Tuesday, October 7, 2014

MWIZI AUAWA MBEYA BAADA YA KUVUNJA DUKA NA KISHA KUIBA


Mtu mmoja mkazi wa Itewe wilaya ya Mbeya Vijijini aliyefahamika kwa jina la Jacob Kimaila (31) ameuawa baada ya kupigwa na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi kutokana na tuhuma za kuvunja duka, salon na kuiba.
Mtuhumiwa alifariki mnamo tarehe 05.10.2014 majira ya saa 09:30 asubuhi huko katika kituo cha afya Inyala, kata ya Inyala, tarafa ya Tembela, wilaya ya Mbeya vijijini, mkoa wa Mbeya. Inadaiwa kuwa, chanzo cha kifo chake ni  kutokana na majeraha aliyoyapata kutokana na kupigwa na wananchi siku ya tarehe 04.10.2014 majira ya asubuhi.
Jitihada za kuwatafuta waliohusika katika tukio hili zinaendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya Inyala alipokuwa anapatiwa matibabu.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake wawafikishe katika mamlaka husika watuhumiwa wanaowakamata kwa tuhuma mbalimbali kwa hatua zaidi za kisheria.

No comments:

Post a Comment