba darasa, na iwapo wanapata  tatizo linalohitaji ufumbuzi wanae Afisa kilimo Bwana Amir Abdul ambaye amekuwa msaada mkubwa sana kwao kwani ndiye anayewapa elimu ya kilimo kila wanapohitaji elimu hiyo.



Nae Bi Halima Muhamed Athumani (58) mjumbe wa UFUMAKIFU alisema elimu waliyopewa ni bora na isiyo ya gharama katika kufanikisha kilimo hicho.
“Tumeletewa mbegu za mananasi isiyokuwa na magonjwa yaliyokuwa yanatusumbua kipindi cha nyumaa, na tumejifunza njia ya kulima bila kulichosha shamba wakati huo huo tunazuia matunda yasiharibiwe na jua kwa kupanda mazao mawili shambani yaani mananasi na migomba pamoja, wakati huo huo tunarutubisha shamba kwa kuchoma masalia ya nanasi shambani baada ya kuvuna kitu ambacho  tulikuwa hatukijui hapo awali”. Alisema Bi Halima
“Siku hizi huwa tunaweka mbolea ya DAP na UREA kwa ajili ya kukuzia na hatutumii dawa ya aina yoyote kuzuia magonjwa kwani mbegu hii haina usumbufu huo. Na pia mbegu hii inawahi kukomaa.”
Aliendelea kwa kusema mbegu hii ni nzuri kwa kuwa hainyauki tunda wala kuozea shambani na inatoa mazalia bora pia ambayo huwa yanakuwa ni mbeyu kwa ajili ya kupatwa msimu mwingine nah ii ni tofauti na mbegu tulizokuwa nazo siku za nyuma

 Kikundi hicho ambacho kwa sasa kimeamua kulima kilimo cha kisasa kwa ajili ya kuondoa umaskini majumbani mwao, wameamua kwenda mbali zaidi kwa kufanya biashara ya mananasi nje ya nchi na mikoa ya mbali kwa kuyasindika mananasi na kuyasafirisha.
“Hivi saasa tumejenga makaushio (dryer) kwa ajili ya kukausha mananasi na kuyahifadhi vizuri kwenye mifuko tayari kwa kuyapeleka sokoni ili kuwa na tija zaidi. alisema Mwenyekiti huyo

Bi Farida akiwa ndani ya makaushio (dryer) akitoa maelezo jinsi kipima joto kinavyofanya kazi

Kilimo cha nanasi kinastawi zaidi katika ukanda wa nchi za joto na kwenye udongo usituamisha maji. Hapa Tanzania zao hili linastawi sehemu nyingi lakini kwa wingi linastawi mikoa ya Pwani, Morogoro, Shinyanga Tanga Mtwara Lindi na Bukoba. Katika mkoa wa pwani, zao hili linalimwa katika wilaya ya Bagamoyo, Mkuranga Kibaha na Kisarawe. Kwa Bagamoyo linalimwa zaidi katika kata ya Kiwangwa na maeneo ya Gongo.
Zao hili lina kiasi kikubwa cha vitamini A na B na kiasi kidogo cha vitamini C, pia kuna madini kama potasiam, kalsiam, chuma na magnesiam
Nanasi huliwa baada ya kumenywa ganda la nje na pia hukamuliwa maji yake na kunywa kama juisi.Nanasi pia linaweza  kuanikwa na kukaushwa ambapo huliwa kwa kutafunwa. Nanasi pia baada ya kukauka husagwa na unga wake hutumika kutengeneza juisi au kuchanganywa katika vilaji vingine kama vile Pizza nk


No comments:

Post a Comment