Harbinder ambaye ni singasinga anatajwa pia akidaiwa kuwa
mfanyabiashara tapeli kufuatia vitendo vyake mbalimbali katika kumiliki
makampuni na ukwepaji wa kodi ya serikali.Unamju Ni mfanyabiashara bilionea mwenye asili ya Bara
la Asia na mmiliki wa mtambo wa kufua umeme wa Kampuni ya Independent
Power Tanzania Limited (IPTL) ambayo hivi karibuni imezua tafrani Bongo
kufuatia kampuni yake kuhusishwa na uchotwaji wa fedha kiasi cha Sh.
Bilioni 306 kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Harbinder anatajwa na vyanzo kwamba ni mzaliwa wa Mkoa wa Iringa.
Mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 20 ya kuzaliwa na nduguze wawili, Nota
Singh na Manjit Singh walianzisha kampuni ya ujenzi wa barabara
iliyojulikana kwa jina la Ruaha Concrete Co. Ltd ikitumia SLP 498,
Iringa. Ruaha ni sehemu maarufu kwenye Manispaa ya Mji wa Iringa kukiwa
na vitongoji vya Ipogoro, Kibwabwa na Ndiuka. Jina la Ruaha linatokana
na Mto Ruaha kupita eneo hilo.
Vyanzo vinasema, Harbinder alianza kumiliki fedha nyingi kuanzia
miaka ya 80 wakati familia ya Rais wa Kenya wakati huo, Daniel Arap Moi
ilipoanza kujiingiza kwenye biashara mbalimbali.
Vyanzo vikadai kuwa, miaka hiyo, singasinga huyo alihamia jijini
Nairobi, Kenya ambako alianza kuwa mshirika wa kibiashara na mtoto wa
kwanza wa Rais Moi aitwaye Gideon Moi.
Akiwa nchini humo, vyanzo vinamtaja singasinga huyo kuwa alipata
umiliki wa mtambo wa Westmont wa kuzalisha umeme wa megawati 47 jijini
Mombasa.
Washirika wenzake katika mradi huo walikuwa Mukesh Gohil, Kamlesh Pattni, Gichuru na Mkurugenzi Mtendaji wa KPLC, Mutitu.
Singh pia anatajwa kuwa na miradi 74 iliyofungwa katika maeneo
mbalimbali ya Afrika Mashariki kutokana na kuvurunda kama siyo kufanya
vibaya.
Mwaka 1997, Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Mashirika Kenya ilianika
udhaifu wa Ruaha Concrete katika tenda ya ujenzi wa barabara ambako
kulikuwa na ucheleweshaji, kuongezeka kwa gharama pamoja na utekelezaji
hafifu uliojitokeza.
Kufuatia madai hayo, ilibidi mhandisi msimamizi wa mradi huo
aliyetajwa kwa jina moja la Kitololo ajiuzulu baada ya kukataa kutia
saini kuwa kazi iliyozembewa imekamilika.
Haikujulikana mara moja ni mwaka gani alirejea Bongo, lakini ilidaiwa
kuwa tayari alishawekeza nchini huku akiwa bado ana biashara zake Kenya
na baadaye alirudi jumla kutokana na misala ya kule.
Singh anatajwa kuwa mfanyabishara tapeli kufuatia Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) kumtaja kuwa amehusika na vitendo vya ukwepaji
wa kodi akitumia mbinu za ujanjaujanja.
Mfano mkubwa ni hizo bilioni 306 alizochota kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow hakuzilipia kodi na ndiyo maana Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu
Nchemba akihutubia bunge mjini Dodoma, Ijumaa iliyopita katika mjadala
huo aliamuru kodi hiyo ilipwe mara moja.
Lakini pia kwa mujibu wa TRA na Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG), jamaa huyo amekuwa na tabia ya kuuza hisa kwa bei ya
chini kwa makampuni mengine ili aweze kulipa kodi ndogo jambo ambalo pia
ni kuonesha ni mfanyabiashara tapeli.
Kamati ya Zitto Kabwe ambaye ni mwenyekiti wa PAC, pia ilibaini kuwa,
wakati yeye alijulikana kuwa ndiye mmiliki wa Kampuni ya IPTL ambayo
baadaye aliiuza kwa Pan African Power Solutions Limited (PAP), uchunguzi
wa PAC ukaja kubaini kuwa, mwenye PAP ndiyo huyohuyo mwenye IPTL, yaani
singasinga huyo. Dah!
Kwa mara ya kwanza katika historia ya Bongo, Ijumaa iliyopita bunge
liliendeshwa hadi saa 5:00 kasoro usiku, ishu ikiwa ni kujadili
yaliyotokana na Kamati ya PAC baada ya kuchunguza wizi wa mabilioni ya
shilingi kutoka Escrow kwenda IPTL kwa kupitia PAP.
Baadhi ya mawaziri na vigogo serikalini ambao wengine walimwaga
machozi kutokana na kashfa waliyoipata kupitia Kampuni ya IPTL
hawatamsahau singasinga huyo kwa vile amewaingiza kwenye kumbukumbu
mbaya ya Taifa la Tanzania. Katika listi ya viongozi hao yumo Mizengo
Pinda, Profesa Sopspeter Muhongo, Stephen Masele, Eliakim Maswi, Jaji
Feredrick Werema na wengine wengi.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, Spika wa Bunge, Anne Makinda
aliliahirisha bunge hadi Januari, mwakani katika kikao cha 18 bila
kumwadhibu mtu juu ya sakata hilo.
No comments:
Post a Comment