
Kwa mujibu wa WHO na mamlaka za afya za Uganda, matokeo ya uchunguzi
katika maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Virusi kufuatia kifo cha tabibu
huyo tarehe 28 Septemba yanathibitisha kwamba alifariki kutokana na homa
hiyo hatari ya Marburg. Waziri wa Afya wa Uganda, Erioda Tumwesigye,
alisema kuwa wizara yake inathibitisha daktari huyo aliyekuwa mtaalamu
wa vipimo vya mionzi, alikufa kwa Marburg.
Marehemu alikuwa tabibu katika Hospitali Kuu ya Wilaya ya Mpigi na
alianza kuugua tarehe 17 Septemba akihudumu katika hospitali ya Mengo
jijini Kampala, ambako alikuwa ameajiriwa mwezi mmoja uliopita.
Inahofiwa kwamba katika kipindi cha wiki mbili kabla ya kifo chake
alikutana na watu wengi wakiwemo matabibu wenzake pamoja na kwamba ni
jamaa zake waliomzika.
Kutokana na hilo, mwakilishi wa WHO nchini Uganda, Dokta
Wondimagegnehu Alemu, alitahadharisha watu watu wanaoingia nchini
Uganda, hasa katika wilaya ya Mpigi iliyo jirani na jiji la Kampala na
pia Kasese alikozikwa marehemu. "Tunatoa tahadhari ya usafiri nchini
Uganda baada ya kutambua kwamba mtu mmoja amefariki kutokana Marburg,"
alisema mwakilishi huyo ya WHO.
Watu 80 wawekwa kwenye karantini.
Wizara ya afya ya Uganda pamoja na mashirika na taasisi nyengine
husika zimechukua hatua za dharura mkiwemo kuwabaini na kuwatenga zaidi
ya watu wapatao 80 waliokutana na mtu huyo aliyefariki kutokana na
ugonjwa huo hatari wa Marburg.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, watu hao watachunguzwa katika kipindi cha
siku 21, ambazo ndiyo muda wa ishara za ugonjwa huo kujitokeza na
kubainika na "yule atakayeonesha dalili hizo atasafirishwa moja kwa moja
hadi kituo cha kitaifa cha kushughulikia magonjwa hatari," alisema
Daktari Jane Aceng, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Afya nchini
Uganda, akiongeza kwamba wanafanya kila jitihada kuona kwamba
wanamfuatilia kila mtu na "kuudhibiti ugonjwa huo mara moja kabla
haujasambaa".
Popo husababisha Marburg
Ugonjwa wa Marburg ni homa hatari inayonasibishwa na ugonjwa wa Ebola
kwani virusi vya magonjwa hayo ni ya jamii moja ijulikanayo kama
filoviridae.
Mnyama aina ya popo, ambao ni jamii ya mamalia wanaoruka na wanaoishi
kwa kula matunda, ndiyo wanaosemekana kusambaza kirusi cha Marburg na
maambukizi baina ya binadamu hutokana na kugusana kwa vidonda au
majimaji yoyote kutoka kwa mgonjwa kama vile damu, mate, matapishi,
kinyesi au mkojo wa aliyeambukizwa.
Jamii nyingi za watu wa Uganda, Kongo na eneo la kati ya Afrika, hula
nyama ya popo kama kitoweo au hasusa ya kusindikizia ulevi.
Miongini mwa dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtu kuwa na homa ya
ghafla ya kiwango cha juu cha joto, maumivu ya kichwa, kutapika damu,
maumivu ya viungo na misuli pamoja na kuvuja damu kutoka sehemu kadhaa
kama vile machoni, puani, meno, masikioni, njia ya haja kubwa na hata
kwenye ngozi. Aidha mtu aliyekumbwa na ugonjwa huo huharisha sana.
Kwa bahati mbaya, kama ilivyo kwa Ebola, ugonjwa huo nao haujapatiwa
dawa maalum ya kuutibu wala chanjo dhidi yake. Wagonjwa hupewa tu dawa
za kutuliza ishara husika.
Wataalamu wanaelezea kuwa viwango vya uwezekano wa mtu kufariki
kutokana na ugonjwa huo ni kati ya asilimia 24 hadi 88, huku
wakisisitiza njia za kujilinda na mgonjwa aliyekwishaathirika kuepuka
kukutana kwa majimaji ya miili, damu, kinyesi au mate.
No comments:
Post a Comment