Askofu Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria anayehusishwa na biashara ya madawa ya kulevya.
Vigogo wa madawa ya kulevya wakiwemo viongozi wa dini sasa wanaanza
kupukutika kutoka kwenye mstari wa siri huku baadhi yao wakikimbilia nje
ya nchi kufuatia oparesheni kali inayofanywa na Kikosi cha Kupambana na
Kudhibiti Madawa ya Kulenya Tanzania kuwanasa kila kukicha. Hivi karibuni kikosi hicho kimemkamata askofu
(mwangalizi mkuu wa kanisa) aliyetambulika kwa jina la Emeka Nwachukwu
Mert raia wa Nigeria ambaye ana kanisa la kiroho maeneo ya Sinza jijini
Dar.
Jina la kanisa hilo limedhibithiwa na vyombo husika kwa sababu ya uchunguzi zaidi na uhalali wake wa kuwepo nchini.
Vyanzo vyetu makini ndani ya kikosi kazi vinaeleza kwamba, mchungaji
huyo alikamatwa Oktoba 31, mwaka huu saa kumi usiku Tegeta wilayani
Kinondoni, Dar es Salaam akiwa na madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya
heroine kilo 35.
Habari za ndani kutoka kwenye oparesheni hiyo zinasema kuwa, endapo
unga huo ungeingia sokoni na kununuliwa, basi mtumishi huyo wa Mungu
angevuna kitita cha zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Mchungaji huyo ambaye serikali imeanza kazi ya kulichunguza kanisa
lake, alidakwa na mzigo huo haramu kwenye makazi aliyopanga ambayo ni
nyumba ya profesa mmoja wa chuo kikuu, Mbezi jijini Dar es Salaam.
Askofu akiwa chini ya ulinzi.WASHIRIKA NAO WADAKWA
Kwa mujibu wa chanzo, kamatakamata ya mchungaji huyo pia iliwakumba
watuhumiwa wengine ambao ni Walyat Khan raia wa Pakistani, Chuksi
Sylvester Agbazuo na Tony Olafor wote raia wa Nigeria na inadaiwa kwamba
walikuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali na kutoroka.
a
Habari za siri ambazo Uwazi ilizinasa zinadai kuwa, watumishi wa
Mungu waliokuwa kwenye orodha ya kunaswa walikuwa wengi lakini
wamekimbilia nje ya nchi na kikosi hicho kimeshawasiliana na Polisi wa
Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kuwasaka na kuwatia nguvuni.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, Kamanda wa Polisi Kitengo cha
Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa
amekabidhiwa majina ya vigogo wakiwemo viongozi wa dini ambao ni sugu
katika biashara hiyo. Mbali na majina hayo, pia amepewa ratiba zao za
safari za kibiashara hivyo kilichobaki ni kuwafuatilia na kuwakamata na
ushahidi ili kuhakikisha kwamba hawawezi kupona mahakamani.
Habari zaidi zinadai kuwa, siku za hivi karibuni, Kamanda Nzowa
amekuwa akifumua mtandao wa watu wazito katika biashara hiyo na
imebainika kuwa vigogo hao wana mtandao mkubwa serikalini ikiwemo wizara
ya mambo ya ndani ambao wanawalinda kwa kupewa mamilioni ya pesa kwa
ajili ya usimamizi wa upitishwaji wa biashara hiyo haramu kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar.
“Unajua zamani viongozi hao serikalini walikuwa wakimsumbua Kamanda
Nzowa ili awaachie watuhumiwa waliokamatwa na unga bila mafanikio,
lakini sasa wameshamsoma kiasi kwamba hata wakikamatwa hawampigii simu
tena,” kilisema chanzo kingine.
Dawa za kulevya alizokutwa nazo askofu huyo.
Habari nyingine zinadai kuwa, Kamanda Nzowa pia ana majina ya watoto
wa vigogo wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo na anayafanyia
kazi.
Kukamatwa kwa askofu huyo kumekuja baada ya kukamatwa kwa vigogo ambao ni viongozi wa dini katika makanisa ya kilokole.
Januari 11, mwaka huu, Askofu Moris Charles alidaiwa kukamatwa na
polisi maeneo ya Chinga Mbili mkoani Lindi akiwa na kilo 210 za madawa
ya kulevya aina ya heroine yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4, kesi
yake bado inaendelea mahakamani mkoani humo. Juni 8, 2011 polisi
walifanikiwa kumkamata Mchungaji Kapupu Denis Okechuku wa kanisa la
kilokole lililopo Kinondoni Biafra akiwa na kilo 81 za cocaine, kesi yao
bado ipo Mahakama ya Kisutu, Dar.
Nyumba aliyokutwa askofu huyo.
KAMANDA NZOWA
Kamanda Nzowa ofisini kwake juzi, alisema kuna
watu wanne waliokamatwa Tegeta wakiwa na kilo 35 za madawa ya kulevya
aina ya heroin na kuna wengine wanatafutwa kuhusiana na tukio hilo.
“Kwa sasa nisingependa kuzungumzia sakata hilo kutokana na sababu za
kiupelelezi kwani kuna wengine tunawatafuta na nitahakikisha wanakamatwa
na kufikishwa katika vyombo vya sheria, nawashukuru wananchi kwa
ushirikiano wao,” alisema Nzowa.
No comments:
Post a Comment